WAZIRI MKUU: KILA MKOA UUNDE KAMATI YA AMANI
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika futari aliyoiandaa kwenye
makazi yake mjini Dodoma Juni 15, 2016. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa
mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa na Wapili kushoto ni Kaimu Sheikh
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Ahmed Said.Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Muungano na mazingira, January Makamba.(Picha na ofisi
ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Makamu Mwenyekiti Mstaafu, John
Malecela katika futari aliyoiandaa kwenye makazi yake mjini Dodoma Juni
16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Ulanga, Goodluck
Mlinga katika futari aliyoiandaa kwenye makazi yake mjini Dodoma Juni
15, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba katika futari aliyoianda
kwenye makazi yake mjini Dodoma Juni 15, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Spika wa Bunge Dkt.
Tulia Ackson katika fuatari aliyondaa kwenye makazi kake mjini Dodoma
Juni 15, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema kila mkoa unatakiwa kuunda Kamati ya Amani kama njia ya
kudumisha amani na utulivu kwenye mikoa yote nchini.
Waziri Mkuu ametoa wito huo jana
usiku (Jumatano, Juni 15, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa dini
wa mkoa wa Dodoma na baadhi ya wazee maarufu wa mkoa huo aliowaalika
kwenye futari katika makazi yake mjini Dodoma.
Amesema anatambua kuwa mkoa wa
Dodoma uko shwari kwa sababu ya mshikamano uliopo baina viongozi wa dini
za Kiislamu na Kikristo. “Nimegundua kuwa siri kubwa ya mkoa wa Dodoma
kuwa na utulivu ni kuwepo kwa kamati ya amani yenye viongozi mahiri,
kwani sote tunatambua kuwa kazi ya viongozi wa dini ni kuwaimarisha watu
kiroho,” alisema.
Waziri Mkuu alisema ziko nchi
zinatamani kuwa kama Tanzania kwa sababu wao hawana uhakika wa kulala na
kuamka salama asubuhi. “Pamoja na yote sisi tuna uhakika wa asilimia 99
kulala usiku na kuamka salama asubuhi, kwa sababu ya amani iliyopo,”
alisema.
Hadi sasa mikoa ambayo
imekwishaunda kamati za amani ni Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Dodoma,
Arusha, Lindi, Mtwara, Tanga na Mbeya.
Akigusia suala la mauaji ya hivi
karibuni, Waziri Mkuu alisema anawaomba Watanzania kila mmoja kwa imani
yake akemee kwa nguvu matendo hayo kwa sababu yeye haamini kama
yamefanywa na Watanzania ambao wamelelewa kwenye misingi ya dini.
“Siamini kama kuna mtoto
aliyelelewa kwenye misingi ya Uislamu anaweza kuingia msikitini na
kuwaua wenzake wakati wakimwomba Mungu. Na wala siamini kama kuna mtoto
aliyelelewa na kukuzwa Kikristo anaweza kuingia kwenye nyumba ya ibada
akakuta watu wanasali na kuamua kuwaua. Ninawaomba tukemee kwa nguvu
zote tabia hii,” alisisitiza.
Aliwataka watanzania wote wawe na
walinzi wa wenzao kwa sababu kila mmoja ana jukumu la kumlinda
mwenzake. “Tusiachie majeshi kazi hii kwa sababu kila mmoja na jukumu la
kwanza kujilinda yeye mwenyewe na kisha kumlinda jirani yake,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Sheikh wa
Mkoa wa Dodoma, Sheikh Ahmed Said alisema wanawaombea dua Mheshimiwa
Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika kazi za kuleta maendeleo kwa
Watanzania. “Pia tutaendelea kuiombea nchi yetu ili Mwenyezi Mungu
azidishe amani yake na watu wake waishi kwa amani, upendo na utulivu,”
aliongeza.
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Dk.
John S. Malecela ambaye alikuwa miongoni mwa wazee maarufu walioalikwa
kwenye futari hiyo aliwataka waalikwa wenzake waendelee kuwaombea
viongozi wa kitaifa na kusisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuombea
amani ya Tanzania ambayo imedumu kwa miaka mingi iendelee kuwepo.
Katika hatua nyingine, Askofu wa
Kanisa la Mennonite Tanzania Dayosisi ya Kati, Askofu Amos Muhagachi,
ambaye alipewa fursa ya kutoa salamu fupi kwenye hafla hiyo, alisema
kwenye mkoa huo hakuna magomvi ya kidini kwa sababu viongozi wa dini
zote wanashirikiana kwa karibu sana.
“Hapa Dodoma Maaskofu
tunashirikiana vizuri na Masheikh. Hivi sasa, masheikh vijana na
wachungaji vijana wameanza kuiga haya tunayofanya, na zaidi ya yote
tunashirikiana pia kuwaombea Rais wetu, Makamu wa Rais pamoja na wewe
Mheshimiwa Waziri Mkuu,” alisema
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni