Bunge limepitisha muswada wa marekebisho ya Sheria ya Elimu
———————————————-
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Bunge la Jamhuri wa Muungano wa 
Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria 
ya Elimu kifungu kinachoeleza kuwa mtu anayempatia ujauzito mwanafunzi 
wa shule ya msingi au sekondari kuwa adhabu yake ni faini isiyozidi 
shilingi laki tano au kifungo kisichozidi  miaka mitatu.
“Muswada unapendekeza kuwa kifungu
 hicho kifutwe na badala yake kitungwe kifungu kipya cha 60A ili kuweka 
masharti yanayojitosheleza kuhusu zuio la kuoa au kumpatia ujauzito 
mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari, kinapendekeza adhabu yake 
iwe kifungo cha miaka 30 gerezani,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa 
Serikali Mhe. George Masaju.
Vile vile mtu atakayebainika 
kusaidia, kushawishi au kuacha mwanafunzi wa shule ya msingi au 
sekondari kuolewa au kuoa anatenda kosa la jinai ambalo adhabu yake ni 
faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano 
gerezani au vyote kwa pamoja.
Mhe. Masaju aliendelea kwa 
kufafanua kuwa, sheria hiyo imependekeza kuwa pale ambapo kosa hilo 
litafanywa na mtoto basi adhabu yake itakuwa kwa mujibu wa masharti ya 
sheria ya mtoto. Hii ni kwa sababu sheria ya mtoto inakataza mtoto 
anayetiwa hatiani kufungwa gerezani.
Aidha marekebisho hayo katika 
sheria ya Elimu yanalenga kumjengea mwanafunzi wa shule ya msingi au 
sekondari mazingira mazuri ya kumaliza ipasavyo elimu yake kwa ngazi 
hiyo.Hivyo basi kila Mkuu wa shule au Mwalimu Mkuu atawasilisha kwa 
Kamishna wa Elimu taarifa ya robo mwaka kuhusu matukio ya ndoa na mimba 
kwa wanafunzi katika shule yake na hatua zilizochukuliwa.
Sheria ya Elimu inamruhusu 
mwanafunzi aliyepewa ujauzito kuendelea na masomo mara tu anapojifungua.
 Sheria hiyo inasubiri kuwekwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ili ianze kutumika.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni