Mh. Herman Kapufi aipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.
Na Hassan Silayo
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Same
Mh. Herman Kapufi ameshukuru Jitihada zinazofanywa na Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA) katika kutekeleza miradi inayosaidia kuongeza ubora wa
elimu nchini ikiwemo utekelezaji wa mradi kukarabati shule kongwe nchini
utakaoboresha mazingira ya kufundishia na kusaidia kuinua kiwango cha
elimu katika shule hizo.
Mh. Kapufi amesema kuwa mpango
huo umekuja wakati muafaka wakati uongozi wa wilaya hiyo ukipambana
kutatua changamoto za elimu na kuwataka wadau kuipa ushirikiano Mamlaka
hiyo.
“Kwa kweli napenda kuishukuru
Mamlaka ya elimu Tanzania kwa jitihada zake hizi za kuboresha sekta ya
elimu nchini, kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana katika wilaya hii kwa
kipindi chote nilichokuwa hapa kama mkuu wa wilaya, shule zetu kongwe
zimechoka sana na zinahitaji ukarabati ili kuweza kuzirudisha katika
hali yake ya kawaida kwa utekelezaji wa mpango huu” Alisema Mh.Kapufi.
Naye Meneja Mawasiliano na
Uhusiano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Bibi. Sylvia Lupembe amesema kuwa
kupitia TEA mpango huo utatekelezwa katika shule kongwe 11 katika mikoa
ya Bukoba, Mwanza, Tabora, Singida, Same, Arusha, Dodoma, Morogoro na
Pwani kwa kuzifanyia ukarabati wa miundo mbinu mbalimbali ikiwemo
madarasa, vyoo, maabara, mabweni na mifumo ya umeme.
“hali ya shule zetu kongwe kwa
kweli sio nzuri tumetembea kwenye mikoa takribani Mikoa sita tumejionea
halihalisi ya miundombinu ya shule zetu kongwe hazipo katika mazingira
mazuri ya kujifunzia kutokana na kuwa na miundombinu chakavu na kwa
mradi huu tunataka kuweka mazingira mazuri ya watoto wetu hawa
kujifunzia hasa kwa kuanza na shule hizi kongwe” Alisema Sylvia.
Wakizungumzia ukarabati huo
Mwalimu Mkuu wa shule wa Shule ya Sekondari Nganza Bi. Yacinta Lyimo
aliishukuru Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa Utekelezaji wa mpango
huo kwani utasaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na hata kusaidia
kuinua kiwango cha elimu na ufaulu katika shule hizo.
Aidha, Afisa Elimu wa Manispaa ya
Singida Bw. Omari Kisuda Mpango huu wa maboresho ya shule kongwe ni
mkombozi katika sekta ya elimu na umekuja wakati uhitaji wa maboresho ya
shule hizo unahitajika hasa kutokana na baadhi ya shule kushindwa
kufanya ukarabati wa mara kwa mara kutokana na ufinyu wa bajeti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni