Jumatatu, 27 Juni 2016

Maombi Maalumu Kwa Ajili ya Kumuombea Rais Magufuli na Tanzania Katika Kanisa la IEAGT Shinyanga

Hapa ni ndani ya kanisa la The International Evangelical Assemblies Of God –Tanzania (IEAGT) lililopo katika kata ya Kambarage katika manispaa ya Shinyanga ambapo leo Jumapili Juni 26,2016 kumefanyika Maombi Maalumu kwa ajili ya taifa la Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli,makamu wa rais,bunge,mahakama,polisi na viongozi mbalimbali wa serikali.
—————————————————–
 
Maombi hayo yameongozwa na askofu wa kanisla la (IEAGT) David Elias Mabushi na kuhudhuriwa na kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Josephine Matiro ambaye ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga.
Maombi hayo pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali,vyama vya siasa,mashirika,waandishi wa habari,wageni mbalimbali na waumini wa kanisa hilo.
Pamoja na maombi hayo maalumu, Kanisa hilo  limeadhimisha siku ya watoto katika kanisa hilo ambapo pia Juni 26 ni siku ya kuzaliwa kwa askofu wa kanisa la IEAGT David Mabushi ambaye leo ametimiza umri wa miaka 53.
Sambamba na matukio hayo mawili makubwa,kanisa hilo pia lilikabidhi madawati 20 kwa uongozi wa wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kumuunga mkono rais Magufuli katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa changamoto ya madawati inamalizika katika shule.
Awali akisoma risala,Katibu wa kanisa la IEAGT, Mchungaji Obed Jilala alisema baada ya uchaguzi mkuu 2015,kanisa la IEAGT limekuwa likisikia kwa nyakati tofauti rais Magufuli akiomba maombi kwa ajili ya kazi yake ya kuliongoza taifa,hivyo kanisa lao limeguswa sana na kauli hiyo na katika kuonesha wanamuunga mkono walikubaliana siku ya Jumapili Juni 26,2016 iwe ya maombi maalumu kwa ajili ya kiongozi wa taifa sambamba na kuliombea nchi ya Tanzania.
“Maombi haya yamebebwa kwa kiasi kikubwa na upendo tulio nao kwa nchi yetu ,kanisa la IEAGT kama sehemu ya jamii ya watanzania tumeona siku ya leo iwe kilele cha maombi ya kitaifa katika mkoa wetu na mahali popote lilipo kanisa letu”,aliongeza Mchungaji Jilala.
Naye Askofu wa kanisa hilo David Mabushi akitoa mahubiri yake,mbali na kumpongeza rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa rais,alimuomba kuendelea kuonesha msimamo wake katika kuwaletea maendeleo watanzania huku akimfananisha na Nabii Musa akisema Magufuli amekuja kuiokomboa nchi na kuifanya kuwa nchi ya asali na maziwa.
“Tumeandaa siku hii muhimu kwa ajili ya kuiombea nchi yetu ili iendelee kuwa na amani,tunamuombea rais wetu kwa sababu wenye haki wakiwa na amri,watu hufurahi..sisi kama kanisa tutahakikisha tunamuunga mkono rais Magufuli kwa maneno na vitendo ndiyo maana leo tunatoa sadaka ya madawati 20,tunaomba watanzani waendelee kumuombea rais wetu aliyeonesha kuwajali watanzania tangu alipoingia madarakani amekuwa mstari wa mbele kupigana dhidi ya rushwa na vitendo vyote viovu”,aliongeza askofu Mabushi.
Kwa upande wake mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa mkoa wa Shinyanga ,Josephine Matiro ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro,alilipongeza kanisa hilo kuona umuhimu wa kuombea viongozi wa nchi na kuongeza kuwa kanisa la IEAGT ni kanisa la kwanza mkoani Shinyanga kufanya maombi kwa ajili ya viongozi wa nchi.
“Ndugu zangu watanzania naomba tuendelee kuiombea nchi ili iendelee kuwa ya amani na viongozi kuwa na hofu ya mungu,lakini pia naomba watanzania wafanye kazi,sasa ni muda wa kuchapa kazi tuache siasa za majukwaani,tumuunge mkono mheshimiwa rais katika kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi tu”,aliongeza Matiro
Continue reading →

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni