TIMU YA BUNGE YAHAMASISHA WADAU KUCHANGIA MADAWATI.
…………………………………………………………………………………………………………..
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania wameandaa mechi maalum kwa ajili ya kuchangia 
madawati shule za msingi na sekondari, ili kuunga mkono Serikali ya 
awamu ya Tano kutatua kero ya upungufu wa madawati Nchini.
Mwenyekiti wa Timu ya Bunge 
(Bunge Sports Club) Mhe. William Ngeleja ameyasema hayo leo Mjini Dodoma
 katika mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akiitambulisha kamati 
 itakayoratibu mchezo huo.
Aidha mechi kama hizo zimekuwa 
zikiandaliwa kila baada ya kuahirishwa kwa Bunge na kuhusisha mpira wa 
miguu kati ya wabunge ambao ni wanachama na wapenzi wa timu ya Simba kwa
 upande mmoja na wale wa Yanga kwa upande mwingine.
“Mashindano yatakayofanyika mwaka
 huu ni kwa ajili ya kupata madawati mengi kadri itakavyowezekana kutoka
 kwa wadau mbalimbali ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya 
Tano kutatua kero ya upungufu wa madawati shule za msingi na sekondari 
nchini,” alifafanua Mhe. Ngeleja.
Mhe. Mgeleja aliendelea  kusema 
kuwa, ili kufanikisha mashindano hayo uongozi wa timu ya Bunge (Bunge 
Sports Club) umeunda kamati maalum ya maandalizi ili kufikia lengo 
lililokusudiwa kwa kuwatembelea na kuwahamasisha wadau mbalimbali Nchini
 Ili wachangie madawati.
Wabunge waliochaguliwa katika 
kamati hiyo ni Mwenyekiti Mhe. John Peter Kadutu (Ulyankulu), Makamu 
Mwenyekiti Mhe. Mussa Azzan Zungu (Ilala) pamoja na wajumbe Mhe. Salim 
Hassan Turky (Mpendae), Mhe. Ridhiwani Kikwete (Chalinze), Mhe. Mwigulu 
Nchemba (Iramba Magharibi), Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu (Igunga).
Wajumbe wengine ni Mhe. Raphael 
Chegeni (Busega), Mhe. Mansoor Hiran (Kwimba), Mhe. Ahmed Shabiby 
(Gairo), Mhe. Bonna Kaluwa (Segerea), Mhe. Zaynab Vulu (Viti Maalum), 
Mhe. Abdul-Aziz Abood (Morogoro Mjini) na Mhe. Venance Mwamoto (Kilolo).
Aidha Mhe. Ngeleje amesema kwamba
 ameitambulisha kamati hiyo ili wadau waweze kuwatambua na kusiwe na 
maswali mara wajumbe hao wanapokutana na wadau kwa ajili ya kuwaomba 
kuchangia madawati  au fedha zitakazonunulia madawati na baadaye 
kukabidhiwa Serikalini ili yaweze kusambazwa Nchi nzima.
Vile vile amewaomba wadau ambao 
wako tayari kushirikiana na wabunge  katika uchangiaji wa madawati basi 
wasisite kuonana na kamati hiyo na kutoa michango yao.
Waratibu na waandaaji wa 
mashindano hayo ni Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na uongozi wa (Bunge 
Sports Club) ambapo mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Ogasti 15, 2016
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni