Watanzania watakiwa kutumia fursa za soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki
By Newsroom on June 16, 2016
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO,
WAFANYABIASHARA wa Tanzania
wametakiwa kutumia fursa za biashara zinazopatikana katika soko la nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuuza bidhaa zao ndani ya
Jumuiya hiyo.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari.
“Wafanyabiashara wanatakiwa
kuchangamkia fursa ya biashara katika soko la pamoja kwa kuwa ni haki
yao na ni utekelezaji wa malengo ya Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kifungu cha tano ambapo ilianzishwa itifaki ya umoja
wa forodha ” ,alisema Bi. Mindi
Wafanyabiashara hao pamoja na
wasafirishaji wanaotaka kufanya biashara katika soko la Jumuiya hiyo
watatakiwa kuonesha cheti cha uasilia wa bidhaa wakati wakiingia nchi
wananchama wa Jumuiya hasa kwa wafanyabiashara wadogo wenye bidhaa
zisizozidi dola za kimarekani 2000, ambapo hawalazimiki kuwa na wakala
wa forodha.
Wanatakiwa kufuata utaratibu kwa
kufika katika kituo chochote cha forodha kilichopo mpakani wakiwa na
bidhaa zao ili wapewe cheti cha uasilia wa bidhaa.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara,
Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, katika Wizara hiyo, Bw. Geofrey
Mwambe, amesema ni vyema wafanyabiashara wakatoa taarifa endapo
watakumbana na vikwazo visivyo vya kiforodha kupitia mfumo wa ujumbe
mfupi kwa kuandika neno ‘NTB’ kwenda namba 15539.
Bw. Mwambe amesema pia ,madereva
wanaosafirisha mizigo kwenda nchi wanachama watakapokutana na vikwazo
visivyo vya kiforodha barabarani watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi
kupitia namba 0713631780.
Kwa mujibu wa Mkataba wa
uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu namba 5 ambapo
Jukuiya ilianzisha Itifaki ya Umoja wa Forodha (East African Community
Customs Union) wafanyabiashara wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo wana
fursa za kufanya biashara kwa kuuza bidhaa zao ndani ya nchiwanachama
wa Jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi
bila kutozwa ushuru wa forodha ilimradi bidhaa zao zimezingatia vigezo
na kufuata utaratibu ulioainishwa katika itifaki hiyo.
Japokuwa Sudani ya Kusini
imeridhia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado fursa za kufanya
biashara nchini humo hazijakamilika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni