TANZANIA MWENYEJI MAADHIMISHO YA 6 WIKI YA MAJI BARANI AFRIKA
…………………………………………………………………………………………………….
Frank Mvungi- Maelezo
Tanzania Mwenyeji maadhimisho ya 6
ya wiki ya Maji Barani Afrika na Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa
Maji wa Nchi za Afrika yatakayofanyika Julai,2016 Jijini Dar es
salaam.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkurugenzi Msaidizi Maji Shirikishi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Bw. Sylivester Matemu wakati wa mkutano na waandishi wa Habari leo
jijini Dar es salaam.
Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa
Maonyesho ya Wiki ya maji yatakayofanyika kabla ya mkutano wa Baraza la
Mawaziri atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Kassim Majaliwa.
Akifafanua Matemu amesema kuwa
mkutano huo utahusisha washiriki zaidi ya 1000 kutoka mataifa 54 kutoka
Bara la Afrika na wengine kutoka nje ya Afrika.
Maadhimisho hayo yataambatana na
maonyesho ya shughuli za wadau wa sekta ya maji na umwagiliaji, kwenye
Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es salaam.
Kauli mbiu ya kongomanao hilo ni “
Kufikia lengo la maendeleo Endelevu Juu ya usalama wa Maji na usafi wa
mazingira” alibainisha Matemu.
Mkutano huo utawasaidia wataalamu
wa maji kutoka Mataifa mbalimbali ya Afrika kujadiliana kuhusu
mikakati mbalimbali itakayosaidia kupambana na changamoto zinazoikabili
sekta ya maji katika bara la Afrika.
Akizungumzia faida za Mkutano huo
Matemu amesema kuwa utasaidia kufungua fursa mbalimbali zilizopo
katika sekta ya maji na Sekta nyingine ikiwemo kukuza na Kutangaza
vivutio vilivyopo hapa nchini hali itakayosaidia kukuza Utalii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni