Alhamisi, 23 Juni 2016

Watumishi wa Umma waaswa kuzingatia maadili katika kutekeleza majukumu yao

IMGS1319 Frank Mvungi – MAELEZO – Dodoma
—————————–
Watumishi wa Umma waaswa kuzingatia maadili katika kutekeleza majukumu yao hasa wanapowahudumia wananchi ili kuongeza tija.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Akifafanua Mhe. Majaliwa amesema kuwa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa watumishi wote wa Umma wanazingatia uadilifu, uchapakazi, sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia Utumishi wa Umma.
“Serikali itawachukulia hatua kali wale wote watakaotumia madaraka yao vibaya bila kujali vyeo vyao” alisisitiza Mhe. Majaiwa.
Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali hivi karibuni itawasilisha Bungeni muswaada wa Sheria utakaosaidia kuanzishwa Kwa Divisheni ya kushughulikia Mafisadi katika Mahakama Kuu.
Lengo la Serikali ni Kuhakikisha kuwa wananchi wanahudumiwa vizuri pale wanapohitaji huduma mbalimbali ndio sababu tunaendelea kuimarisha vyombo vyetu kama Taasissi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili zitekeleze majukumu yake vizuri.
Katika kuimarisha maadili Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kuanza kujumuisha masomo ya maadili katika mitaala ya Elimu hapa nchini ili kuongeza kasi ya kukuza na kujenga maadili miongoni mwa jamii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni