MKUU
wa wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Ibrahimu Marwa amesema viongozi
wa Mfuko wa Wakfu wa maendeleo ya zao la pamba uliwapelekea wakulima
pembejeo feki na kuwasababishia hasara.
Amesema hatua hiyo inatokana
wafanyabiashara na viongozi wa mfuko huo kuwa na maslahi binafsi katika
zao la pamba hivyo kushindwa kuwasaidia wakulima ipasavyo.
Marwa aliyasema hayo jana
(Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali
Mstaafu, Ezekiel Kyunga alipokuwa akisoma taarifa ya Mkoa huo kwa Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa alipowasili Mkoani hapo.
Alisema mara baada ya wakulima
kupelekewa pembejeo hizo na kubaini kuwa na kasoro walizipeleka katika
Kiituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukirigulu kilichoko mkoani Mwanza
ambacho nacho kilithibitisha kuwepo kwa kasoro.
Kwa upande wake Waziri Mkuu
amewataka Maofisa Kilimo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na kuwasaidia
wakulima wa pamba ili waweze kupata tija.
Ametaka Maofisa Kilimo na
viongozi wa maeneo yanayolima pamba kujipanga upya baada ya kumalizika
kwa msimu wa mwaka kwa kuanza mikakati ya kufanya utafiti wa mbegu bora
za pamba na kuziandaa za kutosheleza wakulima wote.
Alisema hakuna sababu ya
kuendelea kuwa na Maofisa Kilimo ambao wanashindwa kutimiza majukumu yao
kwa sababu mashamba ya wakulima yanashindwa kuendelea kwa kuwa hakuna
mtu anayewafuatilia.
“Mwakani muanze kufanya utafiti
kuanzia hatua za awali na kituo cha Ukirigulu kipewe kazi ya kusimamia
zao hili na kiwe na shamba darasa kwa ajili ya kufundishia wakulima.
Lengo ni kuhakikisha zao hili linakuwa na tija,” alisema.
Hata hivyo Waziri Mkuu ameziagiza
Halmashauri za Wilaya zinazolima pamba zifanye utafiti ili kujua sababu
zilizosababisha wakulima kupunguza ari ya kulima zao hilo.
Pia amewataka waachane na mfumo
wa kilimo cha mkataba kwa sababu hauna tija kwa mkulima kwani
hautengenezi ushindani na badala yake wajifunze mfumo unaotumika katika
uuzaji wa zao la korosho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni