Serikali yaunda Kikosi Kazi Kudhibiti Uvuvi Haramu wa kutumia mabomu
Serikali
imeunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia uharibifu wa kimazingira
ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu wa kutumia mabomu ili kulinda mazalia ya
samaki na kulinda ikolojia ya bahari.
Kauli hiyo
imetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Wiliam Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chambani
(CCM), Mhe. Yusuf Salim Hussein aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na
serikali kuzuia uvuvi haramu wa kutumia mabomu.
Ole Nasha
alitaja wajumbe wanoaunda kikosi kazi hicho kuwa ni Ofisi ya Rais, Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Wizara za Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Nishati na Madini.
Alizitaja
Ofisi nyingine kuwa ni Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC),
ambapo kikazi kazi hicho kitaratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la
Polisi Nchini.
“Kuna
uhusiano mkubwa kati ya ugaidi na uvuvi wa kutumia vilipuzi, hivyo suala
hili ni la kiusalama zaidi na kwa kutambua hilo Serikali imeanzisha
vituo 5 vya kudhibiti uvuvi huo na baadhi ya vituo hivyo viko Pemba na
Tanga,” alisema Ole Nasha.
Ole Nasha
alisema inaendelea kuziagiza Halmashauri za Ukanda wa Pwani ya Bahari ya
Hindi kushirikiana na jamii kusimamia kwa ukamilifu udhibiti wa uvuvi
haramu wa kutumia mabomu kuwachukulia hatua kali za kisheria wale
wanaojihusisha na uvuvi huo.
“Sheria ya
Uvuvi ya Na. 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2009 zimekasimu
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Raslimali za Uvuvi katika
Halmashauri zote nchini,”Alisema Ole Nasha.
Alisema kuwa
Wizara ina jukumu la kuanda Sera, Sheria, Kanuni zinazotumika katika
Uhifadhi, Udhibiti na Usimamizi wa waza Uvuvi nchini.
Ole Nasha
aliongeza kuwa ili kuongeza nguvu ya kudhibiti uvuvi haramu, Serikali
ilianzisha mfumo wa kushirikisha jamii kupitia vikundi vya usimamizi
shirikishi wa Raslimali za Uvuvi (BMUs) ili kuwaelimisha wananchi juu ya
athari ya matumizi ya mabomu na uvuvi haramu.
Alisema
matumizi ya mabomu katika uvuvi yana athari kubwa kwa samaki na
mazingira ya baharini kwa kuwa huua samaki na viumbe wengine na uharibu
matumbawe ambayo ni mazalia ya samaki.
Ole Nasha
alibainisha athari nyingine kuwa ni kupungua kwa rasilimali za uvuvi,
kupoteza kipato, kuongezeka kwa mmomonyoko wa fukwe za bahari, pammoja
na kuathiri afya za walaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni