DAWASCO kuongeza uzalishaji toka lita milioni 70 mpaka 106 kwa siku
Kaimu Meneja Uhusiano wa Shirika
la Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) Bi. Everlasting Lyaro
amesema kuwa uzimaji wa mtambo wa Ruvu Juu kwa wakazi wa Dar es Salaam
na Mji wa Kibaha mkoani Pwani siku tatu kuanzia ijumaa ya tarehe 17
mpaka tarehe 19 Jumapili umelenga kuongeza uzalishaji kutoka lita
milioni 70 mpaka lita milioni 106 kwa siku.
Bi Lyaro alisema hayo alipokuwa
akifanya mahojiano na Idara ya Habari Maelezo akitoa ufafanuzi kuhusu
taarifa za uzimaji wa mtambo wa Ruvu Juu.
Alisema kuwa sababu kubwa za
kuzima mtambo huo ni kumruhusu mkandarasi (WABAG) kuunganisha mtambo
mpya wa Maji na ule wa zamani ili kufanikisha kampeni ya kumtua mama wa
Dar es Salaam ndoo kichwani kwa kumfikishia maji nyumbani kwake.
Kuzimwa kwa mtambo huo wa Ruvu
Juu kutapelekea maeneo ya
Mlandizi,Kibaha,Ubungo,Kimara,Kibamba,Kibangu,Makuburi,Tabata,Segerea na
Kinyerezi kukosa maji kwa kipindi hicho cha masaa 72.
Aidha wananchi wa maeneo husika
wanashauriwa kuhifadhi maji ya kutosha kwa siku hizo tatu na DAWASCO
inaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza kwani jitihada hizi ni
maboresho ya kuwasogezea maji karibu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni