WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR ATEMBELEA VITUO VYA AFYA MKOA WA KASKAZINI.
By Newsroom on June 13, 2016
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya
Kaskazi ‘A’ Hassan Ali Kombo na Daktari dhamana wa Wilaya hiyo Rahma
Abdalla Maisra wakati akikitembelea kituo cha Afya cha Chaani Masingini.
Mwakilishi
wa Jimbo la Chaani Nadir Abdul-latif akimkaribisha Waziri wa Afya
Mahmoud Thabit Kombo kuzungumza na wananchi waliofika kituo cha Afya cha
Chaani Masingi ambacho kinahitaji matengenezo makubwa.
Waziri
Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na wafanyakazi wa kituo cha afya cha
Donge na Kamati Kiongozi ya Jimbo hilo katika Kituo cha Afya cha Donge
Wilaya Kaskazini B.
………………………………………………………………………………………………………………
Na RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR
Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud
Thabit Kombo amezitaka Kamati Kiongozi za Majibo kusimamia kikamilifu
vituo vyao vya Afya na kuhakikisha majukumu waliyopangiwa
wanayatekeleza kikamilifu ili kuimarisha huduma katika vituo hivyo.
Alisema Serikali imebadili mfumo
katika kusimamia vituo vya afya kwa kuvipeleka moja kwa moja kwa jamii
kusaidia huduma ndogo ndogo huku Serikali kuu ikibakia na jukumu lake
la msingi la kuvipatia vifaa vya matibabu, dawa na mishahara ya
wafanyakazi.
Waziri Mahmoud Thabit Kombo
alieleza hayo alipofanya ziara ya kutembelea vituo vya Afya vya Mkoa wa
Kaskazini Unguja kujua changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa vituo
hivyo katika kutoa huduma bora.
Alisema huduma ya matengenezo
madogo madogo, kulipia umeme na maji, kuviwekea uzio na ulinzi sasa
vipo chini ya Kamati Kiongozi za Majimbo ambazo zinaundwa na Wabunge,
Wawakilishi, Madiwani, Masheha na Mkuu wa kituo cha Afya husika.
Aliongeza kuwa hivi sasa Serikali
haitoa kipaumbele kujenga vituo vipya vya Afya bali inaelekeza nguvu
zake kuviimarisha vituo viliopo kwa kushirikiana na mradi wa ORIO na
Milele pamoja na Kamati Kiongozi za Majimbo.
Aliwahakikishia wananchi wa Jimbo
la Chaani kwamba kituo chao cha Afya cha Chaani Masingini, ambacho
kimesitisha kutoa huduma kwa miaka mitano kutokana na kuwa kibovu,
kitaanza kufanyiwa matengenezo makubwa hivi karibuni kupitia Mradi wa
ORIO.
Waziri wa Afya aliwataka viongozi
na wafanyakazi wa sekta ya Afya kuwapa ushirikiano wa karibu wakunga wa
jadi ambao wanatoa mchango mkubwa katika kupunguza vifo vya mama
wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua.
Alisema wakunga wa jadi bado
wanaendelea kuaminiwa na wanachi wengi, hasa sehemu za vijijini,
kutokana na huduma nzuri wanazotoa kwa wateja wao na ameshauri wapatiwe
vitambulisho maalum ili waweze kutambulika.
Aidha alisema Zanzibar imepata
sifa kubwa mbele ya Jamii ya Kimataifa katika kupambana na Malaria na
maradhi mengine yaliyokuwa yakiwasumbua wananchi, lakini hali sio nzuri
katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga hivyo ametaka
juhudi zaidi ifanywe kukabiliana na tatizo hilo.
Akinamama wa Jimbo la Chaani
walimueleza Waziri wa Afya kuwa wanapendelea zaidi kujifungua kwa
wakunga wa jadi kutokana na kauli zisizoridhisha kutoka kwa wakunga wa
vituo vya Afya wanapokwenda kujifungua.
Walishauri kutolewa elimu ya
ukarimu na upole kwa wakunga wa vituo vya afya ili kuwajengea imani
wajawazito kwenda kujifungulia kwa wingi katika vituo hivyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Chaani
Nadir Abdul-latif alimuhakikishia Waziri wa Afya kwamba yupo tayari
kutoa kila msaada unaotakiwa ili kuona huduma za Afya katika Jimbo hilo
zinaimarika.
Waziri wa Afya alitembelea vituo vya Afya vya Chaani Masingini, Chaani Kikobweni na Kituo cha Afya Donge.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni