Jumatatu, 13 Juni 2016

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI

By Newsroom on June 13, 2016
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TZ 
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 13 JUNI, 2016
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto inaendelea na utaratibu wa kutoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa Kipindupindu nchini kila wiki kama tulivyoahidi, ili kutoa tahadhari kwa wananchi na maelekezo ya hatua za kuchukua ili kukabiliana na mlipuko huu. Hadi kufikia tarehe 12 Juni 2016, jumla ya wagonjwa 21,786 nchini wametolewa taarifa,na kati yao Ndugu zetu 342 wamepoteza maisha tangu ugonjwa huu uliporipotiwa Agosti 2015.
Takwimu zinaonyesha kuwa, katika wiki hii inayoishia   tarehe 12 Juni 2016, Idadi ya wagonjwa walioripotiwa nchi nzima ni 78 na kati yao mmoja  alipoteza maisha.   Wiki iliyotangulia kulikuwa na wagomjwa 62 waliotolewa taarifa na kati yao watatu walipoteza maisha. Hii ikionyesha kuna ongezeko la wagonjwa walioripotiwa wiki hii ikilinganishwa na wiki iliyotangulia ingawa kuna kupungua  kwa Idadi ya waliopoteza maisha.
Mikoa iliyoripoti ugonjwa wa kipindupindu wiki hii ni mitano(5), Morogoro ( wagonjwa 43 na kifo 1), Mwanza (21), Mara (7), Lindi (4) na Manyara (3).  Aidha wiki hii wilaya zilizoripoti ugonjwa wa Kipindupindu ni Morogoro vijijini (wagonjwa 27 na kifo 1), Morogoro mjini (8), Mvomero (8), Ilemela (12), Nyamagana (9), Tarime vijijini (5), Tarime mjini (2), Kilwa (4) na Simanjiro (3).  Mpaka sasa bado mikoa ya Njombe na Ruvuma    haijaripoti mgonjwa yeyote wa Kipndupindu tangu mlipuko huu uanze mnamo mwezi Agosti mwaka 2015

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni