Kituo cha jeshi kilivyobadilishwa kuwa Soko la Kariakoo
Benjamin Sawe Maelezo
HISTORIA ya jina la Kariakoo na
soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati
Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika.
Mahala lilipo soko hilo
palijengwa jengo la utawala wa Wajerumani ambalo lilikusudiwa litumike
kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser
Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.
Hata hivyo baada ya jengo
kukamilika halikutumika kama ilivyokusudiwa kuwa na badala yake
lilitumika kama kambi ya kikosi cha wapagazi waliobeba mizigo ya Vita
Kuu ya Kwanza ya Dunia waliojulikana kama Carrier Corps.
Jina hilo la maaskari wabeba
mizigo katika Kiswahili lilitamkwa ‘karia- koo’ na liliendelea kutumika
kama jina la eneo lote linalozunguka jengo hili la Soko la Kariakoo.
Meneja Mkuu wa Soko la Kariakoo,
Florens Seiya anasema baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuisha rasmi
mwaka 1919 na nchi Tanganyika kuanza kutawaliwa na Waingereza, jengo
hilo lilianza kutumika kama soko na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam.
Anasema wakati huo
wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakuwa
na meza. Wafanyabiashara hao waliendelea kufanya biashara zao sakafuni
hadi miaka ya 1960, meza za saruji zilipojengwa. Seiya anasema kwa
kadiri jiji la Dar es Salaam lilivyokua na wakazi wake kuongezeka,
ndivyo soko hilo la lilivyozidiwa na kushindwa kumudu kutoa huduma nzuri
kwa wananchi.
Wafanyabiashara walifanya
shughuli zao katika hali ngumu kwa sababu kulikuwa na msongamano mkubwa
wa watu pia hapakuwepo ghala za kuhifadhia bidhaa.
Hali hiyo iliwafanya viongozi wa
halmashauri ya jiji kuona haja ya kuwa na soko kubwa na la kisasa
kulingana na maendeleo ya jiji, na hivyo wakaanza kujadili uwezekano wa
kujenga soko jipya kubwa na la kisasa. Uamuzi wa kujenga Soko Kuu la
Kariakoo ulifanywa na serikali mwaka 1970 ambapo Halmashauri ya jiji la
Dar es Salaam iliagizwa kujenga soko jipya la kisasa ambalo lingechukua
nafasi ya soko la zamani.
Anasema matarajio ya serikali ya
kujenga soko hilo yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa jiji soko kubwa la
chakula ambalo lingetosheleza mahitaji yao kwa muda wa miaka 50 hadi 70
Mipango ilikamilika na ujenzi ulianza rasmi Machi 1971.
Ramani ya jengo la soko
ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo Mtanzania Beda Amuli. Kwa
mujibu ya machapisho yanayoelezea historia ya soko hilo, mkandarasi
huyo alitakiwa kwenda kujifunza katika nchi za Accra – Ghana na
Lusaka-Zambia, kuangalia masoko yaliyojengwa katika miji hiyo miwili,
ndipo atengeneze ramani yake, ambalo ndiyo soko linaloonekana hivi sasa.
Anasema kuwa, mkandarasi
aliyechora jengo hili ameweka baadhi ya maumbo yanayofanana na majengo
hayo aliyokwenda kuyatazama. Hii ndiyo sifa pekee inalolifanya soko hili
la Kariakoo kuwa la tofauti na masoko mengine katika ukanda huu wa
Afrika Mashariki na Kati.
Ujenzi wa soko ulikamilika
Novemba 1975 kwa gharama ya Sh milioni 22 na kufunguliwa rasmi Desemba
mwaka huo huo ambapo Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere
alikuwa mgeni rasmi. Jengo la Soko Kuu la Kariakoo lipo katika kiwanja
namba 32 mtaani Kariakoo, katikati ya makutano ya mtaa wa Mkunguni na
mtaa wa Nyamwezi na limezungukwa na mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu
na Tandamti.
Soko hilo lina majengo mawili
ambayo yameunganishwa katika Ghorofa ya chini ya ardhi. Jengo la kwanza
linaweza kuitwa soko kubwa na jengo la pili soko dogo. Soko kubwa
limegawanyika katika sehemu tatu ambayo ni ghorofa ya kwanza, sehemu ya
katikati na ya chini maarufu kama shimoni.
Eneo la Shimoni kuna mabucha 16
yanayouza nyama iliyokaguliwa kiafya toka mikoa ya Dodoma, Mwanza na
Shinyanga, na samaki wabichi toka maziwa na mito ya Tanzania. Soko dogo
ni la rejareja ambalo si tofauti na masoko mengine katika Jiji la Dar es
Salaam.
Ingawa eneo la Kariakoo
limezungukwa na maduka yanayouza bidhaa mbalimbali, bado Soko la
Kariakoo ndio soko kuu la mazao na bidhaa ya kilimo nchini. Linauza
mazao kwa bei ya jumla ya rejareja pamoja na vifaa vya kilimo.
Shirika la Masoko ya Kariakoo
(SMK) linasimamia uendeshaji wa biashara za Soko la Kariakoo, kuweka
kipaumbele katika shughuli za biashara mbili: Anasema shirika
linakodisha ardhi ya biashara kwa wauzaji wa Rejareja.
Pia eneo la soko hilo lina maduka
82 katika soko kuu, yanayokodishwa kwa SMK kwa wauzaji wa rejareja.
Mbali na mazao ya kilimo, maduka mengi yanauza vifaa vya kilimo na
elektroniki. Pia, soko linatoa baadhi ya maduka nje yanayouza mboga za
majani za rejareja katika soko dogo la nje.
Kuhusu uendeshaji wake shirika
hilo linasimamia soko la jumla kwa mazao ya kilimo na jamii ya samaki
wakavu linalofanyika eneo la soko. SMK inatoza asilimia ya faida ambayo
si zaidi ya asilimia nane tu ya bei ya mauzo kwa biashara ya jumla. Vile
vile shirika linawatoza wafanyabiashara wa jumla ada ya usajili.
Kwa masoko ya jumla na rejareja,
Shirika linaweka daraja kati ya wakulima na wateja, ili wateja waweze
kupata mahitaji yao yote ya nyumbani katika sehemu moja kwa bei nafuu na
kuleta uthabiti kwa sekta ya kilimo ya nchi. Seiya anasema Soko la
Kariakoo limekua na kupanuka kwa kiasi kukubwa ikilinganishwa na wakati
lilipofunguliwa rasmi mnamo Desemba 8, 1974.
Kwa kuwa muendeshaji mkuu wa
biashara za mazao yatokayo mikoani kuingia katika jiji la Dar es Salaam.
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana hivi sasa soko hilo
linakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu.
Ili kukabiliana na changamoto
hiyo kuu na nyinginezo za kuboresha huduma kwa watumiaji wa soko,
shirika linategemea kuunda upya soko na kuanzisha soko la jumla Dar es
Salaam. “Kuanzisha vituo vipya vya jumla ni njia mojawapo ya mipango ya
maendeleo ya jiji na maeneo yao ya jirani.
Anaelezea miradi inayotarajiwa
kuanzishwa na shirika hilo kuwa ni ujenzi wa upanuzi wa soko la rejareja
la Kariakoo la leo, kukuza idadi ya magenge na kurahisisha maegesho ya
magari sokoni. “Kwa sasa soko la nje linakosa maegesho salama ya magari,
maduka ya kisasa, ofisi, vyoo, sehemu za kukaa kwa ajili ya mikutano na
mikusanyiko ya kijamii.
Uundaji upya wa soko utalisaidia
shirika kukabiliana na baadhi ya changamoto,” anasema Seiya. Vile vile
ujenzi wa soko la kisasa, litakalokuwa Buguruni-Chanika, wilaya ya Ilala
na ujenzi wa kituo kingine cha soko litakalokuwa Tabata kwa ajili ya
biashara na shughuli za burudani.
Ili kufanikisha haya, Shirika
linahitaji mtaji wa kuanzia ili kufikia malengo hayo . Kwa juhudi na
ufadhili wa serikali, itatoa fursa kwa ubia binafsi kuwekeza kwenye
mradi huu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni