Ijumaa, 6 Mei 2016

Mtafiti wa Hesabu aomba Milioni 12 kufanikisha safari ya Marekani kuwasilisha Utafiti wake.

Anitha Jonas – MAELEZO
Dar es Salaam.
Mtanzania aliyevumbua Fomula ya Hesabu yenye uwezo wa kutumika katika Hesabu za Viwandani Mhandisi Mazoleka Maziku awaomba watanzania, Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali,Kimataifa na za watu binafsi kumchangia kiasi cha Shilingi Milioni 12 kwa ajili ya kuwasilisha utafiti wake katika Mkutano wa Mwaka wa wataalamu wa Hesabu za Viwandani nchini Marekani.
Bw. Maziku ameomba msaada huo alipokuwa akizungumza na waaandishi wa Habari kuhusu utafiti huo aliyoufanya kwa lengo la kuboresha fomula zinazotumika sasa hivi ambapo kama utafiti huu utakubalika na kuanza kutumika basi unaweza kurahisisha ukokotoaji wa hesabu zinazotumika viwandani.
Mbali na hayo mtafiti huyo alisema fomula hiyo aliyogundua inauwezo wa kukokotoa hesabu za aina mbili ambazo hujulikana kama (Arithmetic Progression na Sums of Powers) ambapo hapo mwanzo zilikuwa zikitumia fomula tofauti.
“Baada ya kuwasilisha utafiti wangu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Hesabu (UDSM)kwa ajili  ya kufanya uchunguzi na uhakiki, wataalam hao  walijiridhisha na kuona vyema watume utafiti huo katika  Chuo Kikuu cha Manchester Uingereza, ambapo chuo hicho ni miongoni mwa vyuo bora  Duniani na ndipo nilipotumiwa mwaliko huu,” alisema Mhandisi Maziku.
Hata hivyo mtafiti huyo amewasihi watanzania watakaoguswa kumchangia wanaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0686-632 262 au 0713 037 123 kwa ajili ya kufanikisha safari hiyo, kwani safari hiyo itasaidia kuitangaza nchi yetu pamoja na kupata mtandao wa wanasayansi Duniani.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika huko Marekani kuanzia tarehe Julai 11 hadi 15 mwaka huu katika Chuo Kikuu cha Massachusetts na Utahushisha wanachama zaidi ya 13,000 Duniani pamoja na Vyuo Vikuu vya Kisayansi takribani 500 Duniani kote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni