MSHAMBULIZI wa Taifa Stars, Elius Maguli amekamilisha usajili wake
kutoka Stand United ya Shinyanga kama mchezaji huru na kujiunga katika
klabu ya Dhofar SC ya Oman Professional League.
Kila mmoja anakumbuka namna mchezaji huyo alivyopitia kipindi kigumu
msimu wa 2014/15 akiwa na kikosi cha Simba SC ambacho kabla ya kuanza
kwa msimu wa 2015/16 kocha aliyepita wa kikosi hicho, Dylan Kerr
alitangaza kutomuhitaji na uongozi ukavunja mkataba wake akiwa bado na
mwaka mmoja zaidi.
Kitendo cha kujiunga na kocha Mfaransa, Patrick Liewig katika timu ya
Stand kabla ya kuanza kwa msimu uliopita hakikuonekana kuwastua wengi
lakini game 9 za mwanzo wa msimu ziliambatana na magoli 9 kwa mchezaji
huyo wa zamani wa Ruvu Shooting, pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa
mwezi katika VPL na kujumuhishwa katika timu ya Taifa kwa mara ya kwanza
baada ya miaka mitatu.
Kujiunga na Dhofar timu iliyomaliza katika nafasi ya tano katika ligi
ya kulipwa mwaka mmoja uliopita ni hatua kubwa kwa mchezaji kijana kama
Maguli ambaye ameondoka VPL akiwa amefunga jumla ya magoli 33 katika
misimu yake mitatu aliyocheza kama mchezaji wa vilabu vya Shooting,
Simba na Stand United.
Ameruka vikwazo vingi katika ‘soka lenye fitna’ na matatizo mengi ya
watendaji. Mfano, katika misimu yake miwili ya mwisho VPL (Simba na
Stand) timu hizo zote mbili zimejaa migogoro ya kiutendaji kati ya
viongozi na wachezaji au viongozi kwa viongozi.
Katika mazingira hayo si rahisi kwa mchezaji kutimiza malengo yake na
inapotokea nafasi kama hii ya Maguli-Kusajiliwa moja kwa moja na timu
ya kulipwa ukiwa U25 ni jambo la kumshukuru Mungu na pengine ni sehemu
ya kufanya kazi nzuri zaidi kwa jitihada ili kuthibitisha kwa wale
waliokusaini kuwa hawakufanya makosa.
Maguli ni mshambuliaji wa kikosi cha kwanza katika timu ya Taifa ya
Tanzania kwa mwaka mmoja sasa akicheza sambamba na Thomas Ulimwengu na
Mbwana Samatta katika safu ya mashambulizi kwa maana hiyo, kocha Charles
Mkwassa ataendelea kufurahia vijana wake watatu wakiwa ng’ambo ya nchi
kuendeleza vipaji vyao na kudumisha viwango vyao vya kiuchezaji.
Kama Hamis Mroki anayecheza Thailand, huyu ni nahodha wa kikosi cha
vijana kilichokuwa kikiwajumuhisha kina Ulimwengu, Himid Mao na wengine
ni zao la TSA, Samatta, Tom, Maguli, Mrisho Ngassa watatupiwa jicho la 3
bila shaka timu ya Taifa Stars itaimarika licha ya kwamba bado hatuna
ligi makini ya ndani.
Dhofar ni timu iliyoanzishwa miaka 44 iliyopita, na Oman kuna
mishahara mikubwa hadi kufikia dola 30,000 kwa mchezaji wa kiwango cha
Maguli. Mchezaji wa kikosi cha kwanza wa timu ya Taifa. Sasa mastaa
watatu wa Stars katika kikosi cha mashambulizi wapo ng’ambo. Kila la
heri Elius Maguli.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.