TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU WAZIRI WA AFYA LEO
Kama mnavyofahamu, Serikali
kupitia Wizara yangu imeweka utaratibu wa kutoa kila wiki taarifa ya
mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini ili kuifahamisha
jamii hali ilivyo na hatua zinazochukuliwa na Wizara kudhibiti ugonjwa
huu. Hadi kufikia tarehe 17 April 2016, jumla ya wagonjwa 20,882
wametolewa taarifa, na kati ya hao ndugu zetu 329 wamepoteza maisha
tangu ugonjwa huu uliporipotiwa Agosti 2015.
Takwimu za wiki iliyopita kuanzia
tarehe 10 hadi 17 Aprili 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa
kipindupindu imepungua ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa wiki
hiyo ni 212 ikilinganishwa na 368 wa wiki iliyotangulia. (April 04
hadi Aprili 10, 2016). Mikoa ambayo bado imeendelea kuripoti ugonjwa wa
kipindupindu ni 10. Mikoa iliyopata wagonjwa wengi zaidi ni Morogoro
(wagonjwa 51 na Kifo 1), Mara (45), Kilimanjaro (31), Pwani (24), na
Tanga (24). Aidha hakuna Mkoa mpya uliotoa taarifa ya kuwepo kwa
wagonjwa wa Kipindupindu.
Pia katika wiki hii Halmashauri
zilizoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Morogoro vijijini (23), Same
(20), Tarime mjini (20), Mvomero (wagonjwa 18, na Kifo 1) na Kinondoni
(16). Vile vile, katika wiki hii Mikoa ambayo haijapata mgonjwa wa
Kipindupindu ni Kigoma, Dodoma, Singida, Shinyanga, Tabora, Lindi,
Kagera, Rukwa, Katavi, Mbeya, Simiyu, Iringa na Mtwara.
Tafsiri kubwa tunayoipata kutoka
kwenye takwimu hizi ni kwamba kwa sasa ni dhahiri kuwa juhudi zetu za
pamoja za kupambana na ugonjwa wa Kipindupindu zimeonyesha matunda.
Wizara inawapongeza wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea
kutekelezwa na katika kusimamia kikamilifu miongozo inayotolewa na
Wizara .
Vile vile, napenda kusisitiza
kwamba pamoja na kwamba tuna Mikoa ambayo haijaripoti wagonjwa au mikoa
ambayo imekuwa haina wagonjwa wapya kwa muda, bado hali si salama,
hususani wakati huu wa mvua za masika, na kwa kuwa na uwepo wa
mwingiliano mkubwa wa watu kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usafiri
na za biashara. Hali hii bado inaweza kupelekea ugonjwa wa Kipindupindu
kuenezwa kutoka mkoa wenye uambukizo na kwenda kwenye mikoa mingine.
Hivyo ni budi mikoa yote nchini kuendelea kuchukua hatua za tahadhari
ili kuzuia maambukizi, na pia kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa kila
siku, hata kama hakuna wagonjwa, na kusimamia kikamilifu hatua
mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huo.
Kufuatia Agizo la Mhe. Waziri
Mkuu alilolitoa kwangu tarehe 31 mwezi Machi 2016, Wizara yangu
itaendelea kutoa miongozo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya juu
ya hatua gani za kutekelezwa ili kuweza kudhibiti Ugonjwa huu na kuweza
kuutokomeza kabisa. Ninamshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa kuniamini na
kunipa mamlaka ya kutoa miongozo kwa wakuu hawa juu ya ugonjwa wa
kipindupindu. Aidha ninapenda kumhakikishia Mhe. Waziri Mkuu kuwa Wizara
yangu itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kutokomeza
ugonjwa huu kwa kushirikiana kwa karibu sana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya
zote nchini, pamoja na Viongozi wa Wizara nyingine. Wizara pia
itaendelea kumshirikisha Mhe. Waziri Mkuu kuhusu hatua mbalimbali za
udhibiti wa ugonjwa huu, na kuainisha changamoto zitakazojitokeza ili
kuweza kudhibiti ugonjwa huu. Aidha Wizara yangu pia itaendelea
kusimamia utekelezaji wa maagizo tuliyoyatoa kwa Waganga Wakuu wa Mikoa
na Wilaya wiki mbili zilizopita katika kikao kilichofanyika Mkoani
Dodoma ili kuweza kutathmini mwenendo wa ugonjwa huu na kuudhibiti. Ili
kusimamia hili Wizara inaagiza mikoa kutuma taarifa za shughuli
mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huu kila wiki kwa mujibu wa miongozo
itakayotolewa na Wizara
Katika kipindi hiki cha masika,
Wizara inatoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za usafi binafsi
na usafi wa mazingira. Napenda kurudia kwamba ni marufuku kwa
watu kutitirisha maji taka ovyo, hasa katika kipindi hiki,
kwani kwa kufanya hivyo vimelea vya ugonjwa vinaweza kuenezwa kirahisi
sana kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Tunahimiza mamlaka husika
kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote watakaokiuka sheria ya Afya ya
Jamii. Aidha tunawasihi viongozi mbalimbali wa ngazi zote; za
vitongoji, vijiji, kata na tarafa kusimamia kikamilifu suala hili,
hususan wakati huu wa mvua za masika. Wizara inasisitiza kwamba kila
jitihada zifanyike kote nchini ili kuhakikisha kuwa jamii yote ya
Watanzania inatumia maji safi na salama. Hii ni pamoja na kuzingatia
taratibu za kutibu maji ya kunywa katika ngazi ya kaya.
Tunaendelea kuisihi jamii
kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za
kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia
yafuatayo:
- Utoaji na upatikanaji wa takwimu sahihi za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara, na bila kuingiliwa na viongozi wa kisiasa au kiserikali.
- Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yote ya mijini na vijijini ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu,
- Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia Mamlaka za maji zilizopo katika ngazi zote nchini,
- Kuhakikisha upatikanaji wa ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
- Kuhakikisha utunzaji salama wa maji ya kunywa yaliyotibiwa,
- Kufikisha wagonjwa wa Kipindu pindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu,
- Kuhakikisha upatikanaji na matumizi sahihi ya ORS katika maeneo mbali mbali nchini ili kupunguza athari za ugonjwa
Aidha, Vyombo vya usafiri vihakikishe vinatekeleza yafuatayo ili kudhibiti ugonjwa usisambae;
- kuwa na dawa ya jiki na pakiti za ORS kwenye sanduku la huduma ya kwanza kwa ajili ya kusafisha gari na kumhudumia mgonjwa atakaekuwa anatapika na kuharisha kabla ya kupelekwa kituo cha afya kilicho karibu,
- visipeleke abiria kujisaidia sehemu ambazo hazina vyoo, maarufu “kuchimba dawa”
- Visiwapeleke abiria kwenye sehemu za vyakula ambazo zipo kwenye mazingira ambayo si safi,
Hitimisho
Wizara inaendelea kuwashukuru
wataalamu wa sekta mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa
na Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla, kwa
kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa
Kipindupindu hapa nchini. Tunawasihi hali hii iendelee kwa juhudi kubwa
zaidi ili tuweze kutokomeza Kipindupindu nchini haraka iwezekanavyo.
Kipindupindu kinataka kuota mizizi katika jamii zetu, tusikubali jambo
hili litokee. Kwa ushirikiano wa pamoja tunaweza kukitokomeza kabisa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni