Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Sekta ya 
habari ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya wananchi na serikali 
yao. Ndiyo maana wanazuoni hupenda kusema kuwa habari ni muhimili wa nne
 wa dola. Kwa kuzingatia umuhimu huo, katika kuchekecha huku na huko, 
Mhe. Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
 Pombe Magufuli akamteua mtu mahiri kuongoza sekta hii, Mhe. Nape Moses 
Nnauye.
Kwa uteuzi 
huu ninadiriki kusema hatimaye Wizara imepata mtu sahihi na mchapakazi 
anayeweza kwenda na kasi ya Mheshimiwa Rais Magufuli na ni dhahiri 
kabisa kuwa kumpa Mhe. Nape ni kuthibitisha usemi wa wahenga usemao 
upele umepata mkunaji.
Kwa jinsi 
hii tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na 
Nchi kwa kutujalia kupata kiongozi wa nchi ambaye ni mchapakazi na 
aliyejaliwa kipawa cha kuona mbali kwa kuwaweka viongozi wa chini yake 
katika nafasi za uongozi wanazostahili.
Sekta ya 
habari ni sekta nyeti na muhimu sana katika dunia hii kwa kua bila 
kupashana habari na kujua kinachoendelea daima hakutakua na maendeleo 
kwa hiyo, ni sekta inayohitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu ili 
kuhakikisha kwamba inachukuliwa uzito na inapewa kipaumbele kwa kupewa 
vifaa na elimu ya kutosha ili kuepusha upotoshaji na kukosekana kwa 
habari muhimu hasa za Serikali zinazotakiwa kuwafikia wananchi kwa muda 
husika.
Tukiangalia 
katika sekta ya habari, Mhe.Rais hakukosea kabisa kumuweka Waziri Mhe. 
Nape kwa kuwa ameanza kuitumikia Wizara kwa kasi nzuri na ameonyesha nia
 ya kuiboresha Wizara hasa kwa tasnia ya habari kwa kuanzia kwenye 
wizara yake hadi katika ofisi za umma zilizoko mikoani ili kuhakikisha 
wanahabari wote nchini wanatambua thamani ya kazi yao.
Kwa maneno yake aliyoyatoa Jijini Mbeya alipokua akigawa vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya mawasiliano yaani ipad
 kwa maafisa mawasiliano wa mkoa huo alikaririwa akisema,”Nataka Wizara 
ihamie mikoani” hii haimaanishi kuwa Wizara ihamie mikoani kama 
alivyosema bali alimaanisha kiutendaji zaidi kuwa yale yote anayoyafanya
 katika Wizara yake atahakikisha na maafisa wa mikoani pia wanafanyiwa 
hivyo ikiwemo kugawiwa vitendea kazi pamoja na mambo mengine.
Katika kuhakikisha hilo, kwa upande wa sekta ya habari, Waziri Nape ameanza kwa kugawa ipad 
 kwa maafisa mawasiliano walioko mikoa ya pembezoni ambao wana upungufu 
mkubwa wa vitendea kazi na kwa muda mrefu wameshindwa kuifanya kazi yao 
kwa ufanisi kwa sababu ya uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi hiyo.
Ipad
 hizo zilizotolewa kama msaada kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
 Michezo na kampuni ya Startimes ambayo imeahidi kuwa bega kwa bega na 
Wizara hii  katika kuisaidia ili kuongeza ufanisi hasa katika sekta hii 
nyeti ya habari maana kwa maneno mengine tunaweza kusema sekta ya habari
 ndio daraja linalounganisha serikali na wananchi.
Siku 
aliyokabidhiwa ipad hizo Mhe. Nape alikaririwa akisema “Nawashukuru sana
 Startimes kwa kutujali,ipad hizi tutaanza kuzigawa kwa maafisa habari 
wa mikoa ya pembezoni kwa kuwa ndiko kuna uhaba mkubwa sana wa vifaa kwa
 maafisa hao”alisema Mhe Nape.
Maneno haya 
ya Mhe.Nape yanaungana na usemi wake wa kuifanya Wizara kuhamia mikoani 
kwa maana ya kuwapa kipaumbele katika kuwapatia vitendea kazi ili nao 
wasijione kuwa wametengwa au kutokuthaminiwa kama maafisa mawasiliano 
wengine hasa walioko Dar es salaam na mikoa mingine iiliyoendelea. Maana
 anaamini kuwa mikoani ndiko kuna wadau na ndiko ziliko shughuli nyingi 
kwa kuwa watu wengi wenye uwezo wa kuzikuza tasnia anazozifuatilia wapo 
mikoani.
Ni mengi 
sana Mhe.Nape ameyaongea hasa kwenye ziara zake alizozifanya kwenye 
baadhi ya mikoa kama Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Geita, 
Simiyu,Dodoma, Kagera pamoja na Mwanza ambako alipita kugawa ipad na 
kuangalia jinsi maafisa habari wanavyofanya kazi katika vituo vyao vya  
kazi. Ziara hiyo pia inalenga katika kujua changamoto wanazokumbana nazo
 ili kuweza kufanya kila kinachowezekana kuzitatua ili kufanya sekta hii
 kufanya kazi ya kupeleka taarifa kwa wananchi kama inavyopaswa 
kufanyika ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
 na Jemedari Mkuu Mhe. Rais John Pombe Magufuli.
Kiongozi 
huyu ameongelea kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 
ambao ulishirikisha wadau mbali mbali hasa wahariri pamoja na wamiliki 
wa vyombo vya habari kutoa maoni yao ambayo kwa asilimia 99 maoni hayo 
yamewekwa katika muswada huo.
“Muswada huo
 umeshakamilika, uko tayari kufikishwa bungeni, pia nataka 
niwathibitishie kuwa muswada huo utalinda maslahi ya waandishi wa habari
 kuanzia mishahara yao, mikataba ya kazi zao pamoja na bima ya matatizo 
wanayoyapata kwenye kazi zao lakini muswada huo utakua na sheria 
zitakazobana ufundishwaji wa masomo ya habari ili tupate waandishi ambao
 wamebobea katika fani hiyo” alisema Mhe. Nape.
Ndoto ya 
changamoto zinazoikabili tasnia ya habari mikoani zinakaribia kuwa 
historia kwa kuwa Waziri Nape amepanga kuleta teknolojia mpya na kuzitoa
 zile zilizopitwa na wakati ili kuharakisha ufanisi wa utoaji wa 
taarifa, kuweka busta kwa baadhi ya maeneo ili televisheni ya taifa 
(TBC) iwe bora zaidi na kuongeza urefu wa minara ili matangazo yafike 
mbali zaidi.
Waziri Nape 
ameamua kuboresha urefu wa minara ili matangazo yafike mbali kwani mikoa
 mingi ya pembezoni imepakana na nchi ambazo teknolojia zao za 
mawasiliano ni kubwa kiasi kwamba wananchi wengi wa mipakani 
wanasikiliza redio za nchi jirani na kuacha kusikiliza redio za hapa 
nyumbani Tanzania.
Katika 
harakati za kuboresha tasnia ya habari, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos
 Makalla ameelezea changamoto na jinsi alivyopanga mikakati ya kusaidia 
na kuiboresha tasnia hii mkoani kwake ambapo alikaririwa akisema “Mkoa 
wangu unaomba kibali cha kuajiri maafisa habari ili kila Halmashauri iwe
 na afisa habari wake pia naahidi kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya 
kununua vitendea kazi vya maafisa hao”.
Wakati huo 
huo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa wananchi 
kuanzisha vituo vya utangazaji 19 katika Wilaya na Halmashauri 
mbalimbali na wamewaomba wadau kutuma maombi kabla ya Aprili 29 mwaka 
huu.
Akiongea 
katika mkutano wa Mhe.Nape na wadau wake, Meneja wa Mamlaka ya 
Mawasiliano Tanzania Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Lilian Mwangoka 
alisema, “Mamlaka ya Mawasiliano ipo tayari kushirikiana na wananchi 
kuongeza vituo vya utangazaji ili kuongeza idadi ya vituo na kuongeza 
fursa katika ukusanyaji wa kodi”.
Aidha, 
Waziri Nape amesisitiza suala la maafisa habari kupewa ruhusa ya 
kushiriki katika vikao vya maamuzi ili wajue mambo yanayoendelea katika 
ofisi zao kwani kufanya hivi kutasaidia maafisa habari kuacha kuwakimbia
 waandishi wa habari na badala yake kuwapa taarifa kamili ili 
wakawajulishe wananchi taarifa sahihi kuhusu Serikali yao.
Akiongea kwa
 kujiamini Waziri Nape amehakikisha kuwa yote yatawezekana maana fedha 
za kutatua kero hizo zitapatikana kwa kuwa Mhe.Rais tayari alifanya 
maamuzi ya kuziamuru taasisi zote za Serikali zilizopewa huduma ya kutoa
 matangazo yao kupitia Televisheni ya Taifa bila kulipa waanze kulipa 
madeni yao mara moja kwa hiyo fedha hizo ndizo hasa zitatumika katika 
kuboresha tasnia hii.
Sasa ni 
wakati wa maafisa habari pamoja na waandishi wa habari wote nchini 
kuunga mkono jitihada za waziri wetu kwa kufanya kazi za kukusanya na 
kutawanya taarifa kwa ufanisi na usahihi wa hali ya juu  ili kuifanya 
jamii ielewe umuhimu wetu pamoja na kukuza uchumi wa nchi kupitia 
taarifa tunazozitoa kwenye vyombo vya habari.
Wahenga 
wanasema Taifa lisilo na taarifa haliwezi kukua kiuchumi, litadumaa. 
Hivyo tumuunge mkono Mzalendo huyu ili kukuza na kuinua Tasnia ya Habari
 na ionekane kweli kuwa muhimili wanne wa dola ambao unachangia kwa 
kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo.
i
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni