Taasisi ya Graca Machel mdau muhimu wa elimu ya mtoto wa kike nchini, ikiwa na lengo la kuielimisha jamii.
By Newsroom on April 18, 2016
Mtoto huanza kujifunza kulingana
na mazingira yake yanayomzunguka, mafunzo hayo yanamuwezesha kupata
uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile ili
aweze kuyamudu mazingira yake.
Hali hiyo inajenga dhana ya kupata elimu kulingana na mazingira ambayo hujulikana kama elimu isiyo rasmi.
Ni vema ikaeleweka kwamba
tunapozungumza kuhusu watoto, tunazikusudia jinsia zote mbili, yaani
watoto wa kike na wale wa kiume. Katika hali halisi ndani ya maisha ya
kijamii, elimu ni nyenzo ambayo hutumiwa kupitisha maarifa, ujuzi na
maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine bila kujali jinsia.
Elimu kwa watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini katika mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania.
Manufaa hayo ya elimu kwa watoto wa kike yanaweza kuonekana kwa mtu binafsi, familia zao, jamii yote na taifa kwa ujumla.
Ni dhahiri, manufaa
yanayopatikana kupita elimu ni mengi katika jamii ikiwemo kupunguza
idadi ya watoto ambao wanawake hujifungua, kupunguza idadi ya vifo vya
watoto wadogo, kupunguza idadi ya vifo vya akina mama, kuwalinda dhidi
ya maambukizo ya VVU/UKIMWI na kuongeza idadi ya wanawake wenye kazi na
mapato ya juu ambayo hudumu kwa vizazi vingi.
Hakika ukimuelimisha mtoto wa
kike, umemsaidia kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi bora kwa manufaa yake,
familia yake na hata taifa.
Hali hii imechukua sura mpya
nchini Tanzania ambapo Serikali, watu binafsi, mashirika ya dini na
taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zimekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu ambayo ndiyo kinga na urithi
pekee ambao hawezi kunyang’anywa wala kugawana na mtu mwingine ndani ya
familia na hata jamii inayomzunguka.
Sura hiyo mpya imeoneshwa na
Mfuko wa Graca Machel (Graca Machel Trust) ambao umejikita katika
kusaidia wanawake na watoto nchi kadhaa Barani Afrika.
Taasisi hiyo imebisha hodi na
kukaribishwa nchini Tanzania mkoa wa Mara ambapo imeazimia kuwasaidia
watoto wa kike 20,000 ndani ya mkoa huo ambao watanufaika kwa fursa ya
kupata elimu.
Mapema Aprili 6, 2016 Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Mhe. George Simbachawene alibainisha Mfuko wa Graca Machel umeamua
kuwasaidia watoto wa kike wa mkoa wa Mara mara baada ya kukutana na
kufanya mazungumzo na Mama Graca Machel alipomtembelea ofisini jijini
Dar es salaam.
Moyo huo na juhudi za kusaidia
watoto wa kike ni wa kizalendo ambapo Waziri mwenye dhamana na tawala za
mikoa Simbachawene anasema “Ni fursa nzuri ya kushirikiana na wadau wa
ndani na nje ya nchi kuwasaidia watoto wetu wa kike kielimu ambayo
itawasaidia kutoka katika jamii ya umasikini na kuhakikisha wamepata
fursa ya kuvuka umri wa vishawishi na maamuzi yasiyo sahihi bila shida
na pingamizi lolote”.
Watoto hao wanaotarajiwa
kunufaika na Mfuko huo mkoani Mara watatoka katika shule 104. Hatahivyo
mfuko huo unatarajiwa kuwafikia watoto wa kike wengi zaidi mara baada ya
kuanza kutoa huduma hiyo mkoani humo.
Fursa hiyo adhimu na ni ya
kuungwa mkono hasa na wadau wa elimu mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla
kwani kwa Mama Machel haikuwa lazima kuichagua Tanzania, bali hekima na
busara yake inatokana ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na
Msumbiji kwa kuzingatia mchango mkubwa wa Tanzania kwa nchi hiyo tangu
awali.
Uhusiano huo mzuri uliopo kati ya
nchi hizo mbili ni wa kihistoria kwani pamoja na harakati za ukombozi
Kusini mwa Afrika, wananchi wa nchi hizo walishirikiana katika shughuli
mbalimbali chini ya mwavuli wa unasaba na ushirikiano katika biashara
na tamaduni kwenye miji ya Unguja, Kilwa, Lindi na Mtwara kwa upande wa
Tanzania na katika miji ya Chilimbo, Tete, Pemba na Sofala nchini
Msumbiji.
Jambo jema hakika ni lazima
kusifiwa na kushangiliwa ili liweze kufana na kuwa na manufaa mengi
zaidi, ndio maana Waswahili husema “Chanda chema huvishwa pete”.
Mama Machel amekuwa mfano mwema
wa kuigwa maana anajali, anathamini na anatambua mchango wa mkoa Mara
katika historia ya maisha yake na nchi yake kwa kuwa ndio mkoa
alipozaliwa Mwasisi wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
aliyeongoza harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Ndiyo maana Mama Machel
anasisitiza kwa kusema “Lengo ni kuwabakisha watoto wa kike shuleni ili
wapate elimu, ni lazima tusaidiane wote, tuna kila sababu ya
kusaidiana”.
Alipokuwa mkoani Mara katika chuo
cha ualimu Tarime mapema Mwezi Aprili mwaka huu, Mama Machel ameitaka
Tanzania kuwa na mpango wa utekelezaji katika kuhakikisha
wanashughulikia changamoto ambazo zinaweza kuwa sababu za mimba za
utotoni kwa wasichana.
Mama Machel alisema kuwa iwapo
Tanzania na nchi nyingine za Afrika watu wataungana kwa pamoja kila mtu
atimize wajibu wake kwa nafasi yake, kwa utaratibu huo wa kujipanga ili
kusaidia kundi hilo la wasichana ni hakika mambo yaliyoko mbele
yatafanyiwa kazi vilivyo na ndoa za utotoni zitatokomezwa.
Mama Machel alisema kuwa watoto
wa kike wanatakiwa kupata nafasi ya kusoma na sio kuolewa wakiwa na umri
mdogo, hivyo Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha inakuwa bega kwa
bega kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki zake za msingi zikiwamo za
elimu.
“Katika mapambano yoyote, kitu
kikubwa na cha msingi ni elimu! Elimu pekee ndiyo itamaliza mila zote
potofu tutafute mbinu mbadala kuhakikisha watoto wanasoma, walimu wawe
ni waangalizi wa watoto, asipofika shule mzazi aulizwe maana watoto wote
wanajulikana wanakotoka, tunahitaji tuongeze idadi ya watoto wafike
hadi elimu za juu”alisema Mama Machel.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Magesa
Mulongo alimshukuru Mama Machel kwa moyo wake wa kizalendo kwa kuupa
heshima mkoa huo kupitia taasisi hiyo.
Akiwa mkoani Mara, wilayani
Tarime Mama Machel alisisitiza jamii iondokane na suala la ukatili wa
kijinsia ukiwamo ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni kwa lengo la
kumlinda mtoto wa kike na kumpa nafasi ya kutimiza ndoto zake.
Hatua hiyo ilitokana na Mama
Machel kujionea hali ilivyokuwa katika Shule ya Msingi Masanga ambapo
alizungumza na wananchi, wanafunzi na mabinti waliokimbia ukeketaji
katika msimu wa tohara na kuhifadhiwa kwenye Kituo cha Termination Of
Female Genital Multilation (TFGM) Masanga wilayani Tarime mkoani humo
ambacho kimeanzishwa na Kanisa Katoliki katika kumuokoa mtoto wa kike na
maswahibu ya minyororo ya mila na desturi zisizofaa.
Katika kuthamini na kuupokea kwa
vitendo mchango wa Mama Machel, Serikali, viongozi wa dini na wananchi
wa mkoa wa Mara wamesaini mkataba wa kutekeleza ili kuhakikisha watoto
wa kike wanapata elimu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa
dhana ya mtoto wa kike kuchunga mifugo zifutiliwe mbali, kila taasisi
imepewa jukumu lake, Serikali kupitia mkoa na halmashauri, Wizara ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) viongozi wa dini na wananchi.
Pande hizo kila mmoja wamesaini
pamoja mkataba wa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kwa kuziweka
pembeni imani potofu ambazo ndio zimekuwa kikwazo kwa mtoto wa kike
kupata elimu.
“Halmashauri wanawajibu wa
kuhakikisha watoto wanaotambuliwa na wasitoroke katika vituo na shule
wanaposoma, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na TAMISEMI
wajibu wao ni kuandaa sera zinazombeba msichana asitoroke shuleni,
wajibu wa Serikali za mitaa na vitongoji ni kuhakikisha kila mtoto
anapata haki yake ya elimu wakati mkoa jukumu lake ni kuhakikisha
unafanya uratibu wa wadau wote wanahakikisha mtoto wa kike anapata
elimu” alisema Mulongo.
Mtazamo huo wa Serikali na wadau
wengine wa elimu unaungwa mkono na Mwakilishi wa Shirika la Mfuko wa
Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem ambapo
aliwahimiza watoto walio katika kituo cha Masanga kutokata tamaa bali
waweze kushikilia msimamo wa ndoto zao kwa kushirikiana na wazazi
waliopata mabadiliko katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aliongeza kuwa mwaka 2014 ulikuwa
ni mwaka wa matumaini baada ya wazee wa mila kusema wameondokana na
vitendo vya ukeketaji ikiwa ni pamoja na wavulana kufanyiwa tohara.
Mwakilishi huyo alisema vyombo
vya kisheria vya mahakama pamoja na polisi vitaendelea kupewa mafunzo
juu ya kupinga vitendo hivyo kwa lengo la kuvikomesha kabisa.
“Tanzania ni nchi ndogo na idadi
ya watoto waliochini ya miaka 17 ni nusu ya Watanzania kwa hiyo hatuna
budi kuwalinda watoto hao kwa kuwapenda na kuwathamini,”alisema Dk
Kanem.
Juhudi hizo za elimu kwa mtoto wa
kike zinachagizwa na Serikali Tanzania ambayo imekusudia kuleta
mapinduzi ya kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025.
Kusudio hilo la Serikali
linaongozwa na Sekta ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo kwa kwa
mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa
Maendeleo ya Taifa 2011/12 hadi 2024/25, inatarajiwa kuleta maendeleo ya
haraka ya rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya
Watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya
Taifa lipate maendeleo na kuwa lenye uchumi wa kati na shindani ifikapo
mwaka 2025.
Sera hiyo mpya imeweka dira ya
elimu na mafunzo nchini ambayo inayojali jinsia zote kupata elimu kwa
usawa na kusimamia nchi iwe ya maendeleo endelevu.
Dira hiyo inasimamia uhalisia
“Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na
mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa”
anapaswa kuzingatia utaifa kwanza.
Ili kuhakikisha elimu inawafikia
watoto wote, Serikali imeweka bayana katika Sera ya Elimu ya mwaka 2014
yenye lengo la kuwa na usawa wa kijinsia katika elimu na mafunzo. Pia
Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha usawa wa
kijinsia katika elimu na mafunzo unazingatiwa.
Hapa nchini taasisi binafsi
zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu licha
ya mazingira magumu aliyonayo.
Miongoni mwa taasisi za
kupongezwa na kuigwa mfano kutokana na kutoa umuhimu wa mtoto wa kike
kupata elimu ni ya Graca Machel Trust, Wanawake na Maendeleo (WAMA)
inayoongozwa na Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Mama
Salma Kikwete, taasisi ambayo inasimamia Shule ya Sekondari
WAMA–Nakayama iliyopo Kijiji cha Nyamisati Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa
Pwani na Shule ya Sekondari ya WAMA- Sharaf iliyopo Mitwero katika
Manispaa ya Lindi.
Taasisi nyingine inayosimamia na
kutoa elimu kwa mtoto wa kike ni Mama Clementina Foundation (MCF) yenye
makao yake makuu mkoani Kilimanjaro inayoongozwa na aliyewahi kuwa Mkuu
wa Shule ya Sekondari Weruweu Dkt. Maria Kamm.
Taasisi ya MCF inatoa elimu kwa
mtoto wa kike kupitia shule za Kilimanjaro Academy iliyopo mjini Moshi
mkoani Kilimanjaro na shule ya sekondari ya Wasichana MCF Makambako
iliyopo Makambako.
Katika harakati za kuhakikisha
mtoto wa kike anapata elimu bora ili aweze kujitegemea, kujenga familia
bora na kuwa mchango chanya katika kujenga taifa imara kiuchumi, taasisi
hizo zimeonesha njia ya kuwa nuru ya mtoto wa kike katika kupata elimu.
Sera ya elimu nchini, inasisitiza
uwiano wa uandikishaji wa wanafunzi katika elimu ya msingi kwa wavulana
na wasichana uwe takribani 1:1, elimu ya sekondari uwe ni 1:0.9 wakati
elimu ya juu ni 1:2.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa
mwendelezo wa idadi ya wanafunzi kutoka ngazi moja kwenda ngazi
inayofuata kwa wasichana uwiano huo umekuwa ukipungua.
Ingawa kiwango cha mdondoko
kinaathiri wavulana na wasichana, tathmini inaonyesha kuwa wasichana
wana uwezekano mkubwa zaidi wa kukatisha masomo hususan wanapofikia
katika madarasa ya juu kuanzia darasa la tano.
Ndiyo maana taasisi za Graca
Machel, WAMA na MCF zimeona kuna umuhimu wa kumsomesha mtoto wa kike kwa
ushiriki katika fursa za elimu na mafunzo hatua ambayo itawasaidia
wasichana kupata nafasi za usimamizi na uendeshaji katika sekta
mabalimbali nchini.
Kwa taarifa za mwishoni mwa mwa
2015 jumla ya wanafunzi 503,914 kati ya wanafunzi 518,034 waliofaulu
kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016.
Ki uhalisia, idadi ya wanafunzi
waliojiunga kidato cha kwanza mwaka huu sawa na asilimia 97.3 ambao
wamepata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za
Serikali.
Ili kuhakikisha wanafunzi hawa
wanapata elimu inayotarajiwa Serikali imetenga Sh. bilioni 131 kwa ajili
ya shughuli za uendeshaji shule, chakula kwa wanafunzi wa bweni na
fidia ya ada ya mitihani kwa kipindi cha kuanzia mwezi Desemba mwaka huu
hadi Juni mwaka 2016.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, alisema
kati ya wanafunzi waliochaguliwa, wasichana ni 255,843 sawa na asilimia
99.2 na wavulana ni 248,076 sawa na asilimia 97.7
Sura hiyo inaonesha idadi ya
wasichana waliojiunga kidato cha kwanza ni kubwa kuliko ya wavulana kwa
zaidi ya asilimia 1.5, ongezeko ambalo linaonesha kuwa Tanzania iko
kwenye hatua nzuri ya uelewa wa kumpatia elimu mtoto wa kike.
Siyo wanafunzi wote wanaomaliza
shule ya msingi, kidato cha nne na kidato cha sita wanajiunga na shule
za Serikali, ndio maana taasisi nyingine zinatoa mchango wao katika
kuhakikisha watoto wa kike nchini wanapata elimu katika ngazi
mbalimbali.
Hatua hiyo ya Tanzania inaungwa
mkono na mataifa duniani ndio maana ikaanzishwa Siku ya Kimataifa ya
Mtoto wa Kike ili kutambua haki za watoto wa kike na kuimarisha jitihada
za kimataifa za kutokomeza unyanyasaji, ubaguzi na ukatili wa kijinsia
na tofauti ya fursa za kiuchumi zinaowaathiri zaidi watoto wa kike.
Takwimu zinaonyesha kuwa nchi zinazowaelimisha watoto wa kike kwa usawa huwa na ustawi na maendeleo makubwa zaidi.
Kwa kuwapa watoto wa kike mwaka
mmoja wa ziada wa masomo baada ya muda wa wastani katika elimu ya msingi
utawaongezea kati ya asilimia 15 na 20 ya kipato chao na mwaka mmoja wa
ziada katika elimu ya sekondari utaweza kumuongezea mtoto wa kike
kipato chake kwa kati ya asilimia 15 na 25.
Aidha, watoto wa kike walio soma
hukawia zaidi kuolewa na kupata watoto, Hali kadhalika, kuna uwezekano
mkubwa zaidi kwa wasichana waliopata elimu hapo baadaye kuwa na watoto
wenye afya njema na ambao pia watapata elimu nzuri.
Ndio maana Mke wa Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu ya Nne Mama Kikwete aliwahi kusema “……. Mtoto wa
Mwenzio ni mwanao, tunamaanisha sote tunapaswa kuwajibika kwa ajili ya
ulinzi na ubora wa maisha ya watoto toka wakiwa tumboni hadi
wanapozaliwa na kusimamia maadili yao wanapoendelea kukua”.
Mama Salma alitoa msisitizo kwa
Watanzania na kuwaasa waache kulaumiana juu ya maadili ya vijana, na
kuwaomba warejee malezi ya wazee ili kila mmoja awajibike kumuona mtoto
wa mwenzake kuwa ni wa kwake na kumrekebisha pale anapokosea.
Ni wajibu wa kila mpenda
maendeleo kujua kuwa ni fursa ya pekee kumuelimisha mtoto wa kike wajibu
na dhamana ya jamii kutambua ukimuelisha mtoto wa kike ni kuelimisha
jamii nzima.
Ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka
huu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila
mwaka Machi 8 imesisitiza kuwa “Usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa
wote”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni