SERIKALI YAZUIA UINGIZAJI HOLELA WA MCHELE
Ametoa agizo hilo leo mchana 
(Jumatano, Aprili 27, 2016) wakati akijibu hoja za wabunge na 
kuhitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa 
mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.
“Napenda kuviagiza vyombo vya 
dola viendelee kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu hasa katika mwambao wa 
Bahari ya Hindi ili kuzuia uingizwaji holela wa mchele wa magendo kutoka
 nje ya nchi. Endapo patatokea upungufu wa mchele nchini, Serikali 
itaangalia uwezekano wa kuruhusu kuagiza mchele kutoka nje,” amesema.
Waziri Mkuu amesema katika 
kipindi cha miaka sita iliyopita, kumekuwa na ongezeko la asilimia 14 
katika uzalishaji wa mpunga hapa nchini na hivyo kufanya kiwango cha 
uzalishaji kiwe ni kikubwa kuliko mahitaji.
“Takwimu za uzalishaji mpunga 
zinaonesha kuwepo ongezeko katika kipindi cha miaka sita iliyopita 
ambacho kiliongezeka kutoka tani 1,699,825 mwaka 2009/2010 hadi kufikia 
tani 1,936,909 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 14. Katika 
kipindi chote hicho, kiwango cha uzalishaji wa mpunga kimekuwa kikubwa 
kuliko mahitaji,” amesema.
“Kutokana na mwenendo huo mzuri 
wa uzalishaji wa mpunga hapa nchini, Serikali ilisitisha kutoa vibali 
vya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi tangu Machi, 2013. Hatua hii 
itasaidia wakulima wetu kupata soko la uhakika na bei nzuri, jambo 
ambalo linawaongezea kipato na pia kuwahamasisha kuongeza uzalishaji 
zaidi,” amesema.
Akizungumzia kuhusu deni la sh. 
bilioni 134 ambalo Serikali inadaiwa na Bohari ya Dawa nchini (MSD), 
Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kulishughulikia deni hilo kwa 
kumwelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ahakiki
 deni hilo. “Mpaka sasa CAG amehakiki madai ya jumla ya shilingi bilioni
 67 na kazi ya uhakiki inaendelea.”
Akifafanua kuhusu vigezo 
vilivyutumika kugawanya majimbo mapya ya uchaguzi, Waziri Mkuu alisema 
mwaka 2015, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea maombi 77 ya kuanzishwa 
majimbo mapya, ambapo Halmashauri 37 ziliwasilisha maombi ya kugawa 
majimbo ya uchaguzi na maombi 40 yalitoka katika majimbo yaliyokuwepo 
yakiomba kugawanywa. Kati ya maombi yaliyowasilishwa, maombi 35 tu ndiyo
 yalikidhi vigezo na yalistahili kugawanywa.
“Kutokana na ongezeko la 
Halmashauri mpya ambazo kisheria ni majimbo ya uchaguzi, ongezeko la 
idadi ya wabunge wanawake wa viti maalum na uwezo wa ukumbi wa Bunge; 
Tume iliamua kutumia vigezo vitatu tu ili kupata idadi ya majimbo 
yanayoweza kugawanywa. Vigezo hivyo ni: Wastani wa idadi ya watu 
(Population Quota), mipaka ya kiutawala na uwezo wa ukumbi wa Bunge,” 
alisema.
Waziri Mkuu alisema chini ya 
mchakato huo, Tume ilianzisha majimbo mapya 25  ambapo majimbo 19 
yalitokana na ongezeko la Halmashauri mpya; na majimbo sita yalitokana 
na kigezo cha wastani wa idadi ya watu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu 
alibainisha kwamba kwa sasa Serikali haina mpango wa kuongeza maeneo 
mapya ya utawala zikiwemo wilaya na mikoa mipya kwa sababu bado 
inaendelea kujengea uwezo wa rasilmali watu na vitendea kazi katika 
maeneo mapya ya utawala yaliyopo hivi sasa.
Bunge limepitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2016/2017.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni