Balozi Amina Salum Ali awataka watendaji Wizarani kuleta mabadiliko katika utendaji wa kazi
WAZIRI
wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali
amewataka watendaji wa Wizara hiyo kuleta mabadiliko katika utendaji wa
kazi, ili kuifanya Zanzibar iweze kufikia katika uchumi wa kati.
Alisema
kuwa, Wizara imeandaa sera mbali mbali ambazo zinaweza kuifanya
Zanzibar kufikia uchumi wa kati, ikiwa ni pamoja na sera ya biashara,
viwanda na sera ya mpangokazi ambao utekelezaji wake utaanza leo (jana).
Akizuzungumza
na watendaji wa Wizara hiyo pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo
tofauti katika ukumbi wa Makonyo Chake Chake, alisema ipo haja kwa
watendaji wake kujibadilisha kwa kuwa na sera madhubuti ya kuwa na
viwanda vikubwa, ambavyo vitaifanya Zanzibar kufikia uchumi wa kati.
Alieleza
suala la kukuza viwanda Zanzibar kuwa, Wizara inataka kukiendeleza
kiwanada cha sukari Mahonda, kujenga kiwanda cha maziwa, kiwanda cha
Zanzibar Milin na kiwanda cha makonyo ambacho hutoa mafuta ya karafuu,
makonyo na mafuta mengine ya mimea.
”Kuna
mambo lazima tuyabadilishe, kwanza utendaji wa kazi wa silka ya kawaida
ambapo wanataraji matokeo yatakayobadilisha maisha ya wananchi,
utendaji utakaotuletea mapato na maendeleo, hii ndio itakayoifanya
Zanzibar kufikia uchumi wa kati”, alisema Balozi huyo.
Balozi
Amina aliwataka watendaji hao kufanya kazi ya ziada katika kubadilisha
Zanzibar na kuwa ya maendeleo zaidi kwa kutumia bidhaa zinazotokana na
kilimo.
Alisema
kuwa, asilimia 85 ya viwanda Zanzibar ni vya wananchi, hivyo ni vyema
juhudi zikatendeka katika kuvibadilisha na kufikia viwanda vikubwa,
kwani Zanzibar inayo nafasi kubwa ya kuzalisha na kuuza bidhaa
zinazotokana na kilimo.
”Tunatakiwa
tufanye kazi ya kuibadilisha Zanzibar kwa kutumia bidhaa zinazotokana
na mimea, kwani uzalishaji unataka bidii kubwa, hivyo ipo haja ya
kuwashirikisha wa Zanzibar na nje yake kwa kutembeleanaili kuona wenzetu
wanafanya nini na sisi tuweze kufuata”, alieleza Waziri huyo.
Waziri
huyo alisema, ipo haja ya kutolewa elimu kwa wajasiriamali na
kuwezeshwa kwa kupitia sehemu za nje zenye maeneo ya kiuchumi ili
kujifunza mambo mbali mbali ambayo wataiga kutoka huko.
”Ili
tufikie huo uchumi wa kati ni lazima Serikali ijipange kuwawezesha
wajasiriamali na wawekeze kupitia sehemu za wenzao ka kuwatembeza,
kupatiwa elimu na soko, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwetu”,
alieleza.
Akizungumzia
suala la karafuu alieleza kuwa, Zanzibar imefanya vizuri kwa miaka
mitano iliyopita kwa uzalishali wa zao hilo, ambapo Serikali imenunua
tani elfu 20 kutoka kwa wananchi, ikiwa na thamani ya shilingi billioni
285.89.
”Serikali
imejiandaa vizuri na bei itaendelea kuwa ile ile kama alivyoahidi Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed
Shein, lengo ni kuivusha Zanzibar kwenda katika uchumi wa kati”,
alisema.
Alisema
bei ya ununuzi wa zao la karafuu haijashushwa kama baadhi ya wananchi
wanavyodai, kwani hiyo ni ahadi ya serikali katika kustawisha maisha ya
wakulima wa zao hilo.
Aliwataka
wananchi kuacha kabisa uuzaji wa karafuu kwa njia ya magendo na
waendelee kuuza hapa Zanzibar, kwani fedha zinapoingia serikalini
huwafaa wananchi wenyewe kutokana na huduma za kijamii.
”Pia
tufanye biashara inayokubalika kimataifa, karafuu zetu tusuzichanganye
na makonyo kwa sababu kuna ushindani mkubwa wa soko, hivyo ni vyema
tukazianika sehemu sahihi na kuwa kavu kabisa”, alifahamisha.
Aidha
alisema kuwa, Wizara itakuwa na utaratibu wa kuangalia bei ya vyakula
na kuhakikisha kwamba vyakula vinavyoingia vinakuwa na viwango vya
kimataifa pamoja na usafi.
”Tuko
tayari kuingia katika mapambano, kwa nini tusiwe na viwango vya vyakula
vinavyoingia wakati nchi nyengine wanavyo, tutahakikisha zinaingia
bidha zenye ubora na viwango”, alisisitiza.
Mwandishi
wa habari Salim Ali Mselem kutoka redio Istiqama akiuliza swali,
alisema serikali itapanga sera ipi ambayo itawawezesha wananchi wote
wakati wanapoimarisha upande huu, wananchi hukwama kwa upande wapili.
”Zao
la karafuu limeongezwa bei lakini na kodi inaongezeka kwa
wafanyabiashara siku hadi siku, jambo ambalo wenye kipato cha chini
wanaumia, kwa mfano wafanyabiashara wa sokoni hapa Chake Chake wanatozwa
kodi elfu 60 badala ya elfu 30, kweli wananchi wanawezeshwa hivi”,
alihoji Salim.
Nae
Nasra Mohamedi kutoka ZBC televisheni akitoa hoja yake kuwa, kama
iliyoelezwa wajasiriamali wapo asilimia 85, hivyo serikali itafute njia
mbadala ya kuwawezesha ili kutumia njia ya digital katika kufanya kazi
zao ili kufikia maendeleo zaidi.
Waziri
Amina alikuwa kwenye ziara ya kutembelea vitengo mbali mbali vya
Wizara, ambapo aliona jitihada mbali mbali zinazofanywa na wajsiriamali
na kujionea mambo mbali mbali ambayo hufanywa katika kiwanda cha makonyo
Wawi Chake Chake, ikiwa ni pamoja na mafuta yanayotengenezwa kwa
karafuu na makonyo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni