TAMKO LA JUKWAA LA WAHARIRI JUU YA MATANGAZO YA BUNGE
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri 
TEF Bw. THEOPHIL  MAKUNGA akitoa tamko la wahariri kwa waandishi wa 
habari kuhusu urushwaji wa matangazo ya vikao vya bunge la bajeti 
vinavyoendelea mkoani Dodoma, kushoto ni makamu mwenyekiti wa jukwaa 
hilo Bw.DEODATUS BALILE.
……………………………………………………………………………………………………………..
Bodi ya Jukwa la Wahariri 
Tanzania (TEF) iliyokaa Ijumaa Aprili 22, 2016 jijini Dar es Salaam 
pamoja na mambo mengine ilijadili hali ya mwenendo wa tasnia ya habari 
nchini hasa juu ya haki ya wananchi kupata habari.
Katika kujadili hali hiyo, TEF 
imeguswa kwa namba ya kipekee kabisa na mwenendo mzima wa urushaji wa 
bahari za Bunge kwa njia ya redio na luninga, hususan katika mkutano wa 
tatu wa Bunge la 11 unaoendelea mjini Dodoma kwa sasa.
Itakumbukwa kwamba Muhimili wa 
Bunge kupitia Kitengo chake cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Aprili 15 
2016 ulitoa taarifa kwa umma ikieleza utaratibu mpya ambao sasa umeanza 
kutumika katika kurusha matangazo ya redio na luninga kutoka Bungeni.
Katika taarifa hiyo, Ofisi ya 
Bunge ilisema kuwa imeamua kuboresha mfumo wa urushaji wa Matangazo ya 
Bunge kwa Bunge lenyewe kurusha Matangazo ya Vikao vyake pamoja na 
Vipindi mbalimbali vyenye Maudhui kuhusu Shughuli za Bunge ambazo 
hazijapata fursa ya kufahamika vyema kwa umma kuanzia katika Mkutano wa 
Bunge la Bajeti unaoendelea sasa.
Ofisi hiyo ilisema kuwa mfumo huo
 mpya ni Utamaduni wa kawaida kwa kila Bunge hususani Mabunge ya Nchi 
Wanachama wa Jumuiya ya Madola kuwa na Studio zake kwa lengo la kurusha 
Matangazo ili yawafikie wadau kwa lengo la kurusha kupitia vituo vyao. 
Kwa maana hiyo, Bunge lilisisitiza kuwa chini ya utaratibu huo mpya, 
jukumu la kurusha Matangzo ya Vikao vya Bunge litafanywa na Bunge 
lenyewe kupitia FEED MAALUM ili kurahisisha kila Kituo cha Radio na 
Televisheni kupata Matangazo hayo kwa sehemu walipo bila kufunga Mitambo
 yao Bungeni Dodoma.
Katika kutekeleza uamuzi huo na 
mfumo huo mpya, kila kituo cha Televisheni na Redio sasa watatumia 
Masafa ya Matangazo ya Bunge (Frequencies) bure kupitia FEED MAALUM 
itakayorushwa na Satellite ya INTELSAT 17 ambayo iko nyuzi 66 Mashariki 
kwa masafa maalum ambayo pia yaliwekwa wazi.
Kwa mantiki hiyo, Bunge sasa 
limezuia vituo vyote vya televisheni nchini kupeleka kamera zake ndani 
ya Bunge kwa kuwa habari hizo zitapatikana kwenye feed maalum ambayo ni 
ya Bunge ambayo inasimamiwa na waandishi wa Bunge ambao pia ndio 
wanaamua nini kionyeshwe kwa utashi wao.
Baada ya kutafakari hatua hizi mpya za Bunge na baada ya kufuatilia kile kinachorushwa, mambo kadhaa yamethibitika:-
Mosi, habari kutoka ndani ya Bunge sasa zinachujwa mno kupitia mfumo huu mpya wa feed maalum;
Pili, ubora za picha zinazorushwa kupitia feed hii nao ni wa kiwango cha chini pia;
Tatu, kwa mantiki ya kawaida 
kabisa, hatua hizi zote zimepunguza na kukwaza haki ya wanahabari 
kufanya kazi yao kwa uhuru, lakini pia inawanyima wananchi haki ya 
kupata kwa uhakika na bila kuchujwa kile kinachofanywa na wawakilishi 
wao.
Kwa kuzingatia haya yote, TEF inasema bayana kwamba:
- Hatua hizi mpya za kuzuia kamera za televisheni kuingia Bungeni ni hatua za dhahiri kabisa za kukwaza uhuru wa habari nchini na kukuza censorship nchini. Hali hii haisaidii siyo Bunge tu, bali hata wabunge, wananchi na taifa kwa ujumla katika kupiga hatua za kweli katika kujenga demokrasia na kulinda haki za kupata habari na uhuru wa kujieleza nchini;
- TEF imeanza kuingiwa na hofu kwamba sababu za awali zilizokuwa zimetolewa za kuzuia utangazaji wa moja kwa moja wa Bunge kupitia TBC kwa sababu ya gharama, huenda hazikuwa za dhati. Hali hii imejionyesha hasa baada ya vituo binafsi vya televisheni kujitokeza na kuendelea kuonyesha vikao vya bunge moja moja, lakini navyo sasa vimenyimwa fursa hiyo kwa utaratibu huu mpya wa feed maalum.
- Ni dhahiri sasa, ushiriki wa wananchi katika kufuatilia mwenendo wa Bunge na wabunge wao umekwazwa sana kwa hatua hizi mpya na kwa maana hiyo, kupunguza ushiriki wa wananchi katika mfumo wa utawala wa nchi yao.
Kwa kuzingatia haya yote, TEF 
inatoa rai kwa uongozi wa Bunge kufikiria upya hatua hizi za kuzidi 
kufunika shughuli za Bunge kwenye blangeti zito la usiri na censorship, 
hivyo uruhusu kituo chochote cha televisheni chenye nia, uwezo na 
utayari wa kurusha matangazo ya Bunge moja moja bila kulazimika kujiunga
 na feed maalum iliyoanzishwa.
Tunaamini kwamba kama hali hii ya
 kutumia feed maalum itaachwa iendelee hakika Tanzania kama taifa 
tunapiga hatua nyuma kwa yale mazuri machache tuliyokuwa tumeyafikia, 
mojawapo, uhuru wa Bunge kuendesha mambo yake kwa uhuru na uwazi mkubwa 
hivyo kuwa mfano mojawapo wa taasisi za umma zinazojiendesha kwa uwazi.
Imetolewa leo, Jumapili Aprili 24 2016 jijijni Dar es Salaam na Jukwaa la Wahariri Tanzania.
Theophil Makunga                 Neville Meena
Mwenyekiti                             Katibu
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni