Ijumaa, 29 Aprili 2016

Bomba la mafuta kukamilika Juni mwaka 2020.

 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akielezea uzoefu wa Tanzania kwenye
ujenzi wa miradi  ya mabomba ya gesi na mafuta katika mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Maendeleo  ya Madini Nchini   Uganda, Mhandisi  Irene  Muloni na kulia ni  Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo  ya Madini Nchini  Uganda, Dk. Fred Kaliisa (kushoto)
akifafanua  jambo katika kikao hicho. Kulia ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini   Uganda, Mhandisi Irene Muloni.
Balozi wa Uganda Nchini Tanzania, Dorothy Hyuha akifafanua jambo katika mkutano huo.
 Wataalam kutoka Wizara, taasisi na makampuni ya mafuta kutoka Tanzania na Uganda wakifuatilia
kwa makini mada iliyokuwa inawasilishwa na mwakilishi kutoka kampuni ya Total
katika mkutano huo.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu
  utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika bandari ya  Tanga nchini
Tanzania. Kulia ni Waziri wa Nishati na Maendeleo  ya Madini Nchini   Uganda, Mhandisi  Irene Muloni.
 Waziri wa Nishati na Maendeleo  ya Madini Nchini   Uganda, Mhandisi  Irene
Muloni (kulia)  akifafanua jambo alipokuwa  akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kukamilika kwa mkutano huo.  Kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo.
…………………………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika bandari  ya Tanga nchini Tanzania linatarajiwa kukamilika  mwezi Juni mwaka  2020.
Hayo yalielezwa na  Waziri wa Nishati na Madini,  Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa   akizungumza na waandishi wa habari  mara baada ya kufanyika kwa mkutano kati yake na Waziri wa Nishati na Maendeleo  ya Madini Nchini   Uganda, Mhandisi  Irene  Muloni  aliyeambatana na ujumbe wake katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili mpango wa  mradi wa ujenzi wa bomba la  mafuta kutoka Hoima nchini  Uganda hadi katika  bandari ya  Tanga  nchini Tanzania ambapo ulikutanisha wataalam kutoka nchi zote mbili, ambao ni  wa  ardhi, miundombinu, maji, ujenzi, uchumi,, maji barabara pamoja na makampuni ya  mafuta.
Profesa Muhongo alisema  kuwa mara baada ya marais wa Tanzania na  Uganda kukubaliana kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta,  kinachofuatia ni utekelezaji wa kasi  ya ajabu ambapo  tayari wameanza kukutana na kuunda kamati  ndogo ndogo  zitakazokuwa na wataalam mbalimbali kwa ajili ya kuanza mara moja kwa utekelezaji  wa mradi huo.
 Profesa Muhongo alisema kuwa  serikali  za nchi zote mbili zimejipanga katika kuhakikisha kuwa  ujenzi huo unakwenda kwa kasi  kubwa, ikiwezekana ujenzi ukamilike mwishoni mwa mwaka   2019.
Aliongeza kuwa serikali ya  Uganda inatarajia kujenga kiwanda kwa ajili  ya kusafisha mafuta ghafi Hoima ambapo  wametoa hisa  40 zenye  thamani  ya Dola za Marekani  bilioni 4.7 kwa nchi  zilizomo ndani ya Jumuiya ya  Afrika Mashariki ambapo kila nchi itaweza kununua asilimia nane ya hisa hizo na kusisitiza kuwa  Tanzania ipo  tayari kununua hisa  nane kwa thamani ya  Dola za Marekani  milioni 150.4
Aliendelea kusema kuwa hisa zitanunuliwa na serikali pamoja na wawekezaji binafsi watakaoonesha nia ya kununua hisa ili waweze kunufaika na mradi huo.
Hata hivyo aliongeza kuwa nchi ya  Uganda pamoja na nchi nyingine zilizomo ndani ya  Jumuiya ya  Afrika Mashariki wameomba  kununua  gesi kutoka nchini  Tanzania  na kusema kuwa kwa kuanzia  serikali inatarajia  kujenga bomba la  gesi hadi nchini Uganda   ili waweze kunufaika na  gesi hiyo.
Alisema kuwa bomba la gesi litasambazwa katika mikoa ya kaskazini na mingineyo ili  uchumi wa nchi uweze kukua kwa kasi na  Tanzania kuwa nchi  yenye  kipato cha kati  ifikapo mwaka  2025 kama   Dira  ya Maendeleo  ya Taifa inavyofafanua.
“ Kila sehemu  yenye  gesi ya kutosha, lazima  tuhakikishe  tunaweka bomba la  gesi ambalo  ni  mkombozi wa uchumi wa nchi,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Wakati huo huo Waziri wa Nishati na Maendeleo  ya Madini Nchini   Uganda, Mhandisi  Irene  Muloni, aliishukuru serikali ya  Tanzania kwa kuwa tayari  kushirikiana na Uganda kwa ajili ya mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta.
Alisema kupitia  uzoefu  wa Tanzania  katika ujenzi wa mabomba ya  gesi na mafuta pamoja na wataalam  waliobobea anaamini kuwa mradi huu  utakwenda kwa kasi  kubwa na kukamilika kwa wakati.
Aliiomba  nchi ya   Tanzania pamoja na  wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na  makampuni ya mafuta, jamii itakayopitiwa na miundombinu  ya  bomba la mafuta kutoa ushirikiano ili mradi uweze kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Alisema kuwa   mkutano  wa pili unatarajiwa kufanyika  Hoima nchini  Uganda tarehe  27 Mei, mwaka huu na kuendelea kufanyika katika  maeneo mbalimbali  yatakayopitiwa na bomba la  mafuta.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni