WAZIRI MKUU: TATIZO LA AJIRA KWA VIJANA LAPUNGUA
Ametoa
 kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Aprili 22, 2016) wakati akiwasilisha 
mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na 
matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 
bungeni mjini Dodoma.
“Utafiti
 wa hali ya ajira nchini wa mwaka 2014 umeonesha kuwa kiwango cha 
ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi 
asilimia 10.3 mwaka 2014. Aidha, ukosefu wa ajira  kwa vijana umepungua 
kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014,” 
amesema. 
Waziri
 Mkuu amesema moja ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira ni 
vijana kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, 
Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi 
Nchini (2015/2016 – 2019/2020).
“Programu
 hiyo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi 
kutoka asilimia tatu ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha 
uchumi wa viwanda. Vilevile, kupunguza idadi ya watu wenye kiwango cha 
ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 54,” amesema.
Amewaagiza
 watendaji wakuu wa wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali, 
taasisi za umma, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha kuwa 
ukuzaji wa ajira  unakuwa ni agenda ya msingi ya kudumu katika 
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumzia
 kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu hususan watu 
wenye ualbino, Waziri Mkuu amesema Serikali inafanya jitihada kubwa 
kukomesha vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwakamata wote 
wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Ukatili
 huo umesababisha watu wenye ualbino kupoteza maisha na wengine kupata 
ulemavu wa kudumu. Hali hiyo haikubaliki na haivumiliki katika jamii ya 
Watanzania. Napenda kusisitiza watu wenye ulemavu wana haki ya 
kuthaminiwa utu wao na kulindwa dhidi ya ukatili na aina yoyote ya 
ubaguzi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaviboresha Vyuo vya Ufundi na Marekebisho (Vocational and Rehabilitation Training Centres)
 vya watu wenye ulemavu nchini ili kutoa ujuzi unaoendana na mahitaji 
yao katika soko la ajira ikiwa ni pamoja na kuandaa walimu wa elimu 
maalum na kutoa vifaa saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye ulemavu 
mashuleni.
Akitoa
 maelezo kuhusu juhudi za Serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi, Waziri
 Mkuu amesema Serikali imesaidia uanzishwaji wa taasisi mwavuli ya 
kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA ambayo imeanza kuonyesha matunda 
mazuri.
“Takwimu
 zilizotolewa mwezi Februari 2016 na taasisi hiyo zinaonesha kuwa kuna 
vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama milioni 2.2 na mtaji wa 
shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya 
wanachama wa VICOBA ni wanawake,” amesema.
Amezitaka
 Halmashauri zote nchini ziweke orodha sahihi ya vyama vya ushirika wa 
kuweka na kukopa vilivyosajiliwa kwa kila kijiji na kuchukua hatua za 
kuwezesha uanzishaji na usajili wa SACCOs zinazokidhi vigezo kulingana 
na shughuli za uzalishaji katika Halmashauri husika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
- L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, APRILI 22, 2016.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni