LUIS SUAREZ; HUYU NDIYE BABA MWENYE NYUMBA MPYA BARCELONA
Na Saleh Ally, aliyekuwa La Coruna
SAFARI
 ya kwenda Hispania kuliwakilisha Gazeti la Championi ilikuwa ni sehemu 
ya mafunzo makubwa katika kazi ya uandishi wa habari ambayo inataka 
mhusika ujifunze kwa wakubwa na wadogo, kila kukicha.
Nilisafiri
 pamoja na washindi wa “Kwea Pipa Kwenda Hispania na Azam Sports HD”. 
Ilikuwa ni safari zaidi ya shule ambayo katika mengi niliyojifunza, 
machache naona yanaanza kwenda kama nilivyoamini.
Kama
 nilivyoeleza juzi Jumamosi, kwamba mimi na wenzangu kutoka Tanzania 
pamoja na washindi wengine na waandishi kutoka Hong Kong na Sweden, 
tulipewa nafasi ya kukaa karibu kabisa wakati wachezaji wa Deportivo La 
Coruna wakiingia vyumbani. Lakini mwisho tukapewa nafasi kama hiyo kukaa
 kwenye Mix Zone.
Mix
 Zone ni sehemu maalum ya waandishi ambayo wanaweza kuwahoji wachezaji 
kabla au baada ya mechi. Pale mwandishi anachagua mchezaji anayemhitaji 
na kumuuliza swali analotaka.
Huu
 ni utaratibu wa kimataifa, kwa wale waliobahatika kuripoti mechi kubwa 
au michuano mikubwa kama Kombe la Dunia wanajua inavyokuwa.
Wakati
 wachezaji wanaingia vyumbani, kulikuwa na ulinzi mkali na watu wengi 
waliwekwa hatua takribani 50 upande wa pili wa barabara tofauti na sisi 
ambao tungeweza hata kupeana nao “tano”.
Wakati
 wachezaji wakishuka, hata kabla ya kufika pale tulipo, ilikuwa ni 
rahisi kujua aliyeshuka ni nyota kweli, maana watu walipiga kelele za 
juu zaidi na baada ya muda ungemuona mchezaji huyo anakuja upande wetu.
Walioongoza
 kushangiliwa walikuwa ni Iniesta, Lionel Messi halafu Neymar ambaye 
alibaki ndani ya basi peke yake kwa takriban dakika 5, ndiyo akashuka 
taratibu kabisa.
Luis
 Alberto Suarez Diaz, alishangiliwa kwa kiwango cha kati. Lakini 
ushukaji wake kidogo ulinishangaza, kwani alishuka haraka sana na 
kukimbia kama mtu ambaye alikuwa akihofia kukamatwa.
Uso
 wake alionekana kama mtu asiyetaka kuonekana au kuzungumza na mtu. 
Hakutabasamu kama wachezaji wengine, hakuonyesha urafiki na yeyote na 
aliwapita wachezaji wenzake waliowahi kuteremka kwenye basi na kuwahi 
kuingia vyumbani.
|  | 
| SUAREZ AKISAINI JEZI ALIYOPEWA NA SALEH ALLY | 
Kwa kuwa nilikuwa na baadhi ya waandishi wa Hispania, nilimuuliza mmoja kwamba hiyo ni tabia ya kawaida ya Suarez? Akanijibu:
“Kawaida
 hapa Hispania, wachezaji hawaruhusiwi kuzungumza kabla ya mechi, hofu 
ni kwamba unaweza kuwapotezea ‘focus’ (uwezo wa kulenga jambo wanalotaka
 kulifanya kwa ufanisi).
“Lakini Suarez yuko hivyo, ana hasira na anataka kufunga kila mechi ikiwezekana zaidi ya mabao mawili.
“Ukiwa
 unataka kumhoji, omba afunge. Kama itakuwa Barcelona imefungwa au 
hajafunga, usimsogelee kabisa, huwa hazungumzi na mara nyingi anakuwa wa
 kwanza kupanda kwenye basi.”
Hakuendelea
 kunipa maelezo kwa kuwa tulitakiwa kuondoka eneo hilo na kwenda kupiga 
picha na wachezaji wa Deportivo La Coruna waliokuwa benchi. Kwa upande 
wa wachezaji wa Barcelona, tulielezwa kwamba lilikuwa jambo gumu. Hivyo 
tukafanya hivyo.
Niliangalia
 mechi nikiwa makini na mambo mengi, lakini maelezo ya Suarez 
yalinifanya niwe makini sana kwake kwa muda wote wa mechi nikitaka kujua
 atafanya nini. Alikuwa ndiye mwiba kwa walinzi wa Deportivo La Coruna, 
akafunga mabao manne, Barcelona ikishinda kwa mabao 8-0.
Wakati
 wachezaji wanatoka tukiwa katika Mix Zone, nilisubiri atokee Suarez 
kuthibitisha yale maelezo ya mwandishi kutoka gazeti namba moja la 
michezo Hispania la Marca.
Alipotoka
 tu, nilikuwa mtu wa kwanza kumuita. Alitoa ushirikiano kwa kusaini jezi
 yangu na kujibu swali nililomuuliza. Hakika alionekana ni mwenye 
furaha, alipiga picha na watoto wawili, halafu akasogea na kupiga picha 
na mtu mmoja ambaye alimuomba, nikaamini hilo.
Lakini
 njaa ya Suarez ikaanza kubadili mawazo yangu, kwamba hata Barcelona 
wenyewe hawaoni kwa kuwa staa mkubwa au tegemeo zaidi kwao ni Suarez, 
tena kwa sasa anazidi hata umuhimu wa Neymar na Messi.
Utaona
 baada ya mechi hiyo, iliyofuatia niliishuhudia kwenye runinga, 
Barcelona wakiwa nyumbani Camp Nou, wakaigaragaza Sporting Gijon kwa 
mabao 6-0, Suarez akapiga mengine manne, safari hii akiwa na mawili ya 
penalti.
Suarez
 ana njaa kweli na ukiangalia, uwanjani utaona ana tofauti kubwa. 
Kikubwa kinachomsaidia hachezi kama supastaa. Anakimbiza mpira, anakaba,
 anabugudhi na anapambana muda wote, jambo ambalo ni nadra kumuona 
Messi, Neymar au hata Cristiano Ronaldo akifanya hivyo.
Ndani
 ya mechi mbili, kafunga mabao 8. Sasa ndiye anaongoza kwa ufungaji. 
Kabla ya mechi hizo mbili alikuwa anazidiwa na Ronaldo mabao matano. 
Sasa anamzidi mshambuliaji huyo nyota wa Real Madrid mabao matatu. Yeye 
kapiga 34 na Mreno huyo 31.
Awali
 ilionekana ni vita ya Messi na Ronaldo, sasa Suarez kaingia katikati na
 huenda akawa ndiye staa namba moja kuliko wote na huenda baada ya msimu
 huu akawa ndiye gumzo kuliko wote kama alivyoondoka England akiwa 
tegemeo na gumzo kuliko wote.
Awali
 ukizungumzia mabao na pasi, ungemtaja Messi. Lakini Suarez 
anadhihirisha anajua mno mpira na ndiye baba mpya mwenye nyumba wa 
Barcelona, yaani tegemeo, kwani baada ya kucheza dakika 2880 za La Liga,
 kafunga mabao 34 akiwa ametoa pasi 15 zilizozaa mabao. Kama hiyo 
haitoishi, katika dakika hizo amepiga mashuti 115 na 62 yamelenga lango.
Utaona takwimu zake ziko juu hata kuliko Ronaldo aliyecheza dakika 3059, akafunga mabao 31 na kutoa pasi 11 tu za mabao.
Messi
 naye amecheza dakika 2458, amefunga mabao 25 na pasi 13 za mabao. 
Neymar amecheza dakika 2787 na kufunga mabao 23 na pasi 10 zilizozaa 
mabao.
 Maana yake kama utazungumzia mabao na pasi za mabao au asisti, Suarez hadi sasa ni bora zaidi ya Ronaldo, Messi na Neymar.
Ndiyo
 anakwenda msimu wa pili wa La Liga, lakini anaonyesha si mtu wa 
kawaida. Suarez aliyetoka England kama mkosaji, Barcelona wakaonekana 
kama “wamebugi”, sasa ndiye shujaa mpya wa Blaugrana.
Huyu
 jamaa, anajua sana. Mbishi, si mwepesi kukubali na anachotaka ni 
kushinda zaidi ya mara moja, kufunga mabao zaidi ya yanayotegemewa na 
hii haina ubishi, atakuwa hashikiki na ndiye shujaa mpya wa Barcelona, 
hasa kama hataharibu na yale mambo yake.
TAKWIMU LA LIGA:
WATANO WANAOONGOZA LA LIGA KWA MABAO:
Luis Suárez
Barcelona
Amecheza dakika 2880  
Mabao 34
Asisti 15 
Cristiano Ronaldo
Real Madrid
Amecheza dakika 3059  
Mabao 31
Asisti 11 
Lionel Messi
Barcelona
Amecheza dakika 2458
Mabao 25
Asisti 13 
Neymar
Barcelona
Amecheza dakika 2787  
Mabao 23
Asisti 10 
Karim Benzema
Real Madrid
Amecheza dakika 1838 
Mabao 23
Asisti 6
SOURCE: CHAMPIONI
 




 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni