Maafisa usafirishaji waaswa kuwa wazalendo
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA 
Mhandisi Manase Ole Kujan akifungua kikao cha maafisa usafirishaji wa 
Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali kilichofanyika leo Jijini
 Dar es Salaam Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Matengenezo 
TEMESA Mhandisi Silivester Simfukwe na kulia ni Mhandisi Elirehema 
Mmari.
Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na
 Matengenezo TEMESA Mhandisi Silivester Simfukwe akizungumza na maafisa 
usafirishaji wa Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika 
kikao kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam kushoto ni Kaimu Mtendaji 
Mkuu wa TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan.
Baadhi ya cha maafisa 
usafirishaji wa Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali 
wakifatilia kikao kati yao na Wakala wa Umeme na Ufundi(TEMESA) 
kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
( Picha zote na Theresia Mwami-TEMESA)
……………………………………………………………………………………………………..
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Maafisa usafirishaji kutoka 
Wizara, Idara na Taasisi mbali mbali za Serikali wameaswa kuwa wazalendo
 kwa kufuata kanuni na utaratibu wa matengenezo na shughuli za kiufundi 
Serikalini.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar
 es Salaam na  Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan 
alipokuwa akifungua kikao cha maafisa usafirishaji kutoka Wizara, Idara 
na Taasisi mbali mbali za Serikali kujadili changamoto zinazowakabili na
 kuzipatia ufumbuzi kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zinazosimamia 
matengenezo ya magari na mitambo ya Serikali.
Kaimu Mtendaji Mkuu huyo amesema 
kwa hali ilivyo sasa imebainika kuwa Sheria na Kanuni za matengenezo ya 
magari na mitambo ya Serikali imekuwa ikikiukwa kwa kiasi kikubwa na 
hivyo kuilazimu mamlaka husika kutafuta njia mbadala ili kukabiliana na 
changamoto hiyo.
“Lengo letu ni kupata namna bora 
ya kutoa huduma ya matengenezo ya kiufundi ya vifaa vya Serikali pasipo 
kukiuka Sheria na Kanuni zilizowekwa hivyo basi tunaomba ushirikiano 
kutoka kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali  kuleta magari na vifaa 
kwetu ili tutekeleze wajibu wetu” alisema Mhandisi Manase.
Mhandisi Manase ameongeza kuwa 
pamoja na uchache wa Wizara , Idara na Taasisi  za Serikali 
zinazotekeleza Sheria na Kanuni za matengenezo ya magari ya Serikali kwa
 kuleta magari TEMESA ila kumekuwa na changamoto katika ulipaji wa 
gharama za matengenezo hali inayosababisha Wakala usiweze kufanya kazi 
kwa ufanisi.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa 
Uzalishaji na Matengenezo kutoka TEMESA Mhandisi Sylivester Simfukwe 
amesema Wizara , Idara na Taasisi  za Serikali zinatakiwa kuzingatia 
Sheria na Kanuni zilizopo kwa kupeleka na kulipa gharama za matengenezo 
ya magari na vifaa vya Serikali kwani Wakala huu ndio mshauri mkuu wa 
Serikali katika masuala ya kiufundi na kusisitiza kuwa kwa kufanya hivyo
 itasaidia kuongezeka kwa mapato ya Serikali.
Naye Meneja Usafirishaji kutoka 
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Jonathan Mhagama ameiomba Serikali 
kuiongezea uwezo TEMESA kwa kuwa na karakana za kisasa ili kuendana na 
mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambapo kwa sasa uwezo walionao 
wakala huo ni mdogo ukilinganisha na magari yaliyopo Serikalini.
Mkutano kati ya Wakala wa Ufundi 
na Umeme (TEMESA) na maafisa usafirishaji wa Wizara,Idara na Taasisi 
mbalimbali za serikali umekuja mara baada ya kauli kutoka kwa  Waziri wa
 Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof  Makame Mbarawa ya kuyataka 
magari yote ya Serikali kutekeleza Sheria na Kanuni za matengenzo ya 
vifaa vya Serikali.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni