JESHI LA POLISI LAKEMEA JAMII KUHUSU MATUKIO YA UBAKAJI WA WATOTO NCHINI
Katika siku za hivi karibuni, 
Matukio ya ubakaji hasa kwa watoto wadogo yamekuwa yakiongezeka kwa 
kiwango kikubwa, ongezeko hili limebainika kutokana na ufuatiliaji 
tulioufanya kupitia matukio yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi 
ambapo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2016 kumeripotiwa 
matukio 1765 ukilinganisha na matukio 1585 katika kipindi kama hicho 
mwaka 2015 ikiwa ni ongezeko la matukio 180.
Katika matukio ya Januari hadi 
machi 2016, jumla ya watuhumiwa 823 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani
 ingawa bado kumekuwa na tabia ya wazazi na walezi kuficha watuhumiwa wa
 ubakaji na  kumaliza kesi hizo kirafiki au kifamilia jambo ambalo ni 
kinyume cha sheria bila kuzingatia madhara aliyoyapata mtoto.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la 
Polisi nchini linakemea vikali wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo
 viovu vya ubakaji na wazazi ama walezi wanaofumbia macho vitendo hivyo 
na kuingia makubalino na watuhumiwa kwa kupeana fedha kama fidia ili 
wamalize kesi kiundugu au kifamilia.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa 
 Wazazi, walezi, Viongozi wa dini, Asasi za kiraia, walimu na Wananchi 
kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano katika kushughulikia vitendo 
hivyo ikiwemo kuwafichua wazazi au walezi wanaofanya makubaliano ya 
kumaliza kesi za ubakaji kirafiki au kifamilia ili kukomesha vitendo 
hivyo.
 Imetolewa na:
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.         
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni