Sio kila homa ni malaria, nenda ukapime
……………………………………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma.
La mgambo likialia kuna jambo,
safari ya kujenga taifa bora na imara katika sekta ya afya ni jukumu la
watu wa taifa husika kuanzaia na mtu mmoja mmoja.
Katika kuhakikisha watu wanajenga
afya njema itakayowawezesha kuwa uchumi imara, ni jukumu la taifa hilo
na kila mtu kutumia nguvu zake katika kujenga uchumi imara wenye
kusimamiwa na afya bora ambayo ni ni msingi maendeleo.
Katika hali ya kawaida, mtu
anayefanya kazi za mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisaiasa ni lazima
awe na afya bora na njema, kwa maneno mengine ni lazima awe mzima.
Siku ya Malaria Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Aprili 25, ni moja ya siku adhimu inayopaswa kuzingatiwa na kutiliwa maanani.
Maadhimisho hayo yalianza
kuadhimishwa tangu mwaka 2001 inatoa nafasi kwa Wataalamu wa Afya na
Wananchi kwa jumla kuchambua kwa kina utekelezaji wa mapambano dhidi ya
Ugonjwa wa Malaria kwa kila mwaka.
Siku hiyo inatoa nafasi ya
kuangalia tulikotoka, tulipo na tunakokwenda katika suala zima la
kufanikisha mapambano dhidi ya malaria.
Jitihada hizo hufanywa
ulimwenguni kote kutokana na kutambua kuwa Malaria haina mipaka hivyo
mikakati ya kupambana na ugonjwa huo inahitaji ushiriki wa Wadau wote si
tu katika Bara la Afrika peke yake, bali Ulimwenguni kote.
Kila mpenda maendeleo anatambua
namna Ugonjwa wa Malaria unavyoendelea kuwa tishio kwa maisha ya
Watanzania kwa miaka mingi sasa.
Taarifa za Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto zinaonyesha kuwa, Ugonjwa wa
Malaria unaongoza kuwa na wagonjwa wengi wa Nje (OPD) katika hospitali
nyingi hapa nchini pamoja na wagonjwa wa malaria wanaolazwa katika
Hospitali katika hospitali mbalimbali. Pia ugonjwa wa malaria unaongoza
kwa vifo vyote vinavyotokea katika Vituo vya Tiba.
Mwanga bora wa kutatua tatizo
hili nchini umeanza kuonekana ambao ni dalili njema ya kulitoa taifa
kwenye janga na hatari za ugonjwa wa malaria hatua ambayo itasaidia
kupungua kwa kiasi kikubwa ugonjwa huo nchini.
Kutokana na Ripoti ya Utafiti wa
viashiria vya VVU/UKIMWI na malaria inaonekana kupungua kwa asilimia 50
kutoka asilimia 18 kwa mwaka 2007/2008 hadi asilimia 10 mwaka 2011/2012.
Pamoja na kupungua kwa maambukizi
ya malaria, takwimu zinaonesha kuwa ugonjwa huo bado ni tatizo kubwa
katika vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mjini ambapo maambukizi ya
maeneo ya vijijini ni asilimia 10.7 na mjini ni aslimia 3.4
Kupungua kwa maambukizi ya
ugonjwa wa malaria nchini, Watanzania wana kila sababu ya kujipongeza na
kumshukuru kila mdau aliyeyechangia kwa namna moja au nyingine katika
jitihada za kutokomeza ugonjwa huo.
Juhudi hizo zinatoa msukumo kwa
Watanzania kutambua kuwa bado kuna kazi ya kufanya ambapo lengo la taifa
ni kuhakikisha maambukizi ya ugonjwa wa malaria yanapungua hadi
asilimia 5 mwaka 2016 na asilimia 1 ifikapo mwaka 2020.
Hatua hiyo inawezekana kufikiwa
na taifa ikiwa kila mtu anawajibika kwa nafasi yake kushiriki katika
kupambana na vita dhidi ya malaria.
Ukiona vya elea ujue vimeundwa,
hatua ambazo zimesababisha kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa huo
zinatokana na juhudi mbalimbali zinazosimamiwa vema na viongozi wenye
dhamira ya dhati ya kupambana na adui wa taifa ambaye maradhi.
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu
ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete wakati wa uongozi wake na hata baadha ya
muda wake wa uongozi amekuwa msari wa mbele katika kupambana na adui wa
taifa ambaye miongoni wao ni ugonjwa malaria.
Jitihada zake za kupambana na
malaria ndani na nje ya nchi zimeonesha tija na zimezaa matunda na
kupelekea kutunukiwa tuzo iliyotukuka ya “White House Summit Award”
mapema Aprili mwa huu ndio maana waswahili husema “Chanda chema huvikwa
pete”.
Je? Mimi na wewe, tumejifunza
nini katika kupambana na ugonjwa wa malaria? Tambua zama zimebadilika,
si kila homa ni malaria, chukua hatua nenda kituo cha afya kilicho
karibu nawe uweze kupima afya yako badala ya kuanza kutumia dawa bila
kufanya vipimo.
Vipimo ndio iwe mwalimu na
mwongozo wa kujua mtu anasumbuliwa na ugongwa gani ndipo aweze kutumia
dawa sahihi za kupambana na adui anayemsumbua.
Hadi sasa nchini, Serikali
inapaswa kupongezwa kwa kuanzisha utaratibu kabambe wa kupambana na
ugonjwa wa malaria ambapo watu watakaoenda kupima ugonjwa huo katika
zahanati, vituo vya afya na hospitali mbalimbali za umma wanakiwa kupima
bure na mara baada ya wakigundulika kuwa wana ugonjwa wa malaria
wanapswa kupewa dawa za kutibu ya ugonjwa huo bure.
Hatua hiyo njema ni na ya
kupongezwa na kila mpenda na mthamini uhai, Waziri mwenye dhamana ya
afya nchini chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee
na Watoto Ummy Mwalimu alipokuwa akitoa tamko la maadhimisho ya Siku ya
Malaria Duniani mjini Dododma amesisitiza kuwa huduma ya vipimo na
matibabu ya ugonjwa wa malaria itakuwa intolewa bure isipokuwa malipo ya
kumuona daktari ndio yanapaswa kulipwa.
Kwa hatua hiyo itaifikisha
Tanzania kujiridhisha na usemi wa “Tanzania bila malaria inawezekana”
maana wananchi sasa wamepunguziwa mzigo mkubwa uliokuwa ukiwasumbua kwa
muda mrefu na kuwafanya watu wengi kupoteza maisha kabla hata ya
kufikishwa vituo vya afya kutokana na kukosa fedha za kupata matibabu.
Hatua hiyo ya taifa ya kupambana
na malaria ni njia na mwanga bora kwa kuwa na watu wenye afya njema
ambao watakuwa mstari wa mbele katika kujenga na kuhakikisha nchi
inafikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Akitoa tamko katika kilele cha
maadhimisho ya siku ya malaria duniani mjini Dodoma, Waziri Ummy alisema
kuwa Watanzania ni lazima kutambua maadhimisho hayo ya Malaria nchini
yapaswa kuwa chachu ya wananchi kupima na kuthibitisha kama wana vimelea
vya malaria kabla ya kuanza kutumia dawa.
Waziri Ummy aliongeza kuwa pale
mtu anapogundulika kuwa ana malaria, anapaswa kuhakikisha anatumia dawa
na kumaliza kozi nzima kulingana na maelekezo ya daktari.
Katika kuhakikisha taifa
linapambana na ugojwa wa malaria, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Mbu
Waenezo Malaria Charles Damas anabainisha umuhimu wa jamii kushiriki
kikamilifu katika kuharibu mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji,
kusafisha mifereji na kuweka mazingira safi ili kuondoa maji yanayotuama
hatua ambayo itachangia kupunguza maambukizi ya malaria.
Ni dhahiri Tanzania sio kisiwa,
imeendele kuwa na mahusiano mazuri na mataifa rafiki pamoja na wadau
wengine wa maendeleo katika kupambana na ugonjwa wa malaria nchini.
Wadau ambao wapo mtari wa mbele
katika mapambano ya malaria ni pamoja na Mfuko wa Dunia wa kushughulikia
ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, Mfuko wa Rais wa Marekani wa
Kushughulikia Malaria (PMI), Shirika la Misaada la Uingereza (DFID),
Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), Shirika la Afya Duniani (WHO),
Shirika la UNITAID,Taasisi zisizo za Kiserikali, Sekta Binafsi kupitia
Mpango wa malaria Safe na Taasisi za Utafiti za NIMRI na Ifakara.
Katika kupambana na adui maradhi,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, alitoa mwongozo wa Serikali yake kupitia hotuba yake ya
kufungua rasmi Bunge jipya la 11 la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,mjini Dodoma Novemba 20, 2015 ambapo alibainisha dhamira ya
dhati katika masuala ya afya.
Rais Dkt. Magufuli anasema
“Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini
linakwenda sambamba na kuwa na wananchi wenye afya bora. Kwa kutambua
ukweli huu na mahitaji ya huduma bora za wananchi wetu Serikali ya Awamu
ya Tano itahakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya”.
Dhamira hiyo ya Serikali ni
kuimarisha huduma za afya sehemu ambapo huduma hizo zipo na kuanzisha
pale ambapo hazipo ikiwa na lengo la kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na
Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya, kila wilaya inakuwa na
Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali ya Rufaa.
Ni dhahiri nia ya Serikali ya
kuboresha huduma za afya nchini itasaidia kuongeza utaalamu katika sekta
ya afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi,
kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati
zilizopo nchini.
Lengo hilo la Serikali kuchukua
hatua hizo itasaidia kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa nchini
na hivyo kutolazimika kupeleka wagonjwa kutibiwa nchi za nje.
Ili kufanikisha hayo, Rais
alisema kuwa Serikali yake itaendelea kuongeza bajeti ya dawa na
kuboresha mfumo wa upatikanaji wa dawa hizo ili kuhakikisha zinapatikana
katika hospitali, vituo vya afya na zahanati na kuhamasisha wananchi
wajiunge na Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya
mahali popote nchini na wakati wowote.
Alipokuwa akitoa tamko hilo siku
ya maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani, Waziri Ummy aliongoza kupimwa
kujua kama ana vimelea vya malaria ambapo waaandishi wa habari ambao
walihudhuria wakati tamko hilo kutolea mjini Dododma waliungana naye
kujua hali ya afya zao.
Ili kutokomeza ugonjwa wa malaria
nchini, kila mtu anapaswa kuzingatia kupima ili kujua uwepo wa vimelea
vya malaria kabla ya kutumia dawa, kumaliza kozi ya dawa kulingana na
maelekezo ya daktari na mtoa huduma, kutumia vyandarua vyenye viaatilifu
kila siku wakati wa kulala pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira
kuzuia mazalia ya mbu katika maeneo yanayozunguka nyumba zao.
Jukumu la kupambana na malaria
sio la mtu moja, halmashauri zao zinapaswa kuboresha takwimu zao ili
kujua ukubwa wa tatizo la malaria katika halmashauri zao na kuweka
bajeti kwenye mipango yao ya halmashauri (CCHP) kwa ajili ya udhibiti wa
mbu.
Majukumu mengine ya halmashauri
ni kuhakikisha miongozo ya uchunguzi na tiba ya malaria inazingatiwa
katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya umma na vya sekta
binafsi pamoja na kufanya ufuatiliaji katika vituo vya kutolea huduma
vya umma na vya sekta binafsi ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Juhudi hizo kupambana na ugonjwa
wa malaria sio za kuachiwa Serikali tu, kila mtu awajibike na atambue
kuwa zama zimebadilika, “Sio kila homa ni malaria, nenda ukapime” na
“lala kwenye chandarua kila siku” kujikinga na malaria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni