Vyeti vya kuzaliwa havitolewi kwa misingi ya kisiasa
Na Masanja Mabula –Pemba 
SERIKALI ya Wilaya ya Micheweni 
Mkoa wa Kaskazini Pemba imekanusha  taarifa zilizotolewa na wananchi ya 
kwamba vyeti vya kuzaliwa katika Wilaya hiyo hutolewa kwa misingi ya 
kisiasa .
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Abeid
 Juma Ali aliyaeleza hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara  ambao 
baadhi yao waliodai kwamba kuna ubaguzi juu ya utoaji wa vyeti vya 
kuzaliwa
Alisema kuwa  kwa kipindi cha 
miezi mitano tangu ashike wadhifa huo  tatizo la upatikanaji wa vyeti 
vya kuzaliwa  kwa watoto  katika wilaya hiyo limeanza kupatiwa ufumbuzi .
Alifahamisha kuwa kwa 
kushirikiana na watendaji wa Ofisi ya Vizazi na Vifo   , ameanza 
kulipunguza tatizo hilo , ambapo watoto wengi wameweza kupatiwa vyeti 
kwa wakati na bila usumbufu .
“Mtoto hana chama iweje basi 
 nimbague kwa misingi ya siasa , natambua wajibu na majukumu yangu kwani
 mimi ni mtumishi wa umma na ninawatumikia wananchi wote pasi na ubaguzi
 ”alifahamisha .
Awali mfanyabiashara Ali Salimu 
Ali (Baraka) wa Wingwi alisema kwamba kunahitaji kuangaliwa upya Ofisi 
inayohusika na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwani imekuwa ikichelewesha 
kupatikana kwa vyeti kwa baadhi ya watoto .
Alieleza kwamba wapo watoto 
wamefikia umri wa kwenda skuli lakini hawana vyeti  vya kuzaliwa , licha
 ya kwamba kumbukumbu zao zipo katika Ofisi ya vizazi na vifo lakini 
zimeshindwa kufanyiwa kazi .
“Vyeti vya kuzaliwa bado ni 
tatizo , kwani kuna baadhi ya watoto wamefikia umri wa kuanza skuli , 
lakini hawana vyeti , tunaomba hii Ofisi  inayohusika na utoaji wa vyeti
 uiangalie upya  nahisi kama kuna  ubaguzi fulani hivi  ”alisema  .
Kikao hicho  pia kilihudhuriwa na
 Madiwani wa Wilaya hiyo ambapo Mkuu wa Wilaya alitumia fursa hiyo 
kuwataka wafanyabiashara kuwapa ushirikiano wakati wanapokusanya mapato 
 yatokanayo na biashara zao .
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni