Wamuomba Rais Dkt.John Pombe Magufuli kuteketeza ghala la meno ya tembo liliopo nchini
Taasisi isiyo ya kiserikali ya 
Okoa Tembo Tanzania imemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 
Dkt.John Pombe Magufuli kuteketeza ghala la meno ya tembo liliopo nchini
 kufuatia Tanzania kusaini mpango wa kuwalinda Tembo mwaka 2014 unaozuia
 uuzaji wa meno ya Tembo kwa muda wa miaka 10.
Ombi hilo limetolewa leo jijini 
Dar s Salaam na Mwenyekiti wa Kampeni ya Okoa Tembo Tanzania Bw.Shubert 
 Mwarabu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Barua ya 
Wazi waliyomwandikia Mheshimiwa Rais.
Amesema Tanzania inafungwa na 
mkataba wa kimataifa wa biashara juu ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka
 (Convetion on International Trade in Endangered Species-CITES) ambao 
unabainisha kuwa Tanzania kwa sasa haiwezi kuuza ghala lake la meno ya 
Tembo.
Amesema uhifadhi wa meno hayo 
unaigharimu serikali fedha nyingi  na kufafanua kuwa kwa sasa Tanzania 
ina hifadhi kubwa ya meno ya Tembo yaliyokamamwa kutokana na ujangili.
“Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa
 kasi yake ya utendaji tangu kuchaguliwa kwake,tunamuomba atekeleze 
lengo la tatu la kampeni yetu ya Okoa Tembo wa Tanzania kwa kuliteketeza
 hadharani ghala la meno ya tembo,tunaona hakuna haja ya kuendelea kuwa 
na ghala hili” amesema Bw.Mwarabu.
Amesisitiza kuwa ombi lao kwa 
Rais kutaka ghala la meno ya Tembo liteketezwe kutasidia kutuma ujumbe 
mzito kwa majangili na wafanyabiashara kuwa meno ya Tembo hayana thamani
 ya pesa kiasi cha serikali kuona wepesi kuteketeza hazina hiyo.
“ Tunataka ieleweke kwamba 
kuharibu ghala la meno ya Tembo kunatuma ujumbe mzito kwa majangili na 
wafanyabiashara kuwa meno ya Tembo hayana thamani ya pesa na kuwa 
ujangili ni kosa la jinai lisilokubalika” Amesisitiza.
Amesema ipo haya ya Tanzania 
kuunga mkono mpango wao wa kuteketeza ghala la meno ya Tembo kama 
inavyotarajiwa katika nchi ya Kenya ambayo inatarajia kuteketeza ghala 
lake la meno ya Tembo hadharani Aprili 30 mwaka  huu.
Amezitaja nchi ambazo zina mpango wa kuchukua hatua kama ya Kenya kuwa ni Ethiopia,Chad,Gabon, Mozambique na Congo.
Naye mmoja wa wajumbe wa Kampeni 
ya Okoa Tembo wa Tanzania Bw.Arafat Mtui akizungumza katika mkutano huo 
amesisitiza kuwa kuendelea kuwepo kwa ghala hilo nchini Tanzania 
kunawapa moyo wafanyabiashara haramu wa meno hayo kuona kuwa ipo siku 
biashara hiyo itaendelea tena.
Amesema Kampeni yao ya Okoa Tembo
 wa Tanzania  inaendelea kusisitiza kuwa  kuwa hatma ya Tembo wa 
Tanzania iko mikononi mwa watanzania,  hivyo ni vema Serikali 
ikashirikiana na wadau mbalimbali  kuchukua hatua madhubuti kuokoa 
viumbe hao walio hatarini kutoweka kwa ajili ya kizazi cha sasa na 
vizazi vijavyo.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni