SERIKALI YAUNDA KAMATI YA KUANZISHA TUME YA TEHAMA
Katika kuhakikisha kuwa Tume ya 
TEHAMA inaanza kazi mara moja, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
 na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano, Prof. Faustin 
Kamuzora, amewakabidhi wajumbe wa Kamati hiyo Amri ya Rais wa Jamhuri ya
 Muungano wa Tanzania Na.532 iliyotolewa kupitia gazeti la Serikali Na. 
47 la tarehe 20 Novemba, mwaka 2015 iliyoanzisha Tume na Hadidu za Rejea
 zinazoainisha majukumu yao. Majukumu hayo ni pamoja na kusimamia 
uanzishwaji wa Tume, kuandaa sheria ya kuanzisha Tume, na kutengeneza 
Mpango Mkakati wa Tume. Prof. Kamuzora amewataka wajumbe wa Tume hiyo 
 kuepuka kuweka mitazamo au maslahi binafsi ya wao wenyewe au ya taasisi
 zao katika kipindi cha kuanzisha Tume, bali waishauri Serikali namna 
nzuri ya kuhakikisha kuwa Tume hiyo inaanza kazi ya kusimamia na 
kuratibu masuala ya TEHAMA nchini. Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na
 Mwenyekiti wao na Katibu wa Kamati ya Kuanzisha Tume ya TEHAMA nchini 
ni kama ifuatavyo:
- James Kilaba (Mwenyekiti), Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,
- Samson Mwela (Katibu), Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
- Idris Rai (Mjumbe), Makamu Mkuu wa Chuo, SUZA,
- Joan Mbuya (Mjumbe), Mkurugenzi wa Sera na Mipango-Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali,
- George Mulamula (Mjumbe), Mkurugenzi Mtendaji-DTBi,
- Juma Rajabu, (Mjumbe), Mkurugenzi Mtendaji-Maxcom Africa,
- Maharage Chande, (Mjumbe), Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Ofisi ya Rais-President’s Delivery Bureau, na
- Nicolaus Mhonyiwa (Mjumbe), Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA-Ofisi ya Msajili wa HAZINA.
Aidha, Tume ya TEHAMA inatarajiwa 
kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na yafuatayo: Kushiriki 
katika kushauri juu ya uwekezaji wa TEHAMA nchini kwa ubia na sekta 
binafsi; kuwatambua, kujenga uwezo na kuwaendeleza wataalam wa TEHAMA; 
kushauri na kushiriki pamoja na wadau katika tafiti za TEHAMA, uwekaji 
viwango na ubunifu katika sekta ya TEHAMA; na kushiriki katika kusimamia
 miundombinu na programu za kitaifa za TEHAMA.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Eng. 
Maria Sasabo, alisisitiza kuwa Kamati ina kazi kubwa ya kuona namna bora
 zaidi ya kuhakikisha kuwa Tume itatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa
 ni pamoja na masuala ya uwekezaji; na kusimamia vema  viwango vya 
wataalamu wa Sekta. Naye Mwenyekiti, Inj. James Kilaba, kwa niaba ya 
Kamati alishukuru kwa kuaminiwa na Serikali na pia aliahidi kuwa 
watatekeleza majukumu yao kikamilifu. Pia alimalizia kwa kusema, 
“hatutawaangusha”.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni