HAKUNA MUDA WA KULALA, WAZIRI MKUU AIAMBIA DART
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaambia watendaji na wadau wa mradi Mabasi Yaendayo Haraka wa jijini
Dar es Salaam (BRT) kuwa hawana muda wa kulala wa kupumzika na akawataka
wakamilisha haraka vipengele vichache vilivyobakia ili mradi huo uweze
kuanza kazi mapema iwezekanavyo.
Ametoa agizo hilo jana usiku
(Ijumaa, Aprili 15, 2016) wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi,
watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha
ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam.
“Watu wa DART, UDA-RT hakuna muda
wa kulala tena. Nanyi wa eGA, MAXCOM, POLISI NA SUMATRA inabidi mfanye
kazi kama timu moja na wenzenu ili maeneo yaliyobakia yaweze kukamilika
katika muda mfupi na kikubwa ni kuhakikisha mnatoa elimu ya kutosha,”
alisisitiza.
Akielezea utekelezaji wa agizo la
Waziri Mkuu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka
(DART), Bw. Ronald Rwakatare amesema miundombinu ya mradi huo
imekamilika na utoaji huduma unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani hivi
sasa wanamalizia ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji nauli na uendeshaji wa
mabasi hayo.
Pia aliwatka wananchi kutunza
miundombinu ya mradi huo na kuwa makini na matumizi ya barabara wakati
mradi huo ukiwa kwenye majaribio na hatimaye kuanza kazi rasmi.
Alisema watakuwa na karakana
itakayotumika kwa ajili ya hayo mabasi ambayo itakuwepo eneo la Jangwani
na kwamba ofisi za mradi pia zitakuwa eneo hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
UDA Rapid Transit (UDA-RT), Bw. Robert Kisena amesema mpango wa kuanza
kwa mradi huo umekamilika na tayari mabasi yote yamelipiwa kodi pamoja
na bima. UDA-RT ni kampuni ya muunganiko wa UDA na wamiliki wa daladala
ya kutoa huduma ya usafiri katika miundombinu ya mabasi yaendayo haraka.
Bw. Kisena amesema kesho wataanza
majaribio ya mradi huo kwa kutumia mabasi 10 na watakuwa wanaongeza
mabasi 10 kila siku hadi yafikie 50 hivyo amewataka wananchi kuondoa
shaka juu ya mradi huo.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Maxcom
Africa, Bw. Juma Rajab amesema mabasi hayo yatakuwa yanatumia kadi za
kielektroniki zitakazokuwa zinalipiwa kwa kutumia mitandao mbalimbali ya
simu za mkononi.
Bw. Rajab amesema Tanzania
inakuwa nchi ya kwanza kuanza kutumia mfumo huo katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kwamba fedha za mteja zitakuwa salama na hata kama
atakapopoteza kadi yake.
“Mtu akinunua kadi yake anapaswa
atunze namba ya usajili iliyoko kwenye kadi hiyo kwani itatumika
kurudishia fedha zake kupitia namba yake ya simu ya mkononi,” alisema.
Amesema Maxcom Africa ndio
wakusanyaji wa nauli kwa kushirikiana na UDA-RT ambapo watatumia
mawakala wa MaxMalipo hivyo kila mwananchi atapata fursa ya kununua kadi
yake kwa urahisi.
Alisema taarifa za kila mtumiaji
zitaunganishwa na simu yake ya mkononi ambapo mhusika ataweza kujua kwa
urahisi salio la fedha lililomo kwenye kadi yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni