Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na Makamanda wa Polisi, Wanasheria wa Serikali, Wafawidhi wa Mikoa na
Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi kabla ya kufungua rasmi Kikao kazi
cha Makamanda hao wa Polisi katika Ukumbi wa Dodoma Convention Center
…………………………………………………………………………………………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi nchini na
Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujirekebisha kwa kutekeleza wajibu wao
huku wakitanguliza maslahi ya taifa.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo
leo tarehe 29 Aprili, 2016 wakati akifungua kikao cha kazi cha
Makamanda wa polisi wa mikoa, Mawakili wafawidhi wa serikali wa Mikoa
na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi, kinachofanyika kwa siku mbili
katika ukumbi wa Mikutano wa Dodoma uliopo katika eneo la Tambukareli
Mjini Dodoma.
Awali kabla ya kutoa hotuba yake
Rais Magufuli aliwapa nafasi Makamanda na Mawakili Wafawidhi hao kutoa
maoni yao juu ya changamoto zinazowakabili katika kutekeleza wajibu wa
kufanya upepelezi na kuendesha mashitaka, hususani kujua sababu za
kuchelewesha kesi za makosa ya jinai, ambapo wamedai ufinyu wa bajeti
ndio sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa kesi za hizo.
Kufuatia kutajwa kwa changamoto
hiyo Rais Magufuli ameahidi kuhakikisha anawatafutia fedha kwa ajili ya
kukabiliana nazo, lakini ametaka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri
kwa kuwa taarifa zinaonesha Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa na
matumizi mabaya ya fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo
yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.
Ametolea mfano wa taarifa za
matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununulia vifaa na
sare za askari, ama mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya
Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya
utendaji kazi kwa jeshi hilo.
“Oysterbay pale ni eneo
ambalo ni very prime, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba
mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo
hayo yanafaa. Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati,
mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za
ghorofa 20 pale, mkaweka investment na Polisi wenu wakakaa pale.
Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia
vibaya nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na muelewe ukweli direction ninayoitaka mimi” Amesema Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli ameitaka
Ofisi ya mwendesha Mashitaka wa Serikali kujipanga kufanya kazi kwa
ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya serikali
kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria
mahiri.
“Niwaombe mawakili na polisi
wanaohusika na upelelezi mtangulize maslai ya nchi mbele, kwa sababu
kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache, nasema
wachache, panapokuwa na kesi inayohusiana na pesa pesa, wana misemo yao
wanasema dili limepatikana, na saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani
wana-collude Mawakili wa serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu, na
wanapo-collude siku zote serikali inashindwa. Unapoona hali hiyo ya kila
siku serikali inashindwa, halafu siku hiyo unataka serikali ikuwezeshe,
kwa vyovyote serikali inapata kigugumizi” amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi
la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake,
ikiwemo maafisa wa Polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na
kuazimisha silaha kwa wahalifu wa ujambazi.
Hata hivyo Rais Magufuli
amelipongeza Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kwa
kazi kubwa wanayoifanya na ametaka apelekewe mpango wa mahitaji yao ili
atafute namna ya kuimarisha vyombo hivyo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
29 Aprili, 2016