ZIARA YA WAZIRI NAPE NA RIPOTI KAMILI YA TFF
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi.
………………………………………………………………………..
Ripoti ya mwenendo wa mpira wa
miguu Tanzania na mipango yake inayofanywa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), imemfurahisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Nape Nnauye hivyo moja kwa moja akaupongeza uongozi wa Rais
Jamal Malinzi akisema unafanya kazi kubwa.
Kutokana na ripoti hiyo, Nape
ambaye ni Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, aliridhia wadau wa mpira wa
miguu kusapoti timu za taifa hususani Serengeti Boys – timu ya taifa ya
vijana wenye umri chini ya miaka 17 ambayo kwa sasa imepiga kambi
Shelisheli kujiandaa kuivaa Congo-Brazzaville Jumapili ijayo.
Serengeti Boys inawania kucheza
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri katika fainali
zitakazofanyika Antananarivo, Madagascar sawa na timu ya taifa ya soka
la ufukweni ambayo inatarajiwa kusafiri kwenda Abidjan, Ivory Coast
kucheza mchezo wa pili wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa mchezo huo.
Timu nyingine ya taifa ni ile ya
wanawake ya Tanzania Bara maaarufu kwa jina la ‘Kilimanjaro Queens’
ambayo kwa sasa iko Uganda kuwania taji la Chalenji ikishirikisha timu
za taifa za Afrika Mashariki katika michuano ya inayotarajiwa kufanyika
jijini Jinja kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, mwaka huu.
Nape amefurahishwa na mipango ya
TFF baada ya kupeleka timu zote kushiriki michuano mbalimbali kwa
vipindi mbalimbali na kwamba Serikali itasapoti lakini hapo baadaye
baada ya kufuata taratibu mbalimbali baada ya Rais Malinzi kumfafanualia
kuwa gharama za kuendesha mpira kwa mwaka zinafika shilingi bilioni 15,
na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) huchangia asilimia
tatu (3) tu ya bajeti nzima kwa mwaka.
“Kwa kuanzia msimu huu tu, FIFA
imeongeza na sasa itafika asilimia 6 kwa mwaka,” alisema Malinzi jambo
ambalo lilimshangaza Nape ambaye leo Septemba 10, 2016 alifanya ziara ya
kutembelea TFF kujionea hali halisi na kushangazwa na taarifa za vyanzo
mbalimbali zinazotuhumu shirikisho.
Nape alisema: “Serikali inasapoti maendeleo, lakini lazima yafuate taratibu, kanuni na sheria za soka.”
Katika eneo la kufuata taratibu,
kanuni na sheria za soka hatua nyingine, Nape alitaka Malinzi na kamati
zake kuwa wakali kwa kuwa huwa hawachui hatua mapema, inatokea wadau
kutaka kuipanda kichwani TFF.
“Naagiza mchukue hatua mapema
kukamua majipu kabla hajajaiva. Sasa ninyi mnasubiri kwa muda mrefu
kabla ya kuchukua hatua, ndiyo maana wanawasumbua. Washughulikieni
mapema, mkiwabana mapema watakaa kimya, kanuni mnazo, sheria mnazo,
wabaneni,” alisema Nape.
Katika hatua nyingine, Nape
alisema kwamba kuna mchakato unaendelea kwa sasa ndani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kwamba wanarejesha mamlaka ya kumiliki
baadhi ya viwanja vya soka Makao Makuu ya chama badala mikoa ambako
wamegundua kuwa kuna matatizo makubwa katika menejimenti.
NA HIZI NDIZO SALAMU ZA RAIS WA
TFF, JAMAL EMIL MALINZI KWA MHESHIMIWA NAPE NNAUYE WAZIRI WA HABARI,
UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO UWANJA WA KARUME TAREHE 10 SEPTEMBA 2016
Mheshimiwa Waziri,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutukutanisha hapa leo.
Ni jambo la heshima na furaha
kubwa sana kwetu sisi wanafamilia ya mpira wa miguu Tanzania kwa
kutembelewa na wewe Mheshimiwa Waziri na ujumbe wako. Mheshimiwa ahsante
sana kwa tukio hili adhimu na karibu sana kwenye makazi ya mpira “home
of football”.
Mheshimiwa Waziri tunashukuru
kwamba umeweza kutembelea eneo letu na kujionea wapi huwa tunafanyia
shughuli zetu mbali mbali za kuendeleza michezo.
Shirikisho la mpira wa miguu
Tanzania TFF limesajiliwa chini ya sheria ya baraza ya mwaka 1967 na
marekebisho yake ya mwaka 1971 na madhumuni yake makuu ni kuendeleza
na kusimamia mpira wa miguu Tanzania. Katika kutekeleza azma hii
shughuli zetu tumezigawanya katika maeneo makuu matano:
- Utawala
Shughuli za kila siku za
uendeshaji wa mpira wetu zinasimamiwa na Sekretariet ya TFF inayoongozwa
na Katibu Mkuu Ndugu Mwesigwa Selestine. Chini yake ana vitengo vikuu
vitano: Ufundi ambacho kinasimamia maendeleo ya mpira, Mashindano
ambacho kinasimamia mashindano mbali mbali, Fedha na utawala, Sheria na
vyama wanachama na cha tano ni cha biashara na masoko. Vitengo hivi kwa
pamoja vinashirikiana kuhakikisha mpira unafundishwa, unachezwa na
unasimamiwa vyema. Aidha zipo Kamati mbali mbali zinazotusaidia
kutushauri kwenye mambo ya kitaalam na kutoa maamuzi vikiwa vyombo huru.
Pia tunacho chombo chetu kinachoitwa Bodi ya Ligi kinachosimamia
uendeshaji wa ligi zetu kuu tatu Ligi kuu ya daraja la kwanza na ya
daraja la pili. Ligi kuu ya vilabu vya wanawake inaendeshwa na kamati
ya mpira wa wanawake.
- Mashindano
Ili mpira uchezwe inabidi kuwepo
na mashindano. Wakati wote TFF inafanya jitihada za kubuni mashindano
mapya na kuhakikisha yaliyopo yanafanyika kwa mujibu wa kalenda. Kwa
sasa TFF tunaendesha mashindano makuu ya kitaifa saba: Ligi kuu, Ligi
daraja la kwanza, Ligi daraja la pili, Ligi ya mikoa, Kombe la
Shirikisho, Ligi ya vijana na Ligi ya vilabu vya wanawake. Ukiondoa ligi
daraja la pili na ligi ya mikoa mashindano yaliyobakia yote yanaonekana
moja kwa moja kwenye (live) kwenye Televisheni. Shirikisho liko mbioni
kuanzisha mashindano ya vilabu nane bora vya ligi kuu (Super 8). TFF pia
huwa inasimamia mechi mbali mbali za kimataifa za mashindano na za
kirafiki kwa timu za Taifa za rika mbali mbali za wanawake na wanaume.
- Masoko na Biashara
Kuendesha mpira ni gharama kubwa.
Wastani wa bajeti ya Shirikisho ni shilingi bilioni kumi na tano kwa
mwaka.Tunawashukuru FIFA ambao hadi mwaka jana walikuwa wanachangia
asilimia 3% ya bajeti hii na kuanzia mwaka huu wanachangia asilimi 6% ya
bajeti hii. Jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika kuhakikisha shughuli
za uendeshaji wa mpira hazikwamishwi na ukosefu wa fedha. Kitengo cha
biashara na masoko kinafanya jitihada kubwa kuhakikisha kila shindano
letu linakuwa na udhamini hata kama sio wa kukidhi mahitaji yote.
- Miundombinu
Ni muhimu sana kuwa na miundo
mbinu ya kutosha na yenye sifa ya kuchezewa mpira. Kwa kushirikiana na
wamiliki mbali mbali wa viwanja vya mpira TFF tumekuwa tukitoa ushauri
wa namna ya kuendeleza na kutunza viwanja vyetu vya mpira ili vifae
kuchezewa mpira wa kisasa. Aidha tunashukuru Halmashauri ya jiji la
Tanga kwa kuiipatia TFF miliki ya eneo la ekari 18 jijini Tanga, kwa
kushirikiana na FIFA eneo hilo litajengwa kituo cha kukuza na kuendeleza
vipaji vya mpira cha TFF. Michoro yake iko katika hatua za mwisho za
maandalizi.
- Maendeleo ya mpira wa miguu.
TFF tumejiwekea malengo mawili
makuu: Kucheza fainali za dunia mpira wa miguu wa wanawake Paris mwaka
2019 na kucheza fainali za kombe la dunia wanaume mwaka 2026.
Kwa upande wa mpira wa wanawake
katika kufikia azma hii mwaka huu tunaanzisha ligi kuu ya vilabu vya
mpira wa wanawake (Tanzania Women Premier League). Kutokana na ligi hii
vipaji vitaibuliwa kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu yetu ya Taifa
Twiga stars. Kikosi hiki mwakani kitakuwa kikikusanywa mara kwa mara,
kufanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki za kimataifa ili kujiandaa
na hatua za awali za kombe la dunia mwaka 2018.
Kwa upande wa maandalizi ya Taifa
stars kuelekea mwaka 2026 tayari program yetu imeanza kwa kuwa na
Serengeti Boys ambayo inapambana kucheza fainali za vijana za Afrika
mwakani umri chini ya miaka 17. Kwa sasa kikosi hiki kiko kambini
Seychelles kujiandaa na mechi dhidi ya Kongo tarehe 18 Septemba . Timu
hii pia ndiyo itapambana kucheza fainali za Afrika za vijana umri chini
ya miaka 20 mwaka 2019. Aidha kwenye shule ya Alliance huko Mwanza
tayari tuna kikosi cha awali cha timu ya Taifa cha vijana umri chini ya
miaka 15 ambacho kinaandaliwa kucheza fainali za Afrika umri chini ya
miaka 17 mwaka 2019. Tanzania tutakuwa wenyeji wa fainali hizi kwa mara
ya kwanza katika historia ya nchi yetu.
Pia mwaka huu tunaanzisha ligi ya
Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20. Kutokana na ligi hii mwakani
itaundwa timu ya Taifa ya awali ya vijana umri chini ya miaka 23
itakayopambana mwaka 2019 kutafuta fursa ya kucheza fainali za Olimpiki
Tokyo mwaka 2020. Kutokana na makundi haya makuu matatu kuanzia mwaka
2021 walimu wetu wa mpira wataweza kuanza kutengeneza kikosi imara cha
Taifa stars kuelekea Fainali za Kombe la dunia 2026. Gharama kubwa
zinahitajika kugharimia program hizi na tunaomba Serikali na wadau
wengine mtushike mkono ili tufikie azma yetu ya kucheza World Cup 2026.
Mheshimiwa Waziri ninaomba nigusie
uendeshaji wa ligi yetu kuu na utoaji wa leseni za vilabu.Kama
nilivyosema hapo awali Ligi kuu inasimamiwa na bodi ya ligi kwa
maelekezo ya kanuni za mashindano kama zinavyopitishwa na kamati ya
Utendaji kila mwaka. Mheshimiwa Waziri kinacholiongoza Shirikisho katika
uendeshaji wa ligi kuanzia usajili, upangaji wa ratiba,upangaji wa
waamuzi na utoaji wa adhabu ni kwa mujibu wa kanuni tulizojiwekea na
kauli mbiu ya #fairplay,haki mchezoni.
Ninaomba nieleze pia kuwa kufuatia
maagizo ya FIFA sasa tupo hatua za awali za kutoa leseni kwa vilabu
zinazohalalisha vilabu kushiriki katika ligi. Mahitaji makuu ya leseni
hizi ni klabu kuwa na menejimenti na kumbukumbu za mahesabu yake ya
fedha ,kuwa na maeneo ya kufanyia mazoezi na kucheza mechi,kuwa na
program za maendeleo ya mpira wa vijana na mwisho kueleza kinagaubaga
nani anamiliki na kuendesha shughuli za kila siku za za klabu (ownership
and control). Katika hili la umiliki ni marufuku klabu zaidi ya moja
katika ligi moja kumilikiwa na mtu au mamlaka moja. Pia kanuni ya leseni
za vilabu ina kipengele cha kipimo cha sifa cha nani anaruhusiwa
kumiliki au kuendesha klabu ya mpira wa miguu , mipaka ya mamlaka yake
na mahusiano na Shirikisho na mamlaka nyingine za juu zikiwemo
Serikali,FIFA,CAF na CECAFA.
Mheshimiwa Waziri, ninaomba
nimalizie kwa kukushukuru tena kwa kuchukua muda wako kuwa na sisi leo.
Familia ya mpira wa miguu Tanzania inafarijika sana unapokuwa karibu na
sisi na tunaahidi kuendelea kudumisha nidhamu katika utendaji wetu na
kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali yetu, vyombo na mamlaka
nyingine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni