DUMISHENI MICHEZO KUONGEZA UFANISI KATIKA KAZI; KATIBU MKUU KIONGOZI
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi
……
Na Shamimu Nyaki WHUSM.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John
Kijazi amewataka Watumishi wa Umma kushiriki katika Michezo mbalimbali
ili kuwa na afya imara itakayosaidia ufanisi katika kutekeleza kazi zao.
Balozi Kijazi ametoa rai hiyo
leo Jijini Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais Utumishi Dk.Lawrence Ndombaro katika Bonanza la
Michezo la ufunguzi wa mashindano ya thelatini na nne yanayojulikana
kama SHIMIWI lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru wa Jijini humo.
“Michezo inasaidia mwili kuwa na
afya njema na kuondoa msongo wa mawazo pamoja na kuleta nguvu na akili
katika mwili vinavyosaidia katika utendaji bora wa Mtumishi kwa
maendeleo ya Taifa”.Alisema Balozi Kijazi.
Aidha Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Kijazi amewataka Viongozi wa Serikali na Taasisi zake
kutenga muda kwa Watumishi wanamichezo wa kufanya mazoezi pamoja na
kuwapatia vifaa vya michezo ili waweze kufanikiwa katika mashindano
hayo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel
amewapongeza Watumishi wake kwa kushiriki Bonanza hilo na kuahidi kuwapa
muda mzuri wa maandalizi ili wafanye vizuri katika mashindano hayo.
Akifafanua maandalizi ya timu ya
Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mwenyekiti wa timu hiyo
Bw. John Manyika ameahidi ushindi kwa timu yake kwani wanaendelea
kijiandaa vizuri katika mazoezi.
Mashindano ya SHIMIWI
yanatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu mjini Dodoma kuanzia
tarehe 14 ikiwa ni kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kmbarage Nyerere.
Bonanza hilo lilimalizika kwa
timu ya Jiji la Dar es Salaam kutwaa Kikombe kwa kuwa na wanamichezo
wengi ikifuatiwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni