HOTUBA YA MGENI RASMI
WAZIRI WA NCHI – OFISI YA RAISI
TAMISEMI
Mh. GEORGE SIMBACHAWENE
KATIKA UFUNGUZI WA SIKU YA
USOMAJI DUNIANI
TAREHE 16 SEPTEMBA 2016
UKUMBI WA KARIMJEE – DAR
ES SALAAM.
Waheshimiwa
mabalozi,
Muwakilishi
wa UNESCO
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Wakuu
wa wilaya
Wakurugenzi
Watendaji wa Halmashauri
Maafisa
elimu
Makampuni
washirika
Mashirika
ya kimataifa
Mashirika
wahisani
Mashirika
yasiyo ya kiserikali
Waalimu
wa shule mbalimbali
Waandishi
wa habari
Wanafunzi
Ndugu
waalikwa
Mabibi
na Mabwana
Kwanza
napenda kuchukua nafasi kutoa shukrani kwa kuniarika katika siku muhimu ya
kujipima hali yetu ya usomaji na kunipa jukumu kubwa la kuwa mgeni rasmi katika
sherehe hizi za Siku ya Kimataifa ya Usomaji. Binafsi nimefarijika kuona ushirikiano
uliopo miongoni mwa mashirika na taasisi zinazojishughulisha na kuboresha elimu
hapa nchini. Kama mnavyojua, hiki ni kipindi cha Bunge, lakini kutokana na
umuhimu wa tukio hili la leo, nimeamua kushiriki nanyi.
Mnamo
mwaka 1965, mkutano wa dunia wa mawaziri wa elimu ulikutana huko Tehran nchini
Iran kuzungumzia jinsi ya kufuta ujinga duniani. Moja ya mapendekezo ya Tehran
ni kuanzishwa kwa siku ya Usomaji duniani, kuendeleza dhana ya usomaji
endelevu. Mwaka 1966, Siku ya Usomaji Duniani ilisheherekewa chini ya usaidizi
wa UNESCO na washirika wake.
Mwaka
2015, viongozi wa nchi mbalimbali duniani walikubaliana na kupitisha malengo
endelevu ya maendeleo, na lengo la nne limejikita katika kuhakikisha tunafuta
ujinga kabisa ifikapo mwaka 2030. Safari hii si nyepesi na serikali pekee
haiwezi kuitembea peke yake, bado ushirikiano wa wadau wote wa elimu
utahitajika, na tayari tunaona taasisi nyingi zimeianza safari hii, na hii
imetupa changamoto kwa upande wetu wa serikali.
Ndugu
zangu wadau, kama wote tunavyojua, moja ya malengo katika ilani ya uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi, ni kuhakikisha kila mtoto nchini anapata nafasi ya elimu
tena bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Kongamano mtakalofanya
leo, limekuja kwa muda muafaka, wakati serikali tunatafakari tutawezaje
kuboresha mfumo mzima wa elimu nchini na kuhakikisha kila mtoto anaweza kusoma
na kuandika vizuri afikapo darasa la tatu.
Ninajua
shirika kama Room to Read limekuwa likichangia sana kuboresha hali ya usomaji
hapa nchin, kwa kutujengea maktaba katika shule za msingi, na kuweka vitabu
vyote stahiki, wanawafundisha waalimu wetu wa darasa la kwanza na la pili mbinu
na stadi za ufundishaji, na kuhakikisha vitabu vya kufundishia vipo shuleni na
vitabu vya wanafunzi vya kujifunzia kwa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.
Mchango wao umeweza kuonyesha njia kuwa wanafunzi wanaweza kujua kusoma na
kuandika vizuri wanapoingia darasa la tatu.
Ndugu
zangu wadau, pia wote tunajua kuwa Raisi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli ameongeza mkakati katika kuboresha
elimu kwa kuhakikisha kila mtoto aliyeko shuleni anakaa kwenye dawati, juhudi
zake zimezaa matunda mazuri sana na kupunguza uhaba mkubwa sana wa madawati,
nipende kutumia fursa hii kuwashukuru nyote na hususani mashirika na taasisi
zilizojitoa kwa dhati kuchangia juhudi hizi. Hata hivyo, juhudi hizi zimeibua changamoto
ya vyumba vya madarasa, tunaendelea na juhudi za kupunguza uhaba huu kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi za wengi wenu mliopo hapa,
wananchi wa maeneo ya shule zilipo na wafadhili mbalimbali.
Takwimu
za kitaifa za sensa ya makazi na watu ya mwaka 2012, inaonyesha asilimia 22 ya
watanzania hawawezi kusoma na kuandika kwa ufasaha, asilimia 81.7 ya
wantanzania wana elimu ya msingi, asilimia 14.4 elimu ya sekondari na asilimia
2.3 tu ndio walio na elimu ya chuo kikuu. Kiwango hiki kidogo kwa kadiri elimu
inavyoenda juu kinasababishwa na kutokuwa na msingi imara kipindi cha mwanzo wa
kuanza safari ya elimu. Hakuna mzazi anayempeleka mtoto wake shule ili amalize
akiwa hajui kusoma na kuandika, kila mzazi anapomuandikisha mtoto shule mtoto
wake, anakuwa na matumaini makubwa juu yake, lakini matumaini hayo hufifia pale
dalili za wazi zinapoonekana za kutojua kusoma na kuandika kwa ufasaha.
Kwa
mfumo na juhudi zinazofanywa na Room to Read, katika kuhakikisha wanafunzi
wanajua kusoma na kuandika wafikapo darasa la tatu, kuna jambo tunalotakiwa
kujifunza sisi kama serikali kutoka kwao, mie binafsi nazijua kazi zao na
matokeo ya kazi zao nayajua, ni wazi kwa mfumo huo uwezekano wa kuwa na
asilimia 0 ya wasiojua kusoma na kuandika ifikapo mwaka 2030 ni mkubwa sana kwa
Tanzania. Tayari wizara yangu tumeanza kufanya kazi kwa ukaribu sana na wadau
mbalimbali wanaotusaidia katika elimu kuhakikisha lengo hili tunarifikia.
Ndugu
zangu wadau, Serikali yetu ya awamu ya Tano ipo tayari kuunga mkono juhudi kama
zenu za kuboresha elimu kwa manufaa ya watoto wetu, napenda kuwahakikishia kuwa
mlango wa Wizara yangu upo wazi kwa wote walio tayari kushirikiana nasi katika
kuutokomeza ujinga na sisi tutatoa ushirikiano mkubwa kwenye hilo.
Ndugu
zangu wadau, filosofia ya Room to Read ni ‘Mabadiliko
ya Dunia Yanaaza na Watoto Walioelimika’ Filosofia hii inatugongea kengele
ya kuamka kutoka usingizini, na kuchangia katika mabadiliko ya Tanzania kwa
kuwa na watoto watakaojua kusoma na kuandika kwa ufasaha wafikapo darasa la
Tatu.
Mwaka
huu kauli mbiu ya Siku ya Usomaji ni “Kusoma
yaliyopita, Kuandika Yajayo” (Reading the Past, Writing the Future). Wakati
ni huu sana wa kuhakikisha tunatafakari safari yetu ya kufuta ujinga kabisa
ifikapo mwaka 2030, ninatamani siku kama hii kila mwaka tuwe tunakutana na
kupeana mrejesho wa wapi tumefika, ninajua mashirika kama Hakielimu, Twaweza na
wengine wanaweza kutusaidia sana kwenye hili. Hata mijadala tutakayofanya hapo
baadae, itakuwa inatusaidia katika juhudi za kuandaa yajayo.
Kwa
mara nyingine tena, nawashukuruni sana kwa kunipa nafasi hii, na nina Imani kwa
kushirikiana nanyi Tanzania tutaweza kufikia lengo la kufuta kabisa ujinga
ifkapo mwaka 2030.
Asanteni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni