TETEMEKO: MALINZI AWAPA POLE KANDA YA ZIWA, BURUNDI NA UGANDA
Rais wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameshitushwa na taarifa za tukio la
tetemeko kubwa ardhi lenye mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7
lililotokea jana Septemba 10, 2016 katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa
kadhalika nchi za Burundi na Uganda.
Mikoa ya Kanda ya Ziwa iliyopata
athari kwa mujibu wa taarifa ni Mwanza, Mara na Kagera nchini na
kuripotiwa kuua zaidi ya watu 10 na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa
sambamba na kubomoa majengo mbalimbali.
Rais Malinzi mara moja
anaungana na Serikali katika kusubiri tathmini na kisha kuangalia namna
TFF itakavyoweza kusaidia kama sehemu ya wadau katika jamii. TFF
inaamini kuwa baadhi ya waliopata maafa ni familia ya mpira wa miguu si
ndani tu ya nchi, bali pia nje ya mipaka ya Tanzania.
Hivyo, Rais Malinzi ametutuma
salamu za rambirambi kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na
marafiki na anawaombea marehemu wapumzishwe mahali pema peponi. Amina.
Na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu.
Katika salamu hizo, pia Rais
Malinzi amemtumia Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Burundi (BFF),
Marlon Kuylen kwa sababu sehemu ya Bujumbura imeguswa na tetemeko hilo
kadhalika ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Uganda (FUFA), Moses Magogo baada ya ripoti kuonesha kuwa
tetemeko hilo limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda.
Wataalamu wa elimu ya miamba – Jiolojia wanasema kwamba lilikuwa ni
kubwa kwa mujibu wa vipimo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni