KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI PWANI CHAKUSANYA BIL.2.033
Kamanda wa kitengo cha Usalama barabarani mkoani Pwani, Abdi Issango pichani.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
……………..
Na Mwamvua Mwinyi
Kikosi cha usalama barabarani mkoa
wa Pwani kimeliingizia serikali mapato ya zaidi ya sh.bil.2.033 katika
kipindi cha januari hadi agosti mwaka huu .
Kikosi hicho kimekusanya mapato hayo kupitia ukamataji wa makosa mbalimbali ya usalama barabarani mkoani humo.
Mkuu wa usalama barabarani mkoani
Pwani, Abdi Issango alisema katika kupambana na ajali wameweza
kuendesha misako na kufanya ukaguzi mbalimbali katika barabara kuu na za
ndani ya miji.
Alieleza kuwa kwa kipindi miezi
nane wamekamata jumla ya makosa 68,109 ambapo yaliyolipiwa kiasi hicho
cha fedha ni 67,785 mwaka huu.
Kamanda Issango alisema makosa
hayo yakilinganishwa na ya mwaka jana kipindi hicho kuna ongezeko la
makosa 20,797 ambayo ni sawa na ongezeko la sh. mil. 569,400 sawa na
asilimia 38.89.
Alisema kuwa katika kipindi kama
hicho mwaka 2015 kitengo hicho kilikamata makosa 47,109 na yaliyolipiwa
ni 46,988 sh.bil. 1,464,150.
Aidha akizungumzia matumizi ya
speed radar mpya 24 za kisasa walizopewa mwaka jana ambazo zinapiga
picha na kurekodi wameweza kukamata makosa ya magari yanayokwenda kwa
mwendo kasi 32,753 .
Kamanda Issango alisema magari
hayo yaliyokamatwa kwa ajili ya kukimbiza magari yalilipiwa faini sh.
mil 982,590 kutoka januari hadi agosti mwaka huu.
“Vitendea kazi tulivyonavyo ikiwa
ni pamoja na speed radar hizi za kisasa, tunaweza kusema sisi Pwani
tumefanikiwa kudhibiti ajali zitokanazo na mwendo kasi kwa asilimia 100
hasa mabasi ya abiria”alisema Issango.
Hata hivyo kitengo hicho kuelekea
maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani wameanza kutoa
mafunzo mbalimbali kwa waendesha pikipiki,wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari na mikusanyiko ya watu ili kuwapa uelewa wa matumizi sahihi
ya alama za barabarani.
Issango aliwataka madereva ,abiria
na watumiaji wengine wa barabara kuu kuzingatia kanuni,sheria na
taratibu ya matumizi ya njia hizo kuu ili kuendelea kudhibiti ajali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni