WAKALA WA UFUNDI NA UMEME TEMESA PWANI WATUPIWA LAWAMA
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi
Evarist Ndikilo wa katikati,akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa
wakiwemo wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri, wakuu wa wilaya na
baadhi ya wabunge kuhusu hoja waliyoiibua kuhusu wakala wa ufundi na
umeme TEMESA ,wa kwanza ma mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Pwani
Ridhiwani Kikwete.
Meneja wa wakala wa ufundi na
umeme(TEMESA )Mkoani Pwani ,Richard Mutagulwa wa tatu kutoka kushoto
aliyefungata mikono akifuatilia kwa makini malalamiko yanayotolewa na
viongozi mbalimbali mkoani hapo juu ya wakala huo kuzorota katika kazi
zake na kutoza gharama kubwa za matengenezo ya magari ya serikali.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………….
Na Mwamvua Mwinyi
WAKALA wa ufundi na umeme (TEMESA)mkoani Pwani,umelalamikiwa
kuwa na mafundi wa mitaani lukuki na kuzorota katika kufanyakazi zake
ipasavyo huku ikitoza gharama kubwa za matengenezo katika magari ya
serikali.
Wakala huo unatupiwa lawama za
kutengeneza kwa gharama kubwa kuanzia 500,000 hadi mil.11 kwa gari moja
wakati magari hayo yangepelekwa kwa mafundi wa kawaida gharama zingekuwa
nafuu.
Licha ya hayo magari ya mkuu wa
mkoa huo sambamba na katibu tawala wa mkoa bado yapo kimatengenezo kwa
zaidi ya miezi mitatu sasa . kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya
ufundi licha ya gharama zao kuwa juu.
Hayo yalisemwa na baadhi ya
wabunge,wenyeviti wa halmashauri,wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa
serikali ya mkoa wa Pwani kufuatia kero kubwa wanayoipata mara
wanapopeleka magari kutengenezwa na TEMESA.
Waliiomba serikali iangalie njia
nyingine ya kutengeneza magari yake ya serikali badala ya kutumia wakala
huo ambao hauwasaidii zaidi ya kupoteza fedha nyingi.
Changamoto hiyo pia imemkuta mkuu
wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo ambae anasema hata yeye gari
lake liko linatengenezwa huko,hivyo kuna haja ya sheria ya utengenezaji
magari kuangaliwa upya.
Nae mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Kibaha Mansoor Kisebengo ,alisema wamepeleka magari yao
matatu kwa ajili ya matengenezo na kila gari limetakiwa gharama ya
mil.11.
Alisema badala ya kutengenezwa kwa
magari hayo lakini baada ya matengenezo yamerudishwa yakiwa na hali
mbaya zaidi hivyo kuwapa hasara.
Kisebengo alisema serikali
inawajibu wa kuliangalia jambo hilo kwani fedha hizo zingeweza kutumiwa
na mambo mengine ya kijamii kuliko kuzipoteza .
Mwenyekiti wa halmashauri ya
Chalinze,Saidi Zikatimu alieleza kwamba ni vyema serikali ikaawamini
kama wanavyowaamini katika matumizi mengine ya fedha kwa kuwaruhusu
kutengeneza magari kwa mafundi wa nje.
Alisema walipeleka magari yao TEMESA lakini magari hayo bado ni mabovu hayafanyi kazi na hela imepotea.
Zikatimu alisema wakala huo
wamekuwa wakitengeneza magari hayo kwa fedha nyingi huku yakiwa chini ya
kiwango na kusababisha magari hayo kutofanya kazi baada ya
kutengenezwa.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kibiti, Alvera Ndabagoye alisema serikali inapaswa kuliangalia jambo hilo kwa umakini.
Alisema kwasasa hakuna haja ya kuwa na Temesa kwani wamekuwa wakifanyakazi kwa kutokuwa na umakini .
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini
Hamoud Jumaa alisema wamefanya utafiti juu yao na kugundua kuwa uwezo
wao ni mdogo ,na siku chache zilizopita walitengeneza gari la wagonjwa
la Kwala ambapo gharama zilikuwa ni mil.5 lakini baada ya muda mfupi
limeharibika na sasa liko sokoni wakitaka kuliuza.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Pwani Abdi
Isango alisema kuwa gharama za wakala hao ni kubwa na hazikidhi lakini
kwa mafundi wengine toka nje wanatengeneza kwa uhakika .
Akijibu malalamiko hayo, meneja wa Temesa mkoa wa Pwani,Richard Mutagulwa, alisema ni vema walalamikaji wakafanya utafiti .
Alisema huwa wakitengeneza magari hayo bila matatizo na lengo lao ni kutoa huduma bora kwa wateja wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni