MKURUGENZI APEWA CHANGAMOTO KUOKOA MIFUGO
Na Mahmoud Ahmad Monduli
Baraza la madiwani limemtaka mkurugenzi wake kuangalia ni jinsi gani wataweza kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa maji ya malisho ya mifugo ambapo mabwawa mengi yapo kwenye hali mbaya kwa kujaa tope na kukauka maji.
Akizungumza kwenye Baraza hilo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Izack Joseph aliwata watendaji wa idara ya mifugo kuanza kutoa elimu kwa wafugaji kupunguza mifugo na kufuga kisasa kwa kuangalia maeneo na hali ya mazingira badala ya ufugaji wa kizamani kuwa na kundi kubwa lisilo na tija.
Izack alisema kuwa kumekuwa na uharibufu mkubwa wa mabwawa ya maji mengi yakiwa yamejaaa tope na mengine kukauka kwa ukosefu wa maji ambapo mengine yaliharibiwa na mvua zilizonyesha na kujikuta yakiwa yamejaa tope,hali inayopelekea mifugo mingi kukosa maji ya kutosha ambapo tutazidi kutoa elimu kwa wananchi kufuga kisasa.
Alisema kuwa halmashauri inachukuwa hatua za maksudi kukabiliana na hali hiyo ambayo kama itaachwa itaweza kuleta maafa kwa mifugo wilayani humo ambapo wataanza na kuunga mabomba na kusambaza maeneo mbali mbali wilayani humo ili kuondokana na tatizo hilo.
“Nawasihi wafugaji wenzangu kuanza kupata elimu ya ufugaji kwa kufuga mifugo michache yenye tija badala ya kuwa na kundi kubwa ambalo halina faida kwa maendeleo yako,tuache kufuga kizamani tuanze kufuga kisasa zaidi”alisisitiza Mwenyekiti huyo wa halmashauri.
Aidha kwa Upande wake diwani wa kata ya Moita Edward Sapnyuu alisema kuwa hadhani kama kuna kijiji wilayani humo ambacho hakiitishi mkutano wa wananchi wa kijiji,kitongoji na Kata na kama wapo wanaofanya hivyo ni kuwakosesha wananchi haki yao ya msingi ya kujadili maendeleo yao.
Sapnyuu akisoma ripoti ya maendeleo ya kata yake ya Moita mbele ya baraza la madiwani kwa robo mwaka alibainisha kuwa bado wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbali mbali katika Nyanja za elimu,maji na Ardhi na huduma za kijamii ambapo aliwataka watendaji kukaza buti kuwasaidia wananchi kutatua kero mbali mbali za kijamii.
Nae Diwani wa viti maalum (Chadema) Secilia Ndosi alisema kuwa Tatizo la uhaba wa maji ya malisho ya mifugo wilayani humo ni changamoto ya kuangalia suala zima la sekta ya mifugo kwa wafugaji kuanza kbadilika na kuachana na ufugaji wa kimazoea kwa kuwa na kundi kubwa lisilo na tija na kugeuka kufuga kisasa na kuwa na kundi dogo lenye tija kwa kuwa na mifugo michache unayoweza kuihudumia kwa matibabu na bila kuathiri mazingira.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni