Ijumaa, 23 Septemba 2016

JUMAA AUNGANA NA WAKAZI SOGA KUMKATAA MENEJA WA MWEKEZAJI MOHAMMED INTERPRISES


jumaa2
Mbunge wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akizungumza na wakazi wa kata ya Soga ,kuhusiana na mgogoro wao baina ya meneja wa mwekezaji Mohammed interprises ,Amir Mndeme pamoja na mgogoro wa wakazi hao na mwekezaji uliodumu kwa miaka 21 sasa.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
jumaa4
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama, akizungumza na wakazi wa kata ya Soga ,kuhusiana na mgogoro baina yao na meneja wa mwekezaji Mohammed interprises Amir Mndeme pamoja na mgogoro uliodumu kwa miaka 21 sasa juu ya mwekezaji huyo kuhodhi eneo kubwa na kusababisha wananchi kupungukiwa na eneo la  kujishughulisha na shughuli za kijamii ikiwemo kilimo(Picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Soga
MBUNGE wa Kibaha Vijijini,Hamoud Jumaa ,ameungana na wakazi wa kata ya Soga kumkataa meneja anaesimamia eneo la mwekezaji Mohammed Interprises ,Amir Mndeme, anaedaiwa kutishia amani watu ,kudharau serikali na kujitia mungu mtu.
Aidha wameitaka serikali ifanye uchunguzi wa kina na kuangalia upya umiliki wa eneo la mwekezaji huyo ambalo lina ukubwa wa hekta 20,000 na kusababisha wananchi kupungukiwa  na maeneo ya kujishughulisha ikiwemo kilimo.
Akizungumza katika mkutano wa wananchi ,katika kijiji cha Soga,Jumaa alisema mgogoro baina ya wananchi kata ya Soga na Mohammed Interprises umedumu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Alisema mgogoro huo umefikia pabaya kwani vijana 16 wamekamatwa na polisi kwa madai ya kuchimba mchanga kwenye eneo la mwekezaji hali iliyosababisha wananchi kuifunga ofisi ya serikali ya kijiji kwa siku mbili kutokana na kutokuwa na imani nayo.
Jumaa alieleza kufuatia kutokea kwa matukio hayo alilazimika kwenda eneo la tukio ambapo wananchi walisema hawafungui ofisi hiyo hadi viongozi wa wilaya ama mkoa wafike kusikiliza kilio chao.
“Mgogoro huu kwasasa unakua na kuhofia kupoteza amani iliyopo,imefikia hatua ya meneja wa MO kutumia polisi kunyanyasa wananchi na upande wa wananchi kuweka chuki nae”
‘Tangu aletwe meneja mpya bwana Mndeme, amekuwa akitishia amani na kutumia nguvu za pesa kunyanyasa wananchi.Mameneja hapa wameshakuja zaidi ya sita lakini meneja huyu amekuwa kero kubwa”alisema Jumaa.
Mndeme amekuwa akikataza watu kukatisha katika eneo lake,kuchimba mchanga kwenye machimbo ya mchanga ambayo anadai yapo kwenye eneo hilo na kupelea kuwanyima uhuru wananchi.
“Machimbo hayo ni ya asili ,vijana wanajitafutia kipato lakini yeye anakataza watu wasichimbe na kutumia polisi kuwakamata ambapo juzi walikamatwa vijana 16 ”alisema Jumaa.
Jumaa alisema hatua zichukuliwe haraka pamoja na mwajiri Mohammed inteprises amwondoe meneja wake ili kurejesha amani kwa jamii.
Nae mtendaji wa kata ya Soga, Betram Mfalamagoha,alisema septemba 20 baadhi ya polisi walioambatana na Mndeme walienda kuwakamata vijana 16 ,waliokuwa wakichimba mchanga kwenye machimbo ya mchanga.
Alisema kijana mwingine aligongwa na gari la mikopo kisha, askari polisi walikwenda na kuendelea kumpiga kijana huyo licha ya kuwa amegongwa na sasa yupo Tumbi hospital kwa matibabu.
Wakazi wa kata hiyo, akiwemo Hussein Maro,Ramadhani Rashid ,Iddi Muhunzi na mwenyekiti wa kijiji cha Kipangege Shomary Mwinshehe ,walisema wamechoshwa na tabia anazozifanya meneja Mndeme.
Walisema baadhi ya polisi wamewekwa mkononi kwani wamekuwa wakitumika na meneja huyo kwenda kuwakamata wananchi na kuwashurutisha bila kosa.
Mzee Omary Kibwana ,alisema anaimani na serikali kuwa itaangalia suala hilo kwa kina ili kuleta suluhisho la mgogoro huo wa kipindi kirefu.
Mkuu wa kituo cha polisi Kibaha,Emmanuel Bondo ,alisema kazi yao ni kulinda amani kwa watu wote bila kupendelea.
Kamanda Bondo alisema ,kutokana na malalamiko aliyofikishiwa atayafanyia kazi na kuahidi kushirikiana na wananchi hao pale patakapokuwa na tatizo.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama alifika katika eneo hilo na kutoa agizo kuwa meneja Mndeme aondoke kuanzia sasa na mwajiri wake atafute meneja mwingine.
Alisema hakuna jeuri zaidi ya serikali na serikali haiwezi kumvumilia mtu mmoja ambae anatishia maisha ya watu na kuwajengea hofu ya kuishi.
Assumpter alieleza hakuna mungu mtu zaidi ya wananchi na sasa yeye ndie atakuwa saizi yake huyo meneja anaetikisa kata nzima kwa pesa zake.
Aliomba wananchi wasibuguziwe na kuwataka polisi wasiwe wepesi wa kuhongwa kitu kidogo kwa ajili ya kuwakandamiza wananchi.
Assumpter alitoa pole kwa kijana aliyegongwa na gari la mikopo  kisha kupigwa tena na polisi kwa madai ya kuingia kwenye eneo la MO, na kuongeza kuwa amesikitishwa na vitendo vya meneja huyo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuanzia sasa Mndeme aondoke,na kuwaasa wananchi wasifanye fujo wala maandamano bali watulie na serikali ipo kwa ajili yao.
Mndeme alipatikana kwa njia ya simu na kusema hawezi kuzungumzia suala hilo kutokana na vitisho ambavyo ameshaanza kuvipata,na baada ya kujibu hayo alikata simu.
Baada ya mkutano huo wananchi waliamua kutoa magogo na makuti waliyofunga kwenye ofisi ya serikali ya kijiji ambayo waliifunga kutokana na sakata hilo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni