NA TINA RUBEN,
Waziri wa Uchukuzi,Samuel Sitta amesema kuwa RAHCO (Kampuni ya Rasimali za Reli)wamekamilisha utaratibu wa kumpata Mshauri wa Mradi ambaye ni Kampuni ya Roths child ambayo itawezesha kupata fedha za ujenzi wa Reli Mpya ya kati kwa Kiwango cha "Standard Gauge "ambayo gharama yake ya ujenzi ni Dola za Kimarekani Bilioni 7.6.
Alisema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari,amesema fedha hiyo ni ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 14 reli hiyo itakuwa na urefu wa Kilomita 2561.
Sitta alisema mradi huo utakuwa mkubwa kutekelezwa na serikali toka tupate Uhuru,na Serikali haitatoa hata dola Moja kutoka Hazina bali utagharamiwa na mabenki ambayo ndiyo yatakayotoa fedha.
Reli hiyo Mpya kabisa tofauti na iliyopo itakuwa yenye uwezo mkubwa wa Kimataifa "Standard Gauge railway " itaanzia Dar es Salaam Mpaka Kigoma, kupitia Tabora, Mwanza,Isaka hadi Rusumo; Kaliua -Mpanda -Karema na Uvinza -Musongati nchini Burundi.
Pia alisema reli hiyo itasaidia kukidhi mahitaji makubwa ya ubebaji mizigo kwenda nchi jirani za DRC, Rwanda, Burundi, na Uganda na itasaidia Wananchi kwenda mikoani kwa wingi na kwa kasi zaidi.
"Wengi watajiuliza kwa nini tumeamua kujenga reli Mpya?
Ni kutokana na sababu kwamba reli iliyopo sasa ambayo ni ya Kiwango cha "meter Gauge " uwezo wake wa kubeba mizigo hata baada ya ukarabati kwa mwaka ni tani Milioni 5,ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo ya Kanda hii ambayo itafikia tani Milioni 30 ifikapo mwaka 2025".Alisema Sitta.
Mradi huu wa kujenga reli ya kati utaajiri watanzania takribani 300,000 watakaohusika na ujenzi wa reli hiyo itakayojengwa kwa muda wa miaka 5 .Reli hiyo itafanya upelekaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam Mpaka nchini DRC kuchukua muda wa takribani saa 12.
"Tumejipanga ili Uzinduzi wa ujenzi wa reli hii ya kihistoria ufanywe na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuweka jiwe la msingi ifikapo tarehe 30 Juni , 2015 yaani Mwaka huu tulionao kule Mpiji Kituo cha stesheni Mkoa wa Pwani ambako ndiko reli itaanzia". Alisema
Kwa ujumla reli zote zitagharimu jumla ya kiasi cha Dola za kimarekani Bilioni 14.2 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 26 zitaajiri zaidi ya watanzania Milioni Moja kwa miaka yote zitakapokuwa zinajengwa.
Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta akizungumza na waandishi leo ofisini kwake jijini Dar Es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni