Mbunge wa Mbinga Magharibi na mkurugenzi wa kundi la uhamasishaji la CCM, Tanzania One Theatre (TOT), Kapteni mstaafu John Komba (61), amefariki dunia jana.
Akithibitisha kifo hicho Dk Elisha Ishan alisema; “Nilimpokea na kuanza kumpima shinikizo la damu na vipimo vingine lakini tayari vilikuwa havifanyi kazi na hapo ndipo tukathibitisha kuwa ndugu yetu ameaga dunia.”
Dk Ishan wa Hospitali ya TMJ alisema kuwa, Kapteni Komba alifikishwa hospitalini hapo saa 10:00 jioni akiwa amebebwa katika machela.
Dk Ishan alisema hawezi kujua kilichomuua lakini akaongeza alikuwa na tatizo la shinikizo la damu na hivi karibuni alikwenda kwenye kiliniki yake.
“Kwa kifupi ni hayo na kwa sasa mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.”
Akizungumzia msiba huo, Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel alisema Komba aliyekuwa nyumbani kwake Tangi Bovu jijini Dar es Salaam alianza kujisikia vibaya kutokana sukari yake kuwa juu wakati huo huo presha yake nayo ilikuwa imepanda, hivyo walimpeleka Hospitali ya TMJ iliyopo Upanga kwa matibabu.
Alisema kwa sasa mwili wa mbunge huyo ambaye ni kada wa maarufu wa CCM umehifadhiwa Hospitali ya Lugalo na kwamba taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni