CHAMA CHA TBN CHATOA SHUKURANI KWA BENKI YA NMB KWA KUKUBALI KUWA MDHAMINI WA MKUTANO WAO.
Kwa niaba ya Chama cha 
Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini ‘Tanzania Bloggers 
Network’ (TBN) napenda kuwashukuru kwa kujitokeza katika mkutano huu 
muhimu. TBN inajua kuwa mnamajukumu mengi ya kuujuza umma masuala anuai,
 lakini mmechagua kuja kwetu ili kutusikiliza tulichowaitia na baadae 
tunaamini mtaujuza umma juu ya tukio letu.
TBN iliosajiliwa rasmi na Serikali
 mwezi Aprili, 2015 kwa kushirikiana na wataalam wa masuala ya habari na
 mitandao ya kijamii imeandaa semina kwa wanahabari hawa wa mitandao ya 
kijamii hasa ‘Bloggers’ itakayofanyika jijini Dar es Salaam. Semina hii 
maalumu ambayo itajumuisha mafunzo ya siku mbili yaani tarehe 5 na 6 ya 
Mwezi Desemba, 2016 kwa washiriki takribani 150 kutoka Tanzania nzima 
(Bara na Visiwani) itafuatiwa na mkutano mkuu kwa wanachama hai wa TBN 
kujadili masuala mbalimbali ya chama na tasnia nzima ya mitandao ya 
jamii.
Ndugu Wanahabari, 
Katika mkusanyiko huu wanatasnia 
watapewa semina juu ya uendeshaji mitandao ya jamii kwa manufaa, 
upashaji habari kwa kutumia mitandao yao kwa kuziangatia maadili na 
namna ya kunufaika na mitandao hiyo kwa waendeshaji (kujipatia kipato) 
hasa ukizingatia kuwa wapo baadhi yetu tunaifanya kama ajira nyingine. 
Kimsingi lazima tukubali kuwa mitandao hii imekuwa tegemeo kubwa la 
kusambaza habari mbalimbali tena kwa muda mfupi tangu kutokea kwa tukio 
fulani, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuwapiga msasa wanaoiendesha
 ili kupunguza matumizi mabaya ya mitandao hii.
TBN inaamini njia pekee ya 
kupambana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ni kuendelea kutoa 
elimu kwa waendeshaji na watumiaji ili mwisho wa siku wasikubali 
kutumika vibaya au kuitumia vibaya mitandao hii katika kutoa taarifa. 
Kwa dunia ya sasa hakuna atakayepinga kuwa mitandao hii imekuwa 
ikielimisha umma, ikikosoa jamii na kiburudisha juu ya masuala anuai ya 
kijamii.
TBN inapenda kutoa shukrani kwa 
Serikali ya Awamu ya Nne na Tano chini ya Mh. Rais John Pombe Magufuli 
kwa ushirikiano alioanza kuuonesha hasa kwa kutambua mchango wa mitandao
 hii ya kijamii na hata kuitumia katika utoaji wa taarifa zao. Kimsingi 
hii ni hatua nzuri na ya kuigwa hasa katika ulimwengu huu ambapo dunia 
imekuwa kama kijiji kutokana na hatua ya maendeleo ya habari na 
mawasiliano.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kulitambua hili mnaweza kuona 
hata taasisi nyeti kama Ikulu nayo ina Blogu maalumu kwa ajili ya kutoa 
taarifa kwa umma, Idara ya Habari Maelezo nayo ina Blogu kwa ajili ya 
kutoa taarifa kwa umma juu ya masuala mbalimbali yanayopaswa kutolewa 
kitaarifa kwa jamii. Jambo la kujivunia zaidi kwa maendeleo ya mitandao 
hii hata Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. 
Nape M. Nnauye amekuwa mstari wa mbele kuona umuhimu wa mitandao ya 
kijamii hasa blogu na hata kuzitumia katika kupasha habari umma. Hata 
katika mkutano wetu wa kesho kutwa ndiye tunayemtarajia kuwa mgeni rasmi
 atakayetufungulia mkutano huo.
Ndugu Wanahabari,
Kwa namna ya pekee TBN inapenda 
kutoa shukrani za pekee kwa Benki ya NMB kwa kukubali kuwa wadhamini wa 
kuu wa mkushanyiko huo wa ‘bloggers’ kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa 
yetu. Kitendo cha kujitolea kufanikisha jambo hili kinaonesha namna gani
 NMB inavyowajali wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo hili la 
upashanaji habari kwa jamii.
Kama hiyo haitoshi tunapenda 
kuwashukuru wadhamini wengine ambao ni NHIF, SBL, PSPF na Coca Cola 
ambao wamejitolea kuungana nasi katika kufanikisha tukio hili la 
kuwaleta pamoja bloggers na kutoa mafunzo kwao. Tunaamini tutakuwa nao 
siku zote katika masuala mengi ya maendeleo ya tasnia ya mitandao ya 
kijamii.
Imetolewa na; Mwenyekiti wa Muda wa TBN
Joachim E. Mushi
0756469470
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni