Ijumaa, 2 Desemba 2016

Miaka 55 ya Uhuru Jimbo la Igalula linajivunia Mafanikio Makubwa


mfutakamba1
Na.  Immaculate Makilika – MAELEZO
WANANCHI wa Jimbo la Igulula wilayani Uyui Mkoani Tabora wamepongeza hatua na jitihada zilizofikiwa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya huduma za maendeleo ya jamii katika kipindi cha miaka 55 ya uhuru wa Tanzania Bara.
Wanazitaja huduma hizo ni pamoja na maji, afya, nishati, na elimu ambazo kwa kipindi kirefu zilikuwa zikikwamisha maendeleo ya wananchi, na kukamilika kwake kunahitimisha ndoto za siku nyingi za kupatikana kwa  huduma muhimu  jimboni  humo.
Wakitolea mfano wanasema mwaka 2015 jimbo hilo  limepata  nishati ya umeme kupitia gridi ya Taifa kwa asilimia 70 na hivyo kufanya kata za Goeko, Ngololo, Kigwa na Igalula kupata nishati hiyo adhimu sambamba na  kufikisha umeme wa mwanga wa jua katika kata za Tara, Loya, na Lutende.
Mbunge wa jimbo la Igalula Athumani Mfutakamba akizungumza na mwandishi wa habari hii, anaeleza kinagaubaga neema zilizopatikana ndani ya miaka 55 ya Uhuru katika jimbo hilo na kukiri wazi zinamfanya awe na shauku ya kuhadithia kila mara.
Dkt. Mfutakamba anasema jitihada hizo za Serikali pamoja na wadau wengine za kufikisha umeme katika jimbo la Igalula imekua nyenzo muhimu  kwa uchumi na ustawi wa maendeleo ya jimbo hilo.
“Umeme huu umekua ukitumika si tu kuwashia taa ama kumulika majumbani na mitaani ila hutumika pia  hospitalini, shuleni na katika shughuli mbalimbali zinazotumia nishati hiyo” anasema Dkt Mfutakamba.
Kwa mujibu wa Dkt. Mfutakamba anasema jimbo hilo limepata mafanikio makubwa katika sekta ya maji kwa kujenga visima virefu viwili vilivyoweza kutatua matatizo ya maji katika jimbo hilo.
Dkt. Mfutakamaba alisema jimbo hilo pia limefanikiwa kukamilisha ujenzi wa zahanati za Imalaseko, Goeko, Ngololo, Igalula na Loya pamoja na kupata vitanda ambavyo vinatumika kusaidia wanawake wanaojifungua.
Kuhusu sekta ya elimu, Mbunge Mfutakamba alisema kwa miaka mingi jimbo hilo halikuwa na shule ya sekondari, ambapo hadi sasa jimbo limeweza kuwa na shule ya sekondari Goeko.
Sambamba na hayo, Mbunge huyo aliipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ikiwemo za kusimamia kikamilifu rasilimali fedha na watu.
“Ni lazima tuunge mkono jitihada hizo kwa kulipa kodi ili fedha zitakazopatikana zisaidie katika shughuli mbalimbali za kutuletea maendeleo, badala ya kutegemea wafadhili pekee” alisema Mbunge huyo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni