WATANZANIA WATAKIWA KUSHIKAMANA NA KUIPENDA NCHI YAO
Na. Jovina Bujulu – Maelezo
WATANZANIA wametakiwa kushikamana, kupendana na kulinda rasilimali zao kwani wao ndio wenye mamlaka ya kuendesha nchi yao.
Wito
huo umetolewa leo jijini Dar es slaam na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Idara ya Sayansi na Siasa Dkt. Bashiru Ally wakati
wa mahojiano na Mwandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 55 ya
uhuru wa Tanzania ambayo yatafikia kilele tarehe 9 Desemba.
Akizungumzia
mafanikio ambayo nchi imefikia tangu ilipopata uhuru mwaka 1961 alisema
kuwa Tanzania imefanikiwa kujenga umoja wa kitaifa hasa kwa kutumia
lugha ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za Kitaifa na kimataifa.
“Matumizi
ya Kiswahili katika kazi za kitaaluma, kibiashara na nyanja za sayansi
yameimarisha umoja wa kitaifa” alisema Dkt. Bashiru.
Aidha
Dkt. Bashiru alimpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutumia
lugha ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa
kwa kuwa lugha hiyo ina utajiri wa maneno hivyo ikutumika vizuri
Tanzania itapiga hatua zaidi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Akizungumzia
suala la nchi kuelekea uchumi wa viwanda vidogo na viwanda vya kati
Dkt. Bashiru alisema kuwa ni vizuri viwanda vinavyoanzishwa sehemu
kubwa ya malighafi vikatumia rasilimali za nchini na vizingatie maslahi
ya watanzania kwa misingi ya usawa, haki na utu ili vizalishe ajira kwa
vijana wa Tanzania.
“Rais
awaamini Watanzania ndiyo wazalishaji namba moja hasa wazalishaji
wadogo na nguvu zielekezwe katika uzalishaji ili fedha zinazopatikana
zielekezwe katika huduma za kijamii kama vile elimu, afya na maji”,
aliongeza Dkt. Bashiru.
Kwa
upande wa suala la nidhamu ,Dkt. Bashiru alisema kuwa kumekuwepo na
mabadiliko makubwa kwa watumishi wa Umma ambapo wafanyakazi wanahi
kazini, kutumia lugha nzuri na kupunguza vitendo vya kudai rushwa.
Alimpongeza
Rais Dkt. Magufuli kwa juhudi anazozifanya za kukusanya mapato na
kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha hizo na alimtaka asilegeze kamba
katika kusimamia eneo la uzalishaji.
Alisema
kuwa jitihada hizo ndio zimesaidia Shule kifurika wanafunzi kutokana na
elimu bure, ongezeko la madawati mashuleni na mafanikio katika sekta ya
afya na kilimo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni