PLAN INTERNATIONAL YAZINDUA MRADI WA KUWAWEZESHA VIJANA NA WATOTO KUPITIA MICHEZO.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa
Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani, Wanchoko Chinchibera akiongea na
wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Mradi wa
Kuwawezesha Vijana na Watoto kwa Njia ya Michezo uliozinduliwa leo
wilayani humo.Mradi huo unaratibiwa na Shirika la Plan International.
Meneja Miradi wa Shirika la Plan
International, Grace Semwaiko akielezea kuhusu malengo ya mradi wa
Kuwawezesha Vijana na Watoto kwa Njia ya Michezo uliozinduliwa leo
wilayani Kisarawe.Mradi huo unaratibiwa na Shirika la Plan
International.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa
Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani, Wanchoko Chinchibera akikagua timu ya
mpira ya watoto wakati wa mradi wa Kuwawezesha Vijana na Watoto kwa Njia
ya Michezo uliozinduliwa leo wilayani humo.Mradi huo unaratibiwa na
Shirika la Plan International.
…………………………………………………………………
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Shirika
la Plan International limezindua Mradi wa Kuwawezesha Vijana na Watoto
kwa Njia ya Michezo ili kuwajengea uwezo wa kuwa mawakala hai wa
mabadiliko chanya katika jamii zinazowazunguka.
Mradi
huo umezinduliwa leo Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani na Afisa Maendeleo
ya Jamii wa Wilaya hiyo, Wanchoko Chinchibera ambaye ametoa wito kwa
watendaji wa Serikali, wazazi pamoja na jamii kwa ujumla kutoa
ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha mradi huo unatekelezeka.
Chinchibera
amesema mradi huo umekuja wakati muafaka kwani watoto na vijana
wanakabiliwa na changamoto ya ulinzi, usawa wa kijinsia pamoja na
ushirikishwaji mdogo katika michezo hivyo kupitia mradi huo watapata
maendeleo mazuri ya kielimu na kimakuzi pamoja na fursa ya kutatua
changamoto zao.
“Kupitia
michezo tunajenga afya, akili, malezi na makuzi ya mtoto lakini pia
michezo ni sehemu ambayo watoto wanaweza kupaza sauti zao na kujadili
kuhusu haki zao za msingi kwa njia ya nyimbo na mashairi hivyo tunaamini
kuwa tukianza kuwashirikisha watoto katika suala zima la michezo
tutatengeneza kizazi chenye maendeleo,”alisema Chinchibera.
Ameongeza
kuwa kupitia michezo, vipaji vingi vitaibuliwa ambavyo vitasaidia
katika kutengeneza ajira mbalimbali zitakazowawezesha vijana kujikomboa
kiuchumi na kuchangia katika pato la taifa hivyo amewahakikishia
wananchi kuwa mradi huo utazaa matunda mazuri.
Kwa
upande wake Meneja Miradi wa Shirika hilo, Grace Semwaiko amesema mradi
huo ni sehemu ya mpango mkakati wa tatu wa shirika hilo ambao kwa
ujumla unalenga kufikia jumla ya watoto 3,075 na vijana 3,109 katika
kuwahakikishia ulinzi na usawa wa kijinsia.
“Ni
matumaini yetu kuwa mradi huu utatekelezwa vizuri na hatimaye kufikia
malengo tuliyojipangia yakiwemo ya kukua kwa uelewa kwa jamii na wadau
wote kuhusu usawa wa kijinsia, kuhakikisha vijana na watoto
waliowezeshwa wanaleta mabadiliko katika jamii pamoja na kuimarika kwa
ulinzi wa watoto katika ngazi ya jamii hadi taifa,” alisema Bi Grace.
Alifafanua
kuwa mradi huo unawalenga wanafunzi wa Shule za Msingi kuanzia darasa
la 4 hadi la 7, wanafunzi wa Shule 6 za Sekondari, walimu, wazazi,
viongozi wa jamii na watendaji wa Vijiji, Kata pamoja na Watoto na
Vijana ambao hawasomi.
Mradi
huo utaratibiwa na shirika la Plan International pamoja na shirika la
Right to Play na utatekelezwa katika Kata mbili za Kiluvya na Malumbo
zilizopo wilayani humo ambapo jumla ya vijiji 10 vitanufaika.
Aidha
Bi.Grace aliongeza kuwa Mradi huo unatarajiwa kuwa wa miaka miwili na
utagharimu jumla ya shilingi 641,468,700 ambapo unatarajiwa kukamilika
mwezi Juni 2018.
Shirika
la Plan International la nchini Ujerumani ni miongoni mwa mashirika ya
Kimataifa yasiyo ya kiserikali ambayo yameonyesha juhudi kubwa za kuibua
miradi mbali mbali katika jamii na kuifadhili katika sekta za
Afya,Maendeleo ya jamii,Wanawake,Watoto na Michezo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni