Ijumaa, 2 Desemba 2016

WATANZANIA WATAKIWA KUSHIKAMANA NA KUIPENDA NCHI YAO


ft
Na. Jovina Bujulu – Maelezo
 
WATANZANIA wametakiwa kushikamana, kupendana na kulinda rasilimali zao kwani wao ndio wenye mamlaka ya kuendesha nchi yao.
 
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es slaam na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi na Siasa Dkt. Bashiru Ally  wakati wa mahojiano na Mwandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 55 ya uhuru wa Tanzania ambayo yatafikia kilele tarehe 9 Desemba.
 
Akizungumzia mafanikio ambayo nchi imefikia tangu ilipopata uhuru mwaka 1961 alisema kuwa Tanzania imefanikiwa kujenga umoja wa kitaifa hasa kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za Kitaifa na kimataifa.
 
“Matumizi ya Kiswahili katika kazi za kitaaluma, kibiashara na nyanja za sayansi yameimarisha umoja wa kitaifa” alisema Dkt. Bashiru.
 
Aidha Dkt. Bashiru alimpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa kwa kuwa lugha hiyo ina utajiri wa maneno hivyo ikutumika vizuri Tanzania itapiga hatua zaidi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
 
Akizungumzia suala la nchi kuelekea uchumi wa viwanda vidogo na viwanda vya kati Dkt. Bashiru alisema kuwa ni vizuri viwanda vinavyoanzishwa  sehemu kubwa ya malighafi vikatumia rasilimali za nchini na vizingatie maslahi ya watanzania kwa misingi ya usawa, haki na utu ili vizalishe ajira kwa vijana wa Tanzania.
 
“Rais awaamini Watanzania ndiyo wazalishaji namba moja hasa wazalishaji wadogo na nguvu zielekezwe katika uzalishaji ili fedha zinazopatikana zielekezwe katika huduma za kijamii kama vile elimu, afya na maji”, aliongeza Dkt. Bashiru.
 
Kwa upande wa suala la nidhamu ,Dkt. Bashiru alisema kuwa kumekuwepo na mabadiliko makubwa kwa watumishi wa Umma ambapo wafanyakazi wanahi kazini, kutumia lugha nzuri na kupunguza vitendo vya kudai rushwa.
 
Alimpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa juhudi anazozifanya za kukusanya mapato na kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha hizo na alimtaka asilegeze kamba katika kusimamia eneo la uzalishaji.
 
Alisema kuwa jitihada hizo ndio zimesaidia Shule kifurika wanafunzi kutokana na elimu bure, ongezeko la madawati mashuleni na mafanikio katika sekta ya afya na kilimo.
 

AZAM SPONSOR FEDERATION CUP KUENDELEA KESHO DES. 3, 2016


asfc
RAUNDI ya Tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam 2016 (Azam Sports Federation Cup 2016) inatarajiwa kuendelea kesho Desemba 3, 2016 kwa michezo minne itakayokutanisha timu nane zilizofanya vema raundi ya kwanza na pili.
Michezo ya kesho ambayo itakuwa mubashara (live),  kupitia chaneli mbalimbali za Kituo cha Televisheni cha Azam ‘Azam Tv’ itakuwa ni kati ya Mtwivila ya Iringa na Jangwani ya Rukwa mchezo unaotarajiwa kufanyika mkoani Iringa wakati Stand ya Bagamoyo itacheza na Mbuga ya Mtwara kwenye Uwanja wa Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
Stand Misuna ya Singida inatarajiwa kuwa wenyeji wa Kabela City ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida wakati Mulusagamba ya Kagera na Baruti ya mkoani Mara zitachuana kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera katika mfululizo wa mechi hizo.
Mechi hizo zitatoa timu nne bora kutoka mabingwa wa Mkoa na hivyo kuungana na timu 24 za Ligi Daraja la Pili kwa michezo ya hatua ya raundi ya nne na tano kutafuta timu nane bora zitakazosonga mbele kukutana na timu za Daraja la Kwanza.

MAJALIWA AZUNGUMZA NA WALIMU WA ARUSHA


wali
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Walimu wa Arusha kwenye    ukumbi wa Simba katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) Desemba 2, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
wali-1
 Walimu wa Arusha jana walifurika kwenye ukumbi wa Simba katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kumsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  katika mkutano kati yake na wo aliouitisha. Pichani, baadhi ya walimu wakiwa wamekaa kwenye ngazi na sakafuni baadaya viti kujaa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

MAJALIWA AKUTANA NA WAFANYABIASHARA WA ARUSHA


waf
Baadhi ya wafanyabiashara wa Arusha wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye Ukumbi wa Simba katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, Desemba  2, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
waf-1
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wafanyabiashara wa Arusha kwenye Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC) Desemba 2, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

CHUO CHA ARDHI CHATOA ZAWADI KWA WANAFUNZI 104 WALIOFAULU.


ardhi
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. Idrissa Mshoro (katikati kulia) akiteta jambo na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma), Prof. Gabriel Kassenga(katikati kushoto), pembeni kulia ni Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho (Mipango, Fedha na Utawala),Prof. Robert Kiunsi, pembeni kushoto ni Maafisa Waandamizi wa chuo hicho. Shughuli hizo zimefanyika leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
ardi-1
Mmoja kati ya washindi wa jumla wenye alama za juu, Anyighwile Lwijiso akipokea zawadi kutoka kwa mmoja wa wafadhili ambao ni Kampuni ya Hightech System mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi. Shughuli hizo zimefanyika leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
ardi-2
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. Idrissa Mshoro akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa chuo na wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma wakati wa shughuli za ugawaji wa vyeti na zawadi kwa wanafunzi waliofaulu masomo mbalimbali uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
…………………..
           Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chuo Kikuu cha Ardhi kimetoa zawadi na tuzo kwa wanafunzi 104 waliofanya vizuri kitaaluma ili kutoa hamasa kwa wanafunzi wengine kuweka juhudi katika masomo.
Zawadi hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrissa Mshoro ambaye ametangaza kuwa jumla ya wanafunzi wanne kati ya waliofanya vizuri wamepata alama sawa hivyo kuibuka washindi wa jumla kwa mwaka 2016.
      
Akisoma hotuba wakati wa sherehe hizo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma), Prof. Gabriel Kassenga amesema kuwa sherehe hizo zimekuwa zikiwezeshwa na wadau mbalimbali waliojitoa kwa hali na mali kutoa zawadi na tuzo kwa wanafunzi waliofaulu vizuri kwenye vipengele mbalimbali vya taaluma hivyo amewasihi wadau hao kuendelee kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wanafunzi hao ili kuwashawishi wanafunzi wengine kufanya vizuri.
“Zawadi mbalimbali zinazotolewa na wafadhili zimekua zikiwasaidia wanafunzi hawa kuongeza tija kwenye maisha yao ya kielimu na kiuchumi kwani wengi wao wamekuwa wakizitumia fedha hizo kama mitaji ya kufanyia biashara pindi wamalizapo masomo yao,”alisema Prof. Kassenga.
Amefafanua kuwa mwaka huu umekuwa wa tofauti kwani idadi ya wanafunzi wanawake na wanaume waliopata tuzo hizo iko sawa tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo wanawake walikua wakiongoza kwa asilimia 3.7 kwa kupata tuzo nyingi wakati wanaume wakiwa ni asilimia 2.2.
Prof. Kassenga ametaja baadhi ya zawadi zilizotolewa na wafadhili walioshiriki katika shughuli hiyo kuwa ni vyeti, Kompyuta mpakato (laptop),vifaa vinavyotumika katika kupimaji wa ardhi pamoja na fedha taslimu.
Aidha, Prof. Kassenga ametoa rai kwa kwa wanafunzi wote waliomaliza chuoni hapo kuwa juhudi walizokuwa wakizionyesha wakati wa masomo waende wakaziendeleze katika jamii zinazowazunguka pamoja na kwenye shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa ili wakawe mfano bora kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Emily Elandogo ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi waliopewa zawadi hizo amewashukuru walimu wa chuo hicho kwa elimu wanayoitoa ambayo itakua ni chanzo cha kuwaletea maendeleo sehemu yoyote watakapokuwa pia ametoa ushauri kwa wanafunzi wenzake kuitumia vizuri elimu waliyoipata ili iweze kuwasaidia katika maisha yao. 
Mahafali ya Kumi ya chuo hicho yanategemewa kufanyika Disemba 3 mwaka huu katika viwanja va chuo hicho ambapo wahitimu wa shahada mbalimbali watatunukiwa stahili pamoja na vyeti vyao. 
                         MWISHO

RC SINGIDA AWAAGA VIJANA WAHADZABE 43 WANAOENDA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA JESHI


rcc
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida Bw. Buhacha Baltazar Kichinda ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya utawala na rasilimali watu akiwaaga Vijana 43 wanaojiunga na kambi ya JKT Makutopora kikosi cha KJ 834 kwa hiyari kwa mkataba wa miaka ya miwili. Bw. Kichinda amesema wakiwa jeshini watafundishwa uzalendo, ukakamavu, stadi za jamii na nidhamu, amewaasa wazazi kuwapeleka shule wanafunzi na kupokea fursa kama za jeshi.
rc-1
Afisa Tawala ofisi ya Mshauri wa Mgambo Rhinocerus Magembesoni akiwaasa vijana 43 wa kihadzabe wakipanda mabasi kuelekea katika kambi ya JKT Makutopora kikosi cha KJ 834 kujiunga na kikosi hicho kwa hiyari kwa mkataba wa miaka ya miwili mara baada ya kuagwa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida. Jamii ya kihadzabe huendesha maisha yao kwa kuwinda na kula nyama pori, matunda ya porini, asali na mizizi.
rc-2
Vijana 43 wa kihadzabe wakipanda mabasi kuelekea katika kambi ya JKT Makutopora kikosi cha KJ 834 kujiunga na kikosi hicho kwa hiyari kwa mkataba wa miaka ya miwili mara baada ya kuagwa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida. Jamii ya kihadzabe huendesha maisha yao kwa kuwinda na kula nyama pori, matunda ya porini, asali na mizizi.
rc-3
Mmoja wa kijana wa kihadzabe Zuhura Ramadhani Longa ambaye alikuwa akiwasindikiza vijana wenzake wanawinda na kurina asali, amesema ameamua kujiunga na jeshi ili aweze kuisaidia familia yake lakini pia aweze kulitumikia taifa.
rc-4
Vijana 43 wa kihadzabe wakipunga mikono kuonyesha utayari wa kujiunga na kambi ya JKT Makutopora kikosi cha KJ 834 kwa hiyari kwa mkataba wa miaka ya miwili mara baada ya kuagwa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida. Jamii ya kihadzabe huendesha maisha yao kwa kuwinda na kula nyama pori, matunda ya porini, asali na mizizi.
rc-5
Vijana wa kihadzabe ambao walikuwa wanawinda na kurina asali, wamesema wameamua kujiunga na jeshi ili waweze kusaidia familia yake lakini pia waweze kulitumikia taifa.

CHAMA CHA TBN CHATOA SHUKURANI KWA BENKI YA NMB KWA KUKUBALI KUWA MDHAMINI WA MKUTANO WAO.


nbc
Kwa niaba ya Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini ‘Tanzania Bloggers Network’ (TBN) napenda kuwashukuru kwa kujitokeza katika mkutano huu muhimu. TBN inajua kuwa mnamajukumu mengi ya kuujuza umma masuala anuai, lakini mmechagua kuja kwetu ili kutusikiliza tulichowaitia na baadae tunaamini mtaujuza umma juu ya tukio letu.
TBN iliosajiliwa rasmi na Serikali mwezi Aprili, 2015 kwa kushirikiana na wataalam wa masuala ya habari na mitandao ya kijamii imeandaa semina kwa wanahabari hawa wa mitandao ya kijamii hasa ‘Bloggers’ itakayofanyika jijini Dar es Salaam. Semina hii maalumu ambayo itajumuisha mafunzo ya siku mbili yaani tarehe 5 na 6 ya Mwezi Desemba, 2016 kwa washiriki takribani 150 kutoka Tanzania nzima (Bara na Visiwani) itafuatiwa na mkutano mkuu kwa wanachama hai wa TBN kujadili masuala mbalimbali ya chama na tasnia nzima ya mitandao ya jamii.
Ndugu Wanahabari,
Katika mkusanyiko huu wanatasnia watapewa semina juu ya uendeshaji mitandao ya jamii kwa manufaa, upashaji habari kwa kutumia mitandao yao kwa kuziangatia maadili na namna ya kunufaika na mitandao hiyo kwa waendeshaji (kujipatia kipato) hasa ukizingatia kuwa wapo baadhi yetu tunaifanya kama ajira nyingine. Kimsingi lazima tukubali kuwa mitandao hii imekuwa tegemeo kubwa la kusambaza habari mbalimbali tena kwa muda mfupi tangu kutokea kwa tukio fulani, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuwapiga msasa wanaoiendesha ili kupunguza matumizi mabaya ya mitandao hii.
TBN inaamini njia pekee ya kupambana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ni kuendelea kutoa elimu kwa waendeshaji na watumiaji ili mwisho wa siku wasikubali kutumika vibaya au kuitumia vibaya mitandao hii katika kutoa taarifa. Kwa dunia ya sasa hakuna atakayepinga kuwa mitandao hii imekuwa ikielimisha umma, ikikosoa jamii na kiburudisha juu ya masuala anuai ya kijamii.
TBN inapenda kutoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Nne na Tano chini ya Mh. Rais John Pombe Magufuli kwa ushirikiano alioanza kuuonesha hasa kwa kutambua mchango wa mitandao hii ya kijamii na hata kuitumia katika utoaji wa taarifa zao. Kimsingi hii ni hatua nzuri na ya kuigwa hasa katika ulimwengu huu ambapo dunia imekuwa kama kijiji kutokana na hatua ya maendeleo ya habari na mawasiliano.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kulitambua hili mnaweza kuona hata taasisi nyeti kama Ikulu nayo ina Blogu maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma, Idara ya Habari Maelezo nayo ina Blogu kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma juu ya masuala mbalimbali yanayopaswa kutolewa kitaarifa kwa jamii. Jambo la kujivunia zaidi kwa maendeleo ya mitandao hii hata Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Nape M. Nnauye amekuwa mstari wa mbele kuona umuhimu wa mitandao ya kijamii hasa blogu na hata kuzitumia katika kupasha habari umma. Hata katika mkutano wetu wa kesho kutwa ndiye tunayemtarajia kuwa mgeni rasmi atakayetufungulia mkutano huo.
Ndugu Wanahabari,
Kwa namna ya pekee TBN inapenda kutoa shukrani za pekee kwa Benki ya NMB kwa kukubali kuwa wadhamini wa kuu wa mkushanyiko huo wa ‘bloggers’ kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa yetu. Kitendo cha kujitolea kufanikisha jambo hili kinaonesha namna gani NMB inavyowajali wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo hili la upashanaji habari kwa jamii.
Kama hiyo haitoshi tunapenda kuwashukuru wadhamini wengine ambao ni NHIF, SBL, PSPF na Coca Cola ambao wamejitolea kuungana nasi katika kufanikisha tukio hili la kuwaleta pamoja bloggers na kutoa mafunzo kwao. Tunaamini tutakuwa nao siku zote katika masuala mengi ya maendeleo ya tasnia ya mitandao ya kijamii.
Imetolewa na; Mwenyekiti wa Muda wa TBN
Joachim E. Mushi
0756469470