WIMBO “CHURA” WA SNURA MUSHI WAFUNGIWA, AFUNGIWA PIA KUFANYA MAONESHO
Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Zawadi Msalla (katikati) akisisitiza
jambo kwa waandishi wa habari (hawapopichani) wakati akitoa tamko la
Serikali kuhusu kusitishwa kwa wimbo wa Msanii Snura Mushi ujulikanao
kwa jina la Chura kwa kukiuka maadili kushoto ni Mwanasheria wa wizara
hiyo Bw. Patrick Kipangula na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Utamaduni Bibi. Lily Beleko.


……………………………………………………………………………………………………..
Serikali imesitisha wimbo na
Video ya Muziki wa Chura wa Msanii Snura Mushi kuchezwa kwenye vyombo
mbalimbali vya habari kuanzia leo mpaka pale msanii huyo atakapoifanyia
marekebisho video ya wimbo huo.
Usitishwaji huo umetokana na maudhui ya utengenezwaji wa Video hiyo ambayo haiendani na maadili ya Mtanzania.
Pia Serikali imesitisha maonyesho
yote ya hadhara ya mwanamziki huyo mpaka pale atakapo kamilisha
taratibu za usajili wa kazi zake za Sanaa katika Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA).
Serikali inawataka wasanii
kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi zao za Sanaa. Wafikirie
wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale
wanaowadhalilisha, Waelewe kwamba Sanaa si uwanja wa kudhalilisha watu
hata kidogo..
Aidha Serikali imechukizwa na
kazi hiyo ambayo si tu inadhalilisha tasnia ya Muziki bali inadhalilisha
utu wa mwanamke na inaifanya jamii kuanza kuhoji hadhi ya msanii,
weledi na taaluma ya Sanaa kwa ujumla.
Serikali inawakumbusha wananchi
wote kutokujiingiza katika makosa ya sheria ya mtandao kwa kusambaza
wimbo huu kwa njia yoyote ile ya kimtandao
Pia inavitaka Vyombo vya habari
viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya Sanaa kabla ya kuwa
mawakala wa uharibifu wa jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa.
Serikali inatoa wito kwa wasanii
wote kuzingatia maadili ya Kitanzania kabla ya kutoa kazi zao kwani
haitawavumilia ‘wasanii’ wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya
Sanaa kuwa sehemu ya uvunjifu wa maadili.
Imetolewa na Zawadi Msalla
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni