Serikali yakamata kilo 140 za dawa za kulevya nchini
Dar es Salaam.
Serikali imefanikiwa kukamata
takribani kilo 139.69 za dawa za kulevya ikiwemo kilo 53.49 za Heroin,
Cocaine kilo 86.2 kuanzia mwaka 2015 mpaka Aprili mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo
vya habari kutoka Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya
iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Elimu, Habari na Takwimu wa tume
hiyo, Amani Msami, pia tume hiyo imekamata tani 97 za bangi na mirungi.
Alisema mbali na kukamata kilo
hizo, takwimu zinaonesha kuwa watumiaji wa Heroin nchini wanakadiriwa
kuwa kati ya 200,000 hadi 425,000 ambapo kati ya hao 30,000 hutumia dawa
hizo kwa njia ya kujidunga sindano.
“Serikali imefanikiwa kukamata
takribani kilo 53.49 Heroin, Cocaine kilo 86.2 kuanzia mwaka 2015 mpaka
Aprili mwaka huu” alisema Msami na kuongeza kuwa:
“Watumiaji wa Heroin nchini
wanakadiriwa kuwa kati ya 200,000 hadi 425,000 ambapo kati ya hao 30,000
hutumia dawa hiyo kwa njia ya kujidunga”.
Msami alifafanua kuwa mbali na kukamata dawa hizo, tume hiyo ilikamata tani 81.3 za bangi na Mirungi tani 15.7.
Aliongeza kuwa mbali na hayo
idadi ya watuhumiwa waliyokamatwa wakijihusisha na usafirishaji wa dawa
za kulevya zikiwemo Bangi,Mirungi, Heroin na Cocaine walikuwa 14,503.
Hata hivyo, alisema takwimu hizo
zinaonyesha jitihada za serikali katika kukabiliana na biashara ya dawa
za kulevya nchini na si ukubwa wa usafirishaji wa Heroin na Cocaine
nchini.
“Moja ya jitihada za Serikali
katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya ni kutungwa kwa Sheria
ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Na.5 ya mwaka 2015.”
Alisema Msami.
Alifafanua kuwa sheria hiyo
imeweka adhabu kali kwa makosa ya kujihusisha na matumizi na biashara ya
dawa ya kulevya ikiwemo kifungo cha maisha kwa yeyote atakayesafirisha
dawa za kulevya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni